STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 07.08.2017
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amesisitiza haja ya kuwaandaa viongozi wa michezo hapa nchini watakaoendelea kuipa sifa Zanzibar katika sekta hiyo kama ilivyokuwa hapo siku za nyuma.
Dk. Shein aliyasema hayo leo, alipokutana na uongozi wa Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo pamoja na Bodi ya Wakurugenzi ya Baraza la Michezo na Uongozi wa Baraa la Michezo katika vikao vinavyoendelea Ikulu mjini Zanzibar.
Katika vikao vya leo, Dk. Shein kwa nyakati tofauti alikutana na Uongozi wa Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo, Bodi ya Wakurugenzi ya Baraza la Sanaa na Sensa ya Filamu ya Uongozi wake, Bodi ya Wakurugenzi ya Baraza la Michezo na uongozi wake pamoja na Bodi ya Wakurugenzi ya Baraza la Kiswahili na uongozi wake.
Dk. Shein katika maelezo yake alieleza kuwa hatua hiyo itapelekea kuwapata viongozi bora wa michezo hatua ambayo itasaidia hata kupunguza migogoro inayotokea katika vyma na vilabu vya michezo hapa nchini.
Aliongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuona umuhimu wa suala hilo katika sekta ya michezo katika chuo chake kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kimeweza kuanzisha kada inayohusiana na michezo ambayo hutoa mafunzo juu ya masuala yote ya michezo ikiwemo uongozi.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alitoa pongezi kwa uongozi na Bodi hiyo ya Baraza la Michezo kwa kuendeleza vyema juhudi za ujenzi wa viwanja vya michezo katika Wilaya zote hapa nchini ambapo kwa upande wa Wilaya ya Kusini kiwanja cha Kitogani kiko ukingoni kumaliza ujenzi wake.
Nae Waziri wa Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo Rashidi Ali Juma alitoa pongezi zake kwa Rais Dk. Shein kwa juhudi zake alizozianza tokea kuwa Rais wa Zanzibar katika kuhakikisha sekta ya michezo inapata mafanikio na kuimarika zaidi.
Waziri Rashid alieleza kuwa umefika wakati vilabu viweze kuwezeshwa na kuahidi kuwa uongozi wa Wizara yake utaandaa mipango kwa lengo la kupata fedha kwa ajili ya kuendeshea michezo hatua ambayo itawavutia na hata wafadhili watakaokuja kuunga mkono sekta ya michezo hapa nchini.
Alieleza kuwa wananchi walio wengi hapa Zanzibar wanapenda michezo na wako tayari kuchangia michezo jambo linalotakiwa ni kuweka mikakati katika kuhakikisha sekta hiyo inaimarika ikiwa ni pamoja na kutoa viingilio katika viwanja vya michezo kwa wingi na kutolea mfano kiwanja cha Gombani Pemba jinsi wananchi wapenda michezo wanavyojaa kwa wingi.
Nae Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee kwa upande wake alisisitiza haja ya kuwepo viongozi makini katika sekta ya michezo
Aidha, aliongeza kuwa michezo ni gharama hivyo ni lazima kuwepo vyanzo vya fedha kwa ajili ya kugharamia michezo.
Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Said Hassan alieleza haja ya kuibua vipaji kwenye michezo sambamba na kupata usimamizi mzuri huku akieleza haja ya kuwepo kwa vituo vya kuendeleza michezo.
Mapema, Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Zanzibar (BTMZ), Sharifa Khamis Salim alieleza kuwa Baraza kwa kushirikiana na Afisi ya Mrajis linatioa muongozo juu ya mambo mbali mbali kwa Vyama na Vilabu vya michezo na kuchukua hatua za kinidhamu kwa mujibu wa kanuni za Usajili wa vyama vya michezo za mwaka 2014.
Aidha, akieleza miongoni mwa mafanikio Mwenyekiti huyo alisema kuwa Chama cha Viziwi kimepata uwanachama wa Shirikisho la mpira wa miguu la Afrika ya Mashariki la viziwi (DEFA) na Rais wake anatoka Zanzibar.Pia, Zanzibar ni mwanachama wa Shirikisho la Kimataifa la Viziwi la mpira wa miguu (DIFA).
Wakati huo huo, Dk. Shein alikutana na uongozi wa Wizara hiyo pamoja na Bodi yake ya Wakurugenzi ya Baraza la Sanaa na Sensa ya Filamu pamoja na uongozi wa Baraza hilo alieleza haja ya kuwatunza wasanii wa zamani na kuwaenzi wale wa hivi sasa.
Pia, Dk. Shein alieleza azma ya Serikali ya kuitengeza studio mpya iliyopo Rahaleo kwa lengo la kuwainua vijana katika maisha yao huku akieleza haja kwa Wizara kufanya utaratibu wa kuwatunza wasanii wakiwemo waibaji, waigizaji na hata wapiga vyombo.
Akieleza haja ya kuimarisha utamaduni wa hapa nchini Dk. Shein alisisitiza kuwa kuna umuhimu wa kudhibiti mmongonyoko wa maadili hapa nchini.
Nae Mwenyekiti wa Baraza hilo, Bi Mariama Hamdani alieleza mafanikio na changamoto za Baraza hilo
Aidha, aliongeza kuwa Baraza limeweza kufanya ukaguzi wa kazi za sanaa 30 za filamu na 136 za muziki na kufanya jumla ya kazi za sanaa zilizokaguliwa kufikia 172 na kati ya hizo 5 zilizuiliwa kuoneshwa hadharani na kazi 7zimezuiliwa kuoneshwa hadharani na hata faragha kutokana na kwenda kinyume na maadili ya Zanzibar.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments :
Post a Comment