AZIMIO LA ZANZIBAR
Tamko la Vyama vya Siasa vya Upinzani Vilivyokutana Zanzibar tarehe 16 -18 Desemba, 2018 KUTAFAKARI Khatima ya Demokrasia Nchini Tanzania.
SISI, Viongozi na Wanachama waandamizi wa Vyama vyetu sita vilivyosaini tamko hili, tumekutana hapa Zanzibar Disemba 16 – 18 kufanya tafakuri na kujadili juu ya dira yetu kama Taifa. Mkutano huu maalum wa Kihistoria ni taswira juu ya namna hali ya Demokrasia yetu ilivyoharibika, na hivyo kututaka kukaa chini kuja na mkakati mpya na wa pamoja wa kupambana na hali husika. Kwa masikitiko tuliwakosa Viongozi wenzetu katika kikao chetu, Kiongozi wa Kambi Upinzani Bungeni, Mhe. Freeman A. Mbowe, pamoja na Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Mhe. Tundu A. Lissu, mmoja akiwa mahabusu, na mwengine akiuguza majeraha ya kupigwa risasi. Tunafurahi kuwa wote wawili wametoa Baraka zao kwa kikao chetu hiki.
TUNATAMBUA kuwa, Tanzania hivi sasa ina mmomonyoko wa DEMOKRASIA, kwa ishara zote za Utawala wa Udikteta, usiojali haki za kisiasa, kijamii pamoja na za kiuchumi kwa wananchi; ikiwemo kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa mwaka 2015 ambao CCM walishindwa; kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara na maandamano ya vyama vya siasa kinyume kabisa na Katiba na sheria; kutekwa na kukamatwa kwa wananchi, wakiwemo viongozi wa kisiasa, waandishi wa habari na wafanyabiashara, kuokotwa kwa miili ya watu kwenye fukwe mbalimbali nchini; jaribio la kuuawa kwa Mbunge Mhe. Tundu A. Lissu na hatua ya Vyombo vya Ulinzi na Usalama kukataa kufanya uchunguzi wowote wa maana juu ya tukio hilo; uwepo wa sheria mbaya za Habari na Takwimu, pamoja na uletwaji wa kanuni za uendeshwaji wa Asasi za Kiraia (AZAKI), Kanuni za Sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Mswada wa mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa.
TUNATAMBUA kuwa, pamoja na kuwa Katiba inalinda mfumo wetu wa Vyama vingi, Dola sasa inaendeleza VITA dhidi ya vyama vya upinzani pamoja na wote wanaonekana wana mawazo mbadala juu ya namna nchi yetu inavyoendeshwa. Imekuwa ni kawaida sasa kwa Mkuu wa Nchi yetu, pamoja na wafuasi wake, kuwaita viongozi na wanasiasa wa vyama vya upinzani, pamoja na wakosoaji wa serikali kuwa ni ‘Mawakala wa Nchi za Nje’ na si Wazalendo. Vita hiyo ya Serikali dhidi ya wote wenye mawazo mbadala imegusa kila kundi la kijamii nchini – Wanahabari, Wamiliki wa Vyombo vya Habari, AZAKI, Wakulima, Wavuvi, Wafugaji, Wafanyabiashara, Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi, Wafanyakazi, Wanafunzi wa Elimu ya Juu, Wanadiplomasia, Viongozi wa Dini, Wanawake, na hata wanachama wa CCM yenyewe.
TUNASHUHUDIA kuanguka kwa UCHUMI wa nchi yetu, jambo ambalo linawaumiza zaidi wananchi masikini. Pamoja na juhudi za propaganda za serikali kuonyesha kuwa hali ya uchumi ni nzuri kinyume na hali mbaya iliyoko, tunaona ni muhimu kueleza kwa uwazi kuwa baada mwelekeo mzuri kiasi wa hali ya uchumi wa nchi yetu kwa miaka kumi, hali ya uchumi wetu imeharibika katika kipindi cha miaka hii mitatu tu ya awamu ya tano.
TUNATAMBUA kuwa tunao WAJIBU kama viongozi na raia wa nchi yetu, wa kushirikiana na wananchi wenzetu kuitoa nchi yetu kutoka katika hali mbaya tuliyonayo sasa, pamoja na kujenga na kupanua zaidi demokrasia yetu, ili ikidhi matakwa na matarajio ya watu wetu. Tunao wajibu wa kutoa dira kwa wananchi. Tunasema SASA BASI, IMETOSHA.
