TAREHE 24 NI SIKU YA KUIPIGANIA DEMOKRASIA TANZANIA:
MSIMAMO WA NGOME YA VIJANA KUHUSIANA NA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA WA TAREHE 24 NOVEMBA 2019.
Ngome ya Vijana ya ACT Wazalendo inaungana na msimamo wa Chama cha ACT Wazalendo na vyama vingine vya upinzani kwa kujitoa kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika tarehe 24 Novemba 2019.
Uchaguzi huu umevurugwa kwa kiwango cha kutisha kwenye kila hatua hivyobasi haupaswi kuruhusiwa kuendelea. Mathalani, kwenye hatua ya kutunga kanuni, Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) iliyapuuza na kuyatupa mapendekezo yote yaliyotolewa na vyama vya upinzani.
Kwenye hatua ya kuandikisha wapigakura, baada ya kuona mwitikio mdogo wa wananchi, wasimamizi wa uchaguzi kwa baraka ya TAMISEMI walilivuruga zoezi la kuandikisha wapiga kura kwa kuongeza wapiga kura wasio na sifa na kupika takwimu za wapiga kura ili kujenga picha kuwa waliojiandikisha ni wengi.
Kwenye hatua ya kuchukua na kurejesha fomu za kugombea ndipo uharamia mkubwa zaidi umejitokeza. Wagombea wa upinzani wenye sifa wameenguliwa na wagombea wa CCM ikiwemo wasio na sifa wamepitishwa bila kupingwa. Kwa hakika huu si uchaguzi bali ni uchafuzi!
MSIMAMO WA NGOME YA VIJANA.
1. Tunaunga mkono msimamo wa Chama wa kujitoa kwenye uchaguzi huu ambao umevurugwa kwa kiwango kikubwa. Kwa hakika, kushiriki uchaguzi huu ni kuhalalisha ubakwaji mkubwa wa demokrasia jambo ambalo ACT Wazalendo hatupo tayari kulifanya.
2. Tunavipongeza vyama nane vya upinzani (CHADEMA, ACT wazalendo, NCCR Mageuzi, CHAUMMA, CCK, UPDP, NLD na CUF) kwa msimamo madhubuti wa kujiweka kando na uchaguzi huu. Ni matumaini ya vijana kwamba hatua hii ya vyama hivi itafuatiwa na hatua ya kushikamana na kudai kwa pamoja demokrasia na Tume Huru ya Uchaguzi.
3. Tarehe 24 Novemba 2019 inapaswa kuwa siku ya kupigania demokraisia Tanzania. Vijana tupo tayari kwa mapambano. Tunasubiri mwongozo wa viongozo wetu kadiri watavyoona inafaa.
4. Tunalikumbusha Jeshi la Polisi kuwa maandamano ni haki ya kikatiba ya wananchi. Waache kutisha raia kuwa iwapo wataandamana watashughulikiwa na Polisi. Ni dhahiri kuwa vyama vyote vya upinzani vilivyosimamisha wagombea vimejitoa kwenye uchaguzi na kuiacha CCM peke yake. Jeshi la Polisi halina sababu ya kutishia kusambaza polisi mitaani kutisha watu kwenye kampeni ambazo hazipo.
5. Iwapo CCM kitavunja sheria na kufanya kampeni kwenye uchaguzi ambao haupo, nasi vijana tutaingia kwenye kampeni ya kuhakikisha uchaguzi kwenye maeneo ambayo tumeshajitoa haufanyiki. Tutafanya hivi ili kuilinda taratibu za kisheria ambazo zipo wazi kuwa iwapo vyama vingine vikijitoa na kubaki mgombea wa Chama kimoja, uchaguzi hauwezi kufanyika.
6. Ngome ya Vijana inafanya mawasiliano na Jumuiya za Vijana za Vyama vingine makini vya upinzani ili kwa pamoja tuhamasishe vijana nchini na wananchi kwa ujumla kutekeleza wajibu wao wa kuitetea na kuipigania demokrasia siku ya tarehe 24 Novemba 2019.
7. Tunatoa onyo la mara ya mwisho kuwa TAMISEMI iache kutuchokoza zaidi vyama vya upinzani kwa kulazimisha kuweka majina ya wagombea wa vyama vya upinzani ambao wao na vyama vyao wamejitoa kwenye uchaguzi. Huu ni uchokozi wa wazi ambao hatutauvumilia.
8. Tunaungana na vyama vya upinzani na wadau wa demokrasia nchini kudai Tume Huru ya Uchaguzi. Tunampongeza Rais Mstaafu Benjamin Mkapa kwa kueleza waziwazi kwamba nchi inahitaji Tume Huru ya Uchaguzi na uhuru wa kufanya siasa. Ingawa mfumo wa uchaguzi umekuwa na dosari kubwa tangu awamu za nyuma ikiwemo enzi za Rais Mkapa, lakini CCM ilikuwa inashindana na kuiba uchaguzi kwenye sanduku la kura. CCM ya sasa ya Rais Magufuli, Dk. Bashiru Ally na Humprey Polepole inaogopa uchaguzi kama ukoma na haitaki kushindana na vyama vingine vya upinzani. Ni CCM dhaifu kuwahi kutokea tangu mfumo wa vyama vingi uanzishwe.
Bonifasia Mapunda, Naibu Katibu, Ngome ya Vijana, ACT Wazalendo.
Tarehe 16 Novemba 2019.
No comments :
Post a Comment