KUHUSU KUHAIRISHWA KWA UTOAJI WA HUKUMU YA SHAURI NA. 23/2016 SIKU YA JUMANNE YA TAREHE 15 JANUARI, 2019:
THE CIVIC UNITED FRONT
(CUF – Chama Cha Wananchi)
TAARIFA KWA UMMA
TAREHE: 12/1/2019
Kutokana na Msajili wa vyama vya siasa Jaji Francis Katabazi Mutungi kufungua shauri jipya Na. 97/2018 dhidi ya Bodi halali ya Wadhamini ya Chama chetu, chini ya hati ya dharura mno (CERTIFICATE OF EXTREME URGENCY), hukumu iliyokuwa imepangwa kutolewa siku ya Jumanne ya Tarehe 15 Januari, 2019 imehairishwa hadi Ijumaa ya Tarehe 22 Februari, 2019.
Shauri Na. 23/2016 ni shauri lililofunguliwa na Bodi ya Wadhamini ya CUF-Chama cha Wananchi mwezi Oktoba mwaka 2016 likihoji mamlaka na uhalali wa Msajili wa vyama vya siasa Jaji Francis Katabazi Mutungi, kumtambua Prof. Ibrahim Haruna Lipumba kuwa Mwenyekiti wa Chama licha ya kujiuzulu kwake mapema Tarehe 5/8/2015 na kuthibitishwa na Mkutano Mkuu wa Taifa Tarehe 21/8/2016 kwa kura 476 (ambazo ni sawa na asilimia 70% ya wajumbe wote wa Mkutano Mkuu).
Msajili wa vyama vya siasa alimrejesha Prof. Ibrahim Haruna Lipumba rasmi ofisi Kuu ya Chama Buguruni akiwa na genge la wahuni Tarehe 24/9/2016 kwa kuvunja milango chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi. Msajili wa vyama vya siasa alikubaliana na Jeshi la Polisi kutoa ulinzi kwa Lipumba kupitia barua Kumb. Na. HA.322/362/14/85 ya Terehe 23/9/2016 iliyopelekwa kwa IGP; kama ilivyokaririwa na barua nyingine Kumb. Na.HA. 322/362/88 ya Terehe 28/9/2016 iliyopelekwa kwa Lipumba. Hatua hiyo ya Msajili wa vyama vya siasa kumrejesha madarakani Lipumba kinyume cha Katiba ya The Civic United Front (CUF- Chama Cha Wananchi) ndiyo imezaa kinachoitwa mgogoro wa uongozi ndani ya Chama.
Shauri Na. 23/2016 lilisikilizwa na kukamilika Tarehe 8/10/2018 na mara ya kwanza lilipangiwa kutolewa hukumu Tarehe 12/10/2018 kabla ya kuhairishwa hadi Tarehe 30/11/2018. Hata hivyo kutokana na dharura ya Mahakama, hukumu hiyo ilihairishwa tena kwa mara ya pili na ikapangwa kutolewa siku ya Jumanne Tarehe 15/1/2019. Msajili wa vyama vya siasa kupitia ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali kwa uzembe hakutekeleza amri ya Mahakama ya kuwasilisha utetezi wake. Kwa hofu ya shauri kupata sura ya upande mmoja (Ex-parte) kisheria, Tarehe 24/12/2018 Msajili wa vyama vya siasa kupitia ofisi ya Mwanasheria Mkuu akafungua shauri Na. 97/2018 chini ya hati ya dharura mno akiomba kuruhusiwa kuwasilisha utetezi wake nje ya muda.
Chama kilipata fununu ya njama na nia ovu ya Msajili wa vyama vya siasa Tarehe 24/12/2018, mara baada ya Mahakama ya Rufaa kutupilia mbali rufaa ya Lipumba na genge lake dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu wa Tarehe 29/5/2018 uliozuia utoaji wa ruzuku ya Chama kwa Lipumba. Baada ya hukumu ya Mahakama ya Rufaa Msajili wa vyama vya siasa kupitia ofisi ya Mwanasheria wa serikali, alianza kuhaha kutafuta jinsi ya kukwamisha mchakato wa utoaji haki. Chama baada ya kupata taarifa za uhakika juu ya njama hizo, kiliwaagiza wasomi mawakili wake Juma Nassoro Dovutwa na Daimu Halfani kufanya maandalizi mapema na kijipanga kukabiliana na hujuma hiyo iliyokusudia kuisimamisha Mahakama Kuu kuendelea na mchakato wa utoaji hukumu kwa kipindi kirefu sana.
