Watoto wanne wamekutwa ndani ya gari lililokuwa limeegeshwa eneo la Jang’ombe, Mkoa wa Mjini Unguja.
Watoto hao wote walio na umri usiozidi miaka miwili na nusu walipotea nyumbani kwao tangu Jumapili asubuhi na hawakuonekana tena hadi jioni walipokutwa kwenye gari hilo jekundu wakiwa wameshafariki dunia.
Watoto hao ni Haytham Mustafa Abubakar, mwenye umri wa miaka miwili, Muslim Hamza Bakari (2), Dodo Mohamed Malali (miwili na miezi sita) na Munawar Ahmed Khamis (miwili na miezi sita).
Watoto hao, ambao walikuwa wakiishi Jang’ombe mjini Unguja, walizikwa jana makaburi ya Mwanakerekwe.
Maswali yaliyoibuka ni namna gani waliingia ndani ya gari, kama milango ilikuwa wazi au imefungwa na iwapo hakukuwa na mtu yeyote wakati watoto hao wakiingia ndani ya gari hilo.
Kamanda wa polisi wa mkoa, Hassan Nassir Ali alisema watoto hao walikutwa ndani ya gari aina ya Toyota Vitz.
Amina Mohamed Haroun, ambaye ni mzazi wa marehemu Haytham, alikuwa akijiuliza maswali kuhusu vifo hivyo alipohojiwa na Mwananchi.
“Sijui vipi wanangu hawa wameingizwa ndani ya gari hiyo na kusababisha kifo chao kwa kuwa si kawaida yao kufanya hivyo,” alisema.
“Tena jambo kubwa linalosikitisha, tulikwenda hadi kwenye gari hilo lakini hatukuwaona mara moja.”
Amina pia amepoteza mtoto wa ndugu yake aitwaye Dodo Mohamed Malali katika tukio hilo.
Amina alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kufuatilia kwa undani tukio hilo ili kubaini chanzo cha vifo vya watoto wao.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo walisema mpaka sasa hawajabaini chanzo cha watoto hao kuingia katika gari hiyo kwa kuangalia umri wao.
Ahmed Hamisi, ambaye ni mzazi wa Munawar, alisema waliwapata watoto hao saa mbili usiku na kwamba gari hilo limekuwa eneo hilo kwa muda mrefu kwa kuwa mmiliki amesafiri.
Hamis alisema alishirikiana na majirani kuvunja milango ya gari hilo na kufanikiwa kuwatoa watoto hao wakiwa wameshafariki.
Maryam Juma Mohamed, ambaye ni jirani wa familia za watoto hao, alisema awali watoto hao walionekana kiwanjani kwake wakicheza na kuna wakati walikuwa wakipigana.
“Baada ya kuwaona wanapigana kutokana na sababu zao za kitoto tuliwaamulia na ndipo walipoondoka sehemu hiyo na kutafuta sehemu nyingine. Hatukuwa na wasiwasi nao kwa kuwa ni jambo la kawaida wao kuranda mtaani kisha wanarudi nyumbani kwao,” alisema.
Alisema ilichukua kama saa tatu tangu walipoonekana uwanjani kwake kabla ya familia za watoto kuingiwa na wasiwasi.
Alisema walishirikiana kwa pamoja na wazazi wa watoto hao kuwasaka sambamba na kupeleka taarifa vituo vya polisi, bandarini na maeneo mengine kuhusu kupotea kwao.
“Tulihangaika sana hadi usiku lakini tulishindwa kuwaona. Ila ghafla tukiwa tumekaa karibu na eneo linalolazwa gari, tukasikia sauti kama mara tatu hivi inasema ‘watoto wamo ndani ya gari jekundu’. Tulihamanika kusikia sauti hiyo, ijapokuwa tulikuwa na wasiwasi mkubwa na sauti hiyo inayotoka wakati mtoaji hatujamjua nani. Lakini tulikwenda hadi kwenye gari na kuwakuta watoto hao wakiwa wanatokwa na mapovu mdomoni,” alisema.
Sheha wa Shehia ya Jang’ombe, Khamis Ahmada Salum alisema walifanya jitihada ikiwa ni pamoja na kufika eneo la maegesho ya magari, lakini hawakuwaona.
“Inashangaza kusikia watoto hao wameonekana ndani ya gari hilo wakati sisi tuliangalia zaidi ya mara tatu ndani. Ijapokuwa gari lina vioo vyeusi, tuliangalia lakini hatukuwaona. Mimi kusikia wameonakana humo, inanishangaza sana,” alisema sheha huyo.
Akizungumzia hilo, Kamanda Ali alisema kuwa Jeshi la Polisi litafanya mahojiano na wamiliki wa eneo hilo pamoja na mmliki wa gari hilo ambaye kwa sasa inadaiwa kuwa yuko Tanzania Bara.
Daktari wa zamu wa Mnazi Mmoja aliyewapokea watoto hao, Dk Makame Zubeir Chinjo alisema walifikishwa hospitalini hapo wakiwa tayari wameshafariki dunia.
Alisema uchunguzi wa awali umebaini walifariki baada ya kukosa hewa ndani ya gari.
No comments :
Post a Comment