TUNATANGAZA kuwa, sasa ni wakati sahihi na muhimu wa kuongeza UMOJA, MSHIKAMANO na KUJITOA kwetu katika kuiendea ajenda yetu hii ya kitaifa ya kulinda Demokrasia yetu na kuupinga udikteta huu, jambo hili ni ajenda ya watanzania wote, ni zaidi ya maslahi ya vyama vyetu vya siasa. Jambo hili litahitaji ujasiri pamoja na kupambana na vitisho na madhara yote yatokanayo na dola, ni jambo litahitaji msisitizo juu ya mshikamano wetu hata pale nguvu kubwa ya kutuvunja na kutugawa itakapotumika, ni wakati wa kusisitiza umoja na kila kundi la kijamii.
TUNAWATANGAZA rasmi wenzetu, Freeman Mbowe na Esther Matiko, ambao mpaka sasa wako mahabusu, kuwa ni WAFUNGWA WA KISIASA, na tangazo husika halitafutwa mpaka pale watakapoachiwa. Tutapambana kuhakikisha kuwa wao na wafungwa wenzao wote wa kisiasa, nchi nzima, wanapewa nafasi ya kupata haki katika mfumo ulio huru, mbele ya mahakama na mbele ya macho ya umma.
TUNAENDELEZA msisitizo wetu wa kutokuitambua Serikali ya sasa ya Zanzibar, na kwamba ni SERIKALI HARAMU. Matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa mwaka 2015 uliofutwa kinyume na Katiba na Sheria yalionyesha kuwa wananchi wa Zanzibar waliopewa nafasi ya kujiamulia khatima yao waliamua kukichagua chama cha CUF na viongozi wake kuwa Viongozi wao.
TUNAUTANGAZA mwaka 2019 kuwa ni MWAKA WA KUDAI DEMOKRASIA, mwaka ambao tutapambana kuzidai haki zetu zote tunazonyimwa kinyume na sheria na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kama vyama vya siasa vyenye uhalali na vyenye utaratibu uliowekwa rasmi kisheria na kikatiba, tutatangaza rasmi namna na utaratibu wa kufanya mikutano yetu ya hadhara katika kila kona ya nchi yetu, hatutaruhusu katazo haramu na lisilo na mashiko ya kisheria litumike kutuzuia kutekeleza wajibu wetu.
TUNAWAPA ARI wanachama na wafuasi wetu, pamoja na wananchi wote kwa ujumla, wakati ni sasa wa kuondoa khofu, kushikamana nasi katika kulinda Demokrasia ya nchi yetu. Hatupaswi kuwa waoga, hatupaswi kujisalimisha katika kudai haki zetu kama mtu mmoja mmoja na kama kundi zima la kijamii. Tutaupeleka ujumbe huu wa Uhuru na Demokrasia kwa viongozi wenzetu wote, wa vyama vyote, katika majimbo na kata zote nchini, kama ishara ya mshikamano wetu.
TUTAUNDA Kamati ya kuratibu, pamoja na mambo mengine, hatua za kuunganisha makundi ya wananchi nchi nzima, ambapo kundi lolote la wananchi, popote walipo, iwe ni wafanyakazi wanaopinga kupunjwa pensheni, wakulima wanaokosa soko la mazao yao, wavuvi wanaonyanyasika, wanafunzi wanaokosa mikopo, wanasiasa wa upinzani wanaokamatwa na polisi bila sababu nk, watafikiwa ili kuwa na mkakati wa pamoja wa kupigania haki zao.
Maalim Seif Sharif Hamad – Katibu Mkuu, CUF.
James Francis Mbatia – Mwenyekiti Taifa, NCCR Mageuzi
Oscar Emanuel Makaidi - Mwenyekiti Taifa, NLD
Salum Mwalimu – Naibu Katibu Mkuu – Zanzibar,
CHADEMA
Hashim Rungwe Spunda – Mwenyekiti Taifa, CHAUMMA
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto – Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo
Zanzibar, Disemba 18, 2018.
This comment has been removed by a blog administrator.
ReplyDeleteSuper site! I am Loving it!! Will return once more, Im taking your food likewise, Thanks.also read
ReplyDeletemassage and myotherapy australia,
Very nice blog post. I absolutely love this website. here is the best site to give you 8 ball pool rewards 8 ball pool rewards apk
ReplyDelete