Tarehe 4/1/2019 saa 5.20 asubuhi, wakili wa serikali aliwapatia wasomi mawakili wetu nakala ya wito na nyaraka za shauri hilo jipya Na. 97/2018 wakitakiwa kufika mahakamani kulisikiliza siku hiyo hiyo ya Tarehe 4/1/2019. Itakumbukwa kuwa siku ya Ijumaa ya Tarehe 4/1/2019 ndiyo siku ambayo ilikuwa inasikilizwa kesi dhidi ya Muswada wa sheria ya vyama vya siasa iliyofunguliwa na Mhe. Joran Bashange, Mhe. Salim Bimani na Mhe. Zitto Kabwe. Mahakama Kuu mara baada ya kuhairisha usikilizwaji wa kesi Na. 31/2018 dhidi ya Muswada wa sheria ya vyama vya siasa, iliendelea kusikiliza shauri Na. 97/2018 la Msajili wa vyama vya siasa dhidi ya Bodi halali ya Chama. Wasomi mawakili wetu waliweza kusambaratisha njama na nia ovu ya Msajili wa vyama vya siasa kwa kukubali bila masharti Mahakama kuongeza muda kwa minajili ya kuruhusu Mwanasheria Mkuu wa serikali kuwasilisha utetezi wa Msajili wa vyama vya siasa nje ya muda jambo lililosababisha kuhairisha utoaji hukumu hadi Tarehe 22/2/2019. Kwa utaratibu huo njama za Msajili wa vyama vya siasa kuisimamisha Mahakama Kuu kuendelea na mchakato wa utoaji haki katika shauri Na. 23/2016 zilisambaratishwa.
Mwanasheria Mkuu wa serikali aliamriwa na Mahakama Kuu kuwasilisha utetezi wake (Reply Submissions) Tarehe 7/1/2019 na Chama kujibu (Rejoinder Submissions) Tarehe 10/1/2019.
Mwanasheria Mkuu wa serikali alitekeleza amri hiyo ya Mahakama na Wasomi Mawakili wetu kwa umahiri mkubwa walikamilisha majibu na kuyawasilisha (filed) Mahakamani mapema Tarehe 9/1/2019 ikiwa ni siku moja kabla ya muda uliotakiwa. Ni imani yetu kuwa sasa hakutakuwa na pingamizi tena la kutolewa hukumu Tarehe 22/2/2019.
WITO KWA WANACHAMA WOTE:
Bodi ya Wadhamini ya THE CIVIC UNITED FRONT [CUF-Chama Cha Wananchi] inawapongeza kwa dhati Wasomi Mawakili wetu kwa kazi na umahiri mkubwa katika kushughulikia shauri hili na mashauri mengine yote na kuwataka kuendelea na moyo wao wa uzalendo katika kutetea haki. Aidha inatoa wito kwa wanachama wote, wapenzi na wapenda demokrasia kwa kadri itakavyowezekana kuhudhuria kwa wingi Mahakama Kuu ya Tanzania Dar es Salaam siku ya Jumatatu ya Tarehe 18/2/2019 kupokea hukumu ya shauri Na. 13/2019 la Mhe. Ally Saleh dhidi ya RITA kuhusiana na Bodi ya Wadhamni na Ijumaa ya Tarehe 22/2/2019 kupokea hukumu ya shauri Na. 23/2016 juu ya uhalali wa Msajili wa vyama vya siasa kumtambua Prof. Ibrahim Haruna Lipumba kama Mwenyekiti wa CUF-Chama cha Wananchi.
Pamoja na wito huo, tunasisitiza kila atakayebahatika kuhudhuria mahakamani kuheshimu na kutunza taratibu za mahakama.
CUF NI TAASISI IMARA, YENYE VIONGOZI MAKINI.
HAKI SAWA KWA WOTE
Imetolewa na Kurugenzi ya Habari CUF-Taifa
SALIM BIMANI
MKURUGENZI WA HABARI
+255 777 414112
+255655 314112
MBARALA MAHARAGANDE
NAIBU MKURUGENZI WA HABARI
maharagande@gmail.com
+255715 062577
+255767 062577
No comments :
Post a Comment