Na Abdi Shamnah
KUWEPO kwa usafiri wa ndege ya Abiria ya Airbus A350 kutoka Shirika la Ethiopian Airlines, na kuunganisha safari zake hadi Zanzibar, kutapanua wigo wa ujio wa watali nchini.
Ndege hiyo mpya yenye uwezo wa kuchukua abiria 345, iliyoundwa kwa teknolojia ya juu zaidi, ni ya kwanza Barani Afrika, ambapo kwa mara ya kwanza imewasili katika Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume, jana ikitokea mjini Addis Ababa, Ethiopia – Kilimanjaro – Zanzibar.
Lengo la safari hiyo, ni kuitangaza ndege hiyo, ikiaminika itakuwa na mchango mkubwa katika uimarishaji wa sekta ya utalii nchini.
Akizungumza mara baada ya kuwasili kwa ndege hiyo, Meneja Mauzo na wakala wa huduma, Tawi la Zanzibar, Mohammed Mansour, alisema watalii wengi duniani wanapenda kusafiri na mashirika ya ndeeg yenye uhakika na usalama wa safari.
Alisema kuja kwa ndege hiyo kutawahamaisha watalii duniani kote, kufika Zanzibar na kutembelea vivutio mbali mbali vya utalii viliopo.
Mapema Meneja wa Masoko wa Ethiopian Airlines, Eshetu Fikadu alisema ndege ya A350 imetengenezwa kwa teknolojia ya hali ya juu zaidi, ikikidhi viwango vyote na yenye kuleta faraja kwa marubani, wafanayakazi pamoja na abiria wakati wa safari.
Alisema Shirika la Ethiopian Airline limekuwa likitowa huduma zake kwa zaidi ya nusu karne sasa Barani Afrika, na kuyafikia maneo mbali mbali, ikiwemo yale yenye vivutio vya utalii.
Alisema kuwepo kwa ndege hiyo, ambapo safari zake nchini zinategemea na mahitaji yatakavyokuwa, kutawafanya watalii kutoka mataifa mbali mbali barani Ulaya na Mashariki mbali, kuunganishwa na ndege hiyo na kuzuru Zanzibar.
Ndege ya A350, ina uwezo wa kuchukua abiria 315 wa daraja la kawaida (Economy) pamoja na abiria 30 wa daraja la kwanza.
No comments :
Post a Comment