Nimeulizwa na watu wengi sana juu ya maoni yangu kuhusu Mzee Edward Ngoyai Lowassa kurudi CCM. Nilisema nasubiri hili vumbi la hizi siku chache zilizopita litulie kwanza, ndipo niweze kusema maoni yangu. Sasa ni muda muafaka kufanya hivyo.
Mzee Edward Lowassa mwenyewe amesema amerudi 'nyumbani.' Maana yake ni kwamba alikuwa 'ugenini' tangu Julai 2015. Hakutuhonga wala hakununua Chama chetu kama tulivyotukanwa huko nyuma.
Tulimkaribisha na kumpatia majukumu ya kutuongoza kwenye mapambano ya 2015. Na alitekeleza majukumu hayo vizuri kwa kadri alivyoweza, na kadri tulivyomwezesha. Matunda ya kazi yake, na ya kazi yetu, yanajulikana.
Sasa mwendo wa 'ugenini' umemshinda. Misalaba ya upinzani imekuwa mizito sana. Ameamua kurudi 'nyumbani' kupumzika.
Pengine sasa mkwe wake anayeozea Gerezani Keko atapata nafuu mahakamani.
Pengine sasa atarudishiwa shamba lake la Handeni na Ranchi ya Dodoma; na wataacha kumsumbua juu ya mashamba mengine ambayo wamekuwa wanatishia kumnyang'anya.
Pengine sasa TRA wataacha kumwandama na madeni ya kodi yasiyolipika kama yale matrilioni ya makinikia Acacia Mining.
Na pengine sasa wataacha kumtishia kumnyang'anya mafao yake ya kisheria kama Waziri Mkuu mstaafu.
Badala ya kumlaani kwa kuondoka kwetu 'ugenini', mimi namtakia kila la kheri na mapumziko mema 'nyumbani' kwake. Sisi tutaendelea na safari yetu ya Canaan.
No comments :
Post a Comment