Mwenyekiti wa chama cha wananchi CUF Prof Ibrahim Lipumba amewateua wakurugenzi wapya pamoja na wajumbe wa kamati ya Utendaji wa chama hicho kufuatia kutengua uteuzi wa baadhi ya wakurugenzi na wajumbe upande wa Zanzibar waliokaidi wito wa kushiriki kikao cha kamati ya Utendaji makao makuu ya chama hicho Buguruni jijini Dar es Salaam.
Prof.Lipumba amewataja aliowateua kuwa ni pamoja na Nasor Seif kuwa Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi ambae pia atamsaidia Mkurugenzi wa haki za binadamu na sheria, Haroub Mohamed Shamis Naibu Mkurugenzi wa fedha na Uchumi, Khalifa Mohammed Khalifa Katibu wa Ulinzi na Usalama na Naibu Mkurugenzi mambo ya nje.
Wengine ni Abdul Kambaya anayekuwa Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano ya Umma na Naibu wake ni Masoud Ali Said, pamoja na Thiney Juma Mohamed anaekuwa Kamanda Mkuu wa Blue Guard huku pia akiwaonya wale waliotenguliwa kutojishughulisha na nafasi zao.
Aidha Prof.Lipumba amemwagiza Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho kuitisha kikao cha kamati ya Utendaji kesho kwa ajili ya kujadili masuala mbali mbali ya chama hicho na kutoa wito kwa wanachama kukijenga chama hicho badala ya kukibomoa.
No comments :
Post a Comment