Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jonathan Shanna ameeleza juu ya tukio la kupotea kwa Mkuu wa Chuo cha Nyakato Islamic Institute kilichopo chini ya Taasisi ya Elimu ya The Registered Trustees of Islamic, Sheikh Bashir Gora na kudai jeshi linaendelea kumtafuta.
Kamanda Shanna amesema ni kweli wamepokea taarifa za kupotea kwa Sheikh huyo hivyo ameagiza kufungwa kwa mipaka yote ya Mkoa wa Mwanza ili kuhakikisha kiongozi huyo anapatikana mapema iwezekanavyo.
"Ni kweli tumezipata taarifa za kupotea kwake, lakini unajua mtu akipotea huwezi kujua tatizo ni nini, na hatujui kwanini hapatikani na tumemtafuta kila mahali hapatikani, tumeshafunga mitambo yetu kwenye maeneo yetu yote."
Akizungumza hivi karibuni, Katibu wa Bodi wa taasisi hiyo, Sadik Mchola alisema tukio hilo lilitokea Disemba 6 chuoni hapo ambapo alikuja kijana mmoja kuulizia nafasi za kujiunga na chuo kwaajili ya mdogo wake.
“Kijana huyo alitukuta ofisini, Sheikh akamwambia aje Januari mwakani atapewa utaratibu, kijana aliondoka lakini baada ya muda kidogo akarudi tena kuulizia malipo, Sheikh akamwambia Januari ndiyo tutakueleza kila kitu, akaondoka."
“Baada ya hapo wakawa wanazungumza na Sheikh huku anamsindikiza kumbe walikuwa wameegesha gari yao nyuma ya chuo walipoikaribia, alitoka kijana mwingine kwenye gari hiyo wakambeba Sheikh na kumuingiza ndani kisha gari likaondoka kwa speed (mwendo) mkali,” alisimulia.
No comments :
Post a Comment