Vyama saba vya siasa kutoka upinzani ikiwemo Chadema, ACT, Chaumma, NCCR, CCK, NLD, UPDP Jumamosi ya leo kupitia kwa makamu mwenyekiti Chadema Abdallah Safari, wametoa tamko lao lenye mambo makuu matano kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa ambao utafanyika Novemba 24, 2019.
TAMKO LA VYAMA VYA ACT-WAZALENDO,CHAMA CHA KIJAMII (CCK), CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA),CHAMA CHA UKOMBOZI WA UMMA (CHAUMMA),NCCR-MAGEUZI,NLD NA UPDP-KUHUSU UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA, 2019.
UTANGULIZI
Uchaguzi wa serikali za mitaa ulitangazwa kufanyika tarehe 24.11.2019 na baada ya tangazo hilo Vyama vyetu vilishiriki kwenye michakato mbalimbali ikiwemo kuandikisha wapiga kura, kuteua wagombea na wagombea kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali .Ilipofikia zoezi lakuchukua fomu ndipo maeneo mengi ya nchi tukashuhudia wagombea wa vyama vya upinzani wakinyimwa fomu za kugombea kwa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi kufungaofisi na kuondoka na au kuwaambia kuwa wanasubiri kupatiwa fomu kutoka kwa wasimamizi wa uchaguzi.
Kwenye baadhi ya maeneo ambako wagombea walifanikiwa kuchukua na kurejesha fomu za kugombea nafasi mbalimbali ilipofika siku moja kabla yasiku ya uteuzi tulianza kushuhudia wagombea wetu wakienguliwa bila kufuatwakwa Kanuni na taratibu za uchaguzi, wengine fomu zao kughushiwa kwa kuongezewa herufi mbele ya majina yao waliyokuwa wamejaza kwenye fomu au tarakimu kwenye kipengele cha tarehe za kuzaliwa nk
Wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi walitumia sababu mbalimbali ambazo walizisababisha wao kwa kuharibu fomu za wagombea kama kigezo cha kuwaengua bila hata kusubiri wagombea hao kuwekewa mapingamizi na wagombea wa vyama vingine jambo lililopelekea zaidi ya asilimia 95% ya wagombea wetu wote waliofanikiwa kurejesha fomu kuenguliwa kugombea nchi nzima .
Baada ya hali hiyo vyama vya Chadema,ACT-Wazalendo, Chaumma,CCK,NCCR-Mageuzi,CUF, UPDP na NLD vilitoa matamko ya kujitoa kwenye uchaguzi huo kutokana na Ukiukwaji Mkubwa wa Kanuni na Sheria zinazosimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Baada ya Vyama tajwa kujitoa kushiriki uchaguzi huo, serikali kwa upande wake ilitoa matamko mbalimbali ambayo yalikuwa yakitofautiana na kujichanganya pamoja na ukweli kuwa yalikuwa yakitolewa na mtu mmoja ambaye ni Waziri wa TAMISEMI Mhe. Suleman Jaffo.
Baada ya wagombea wa vyama tajwa kujitoa kwenye uchaguzi huo wagombea wake waliwajulisha wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi kuhusu kujitoa kwenye uchaguzi na kwa ngazi ya Taifa baadhi ya Vyama vilimjulisha waziri wa TAMISEMI kwa barua kuhusu kujitoa kwao katika kuendelea na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2019.
Baada ya vyama kujitoa ilisababisha wagombea ambao watasalia katika uchaguzi huu kuwa wa chama kimoja pekee cha CCM nchi nzima .
MAELEKEZO YA KANUNI ZA UCHAGUZI WA VIONGOZI WA MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MITAA NGAZI YA VIJIJI, VITONGOJI NA MITAA ZA MWAKA 2019.
i.) Kanuni ya 18 na 19(1)imeweka utaratibu kuwa endapo siku ya uteuzi kutakuwa na mgombea mmoja aliyejitokeza katika kuomba nafasi ya uenyekiti na mwombaji huyo akateuliwa , msimamizi msaidizi wa uchaguzi atamtangaza mwombaji huyo kuwa ni mshindi wa nafasi aliyoomba kugombea kwa kupita bila kupingwa .ii.) Kanuni ya 19(2)inaeleza hivyo hivyo kwa wajumbe wa serikali ya mtaa au kijiji kuwa watatangazwa kupita bila kupingwa endapo hakutakuwa na wagombea wa vyama vingine .
iii.) Kanuni ya 20(1) imeweka utaratibu wa wagombea kujitoa baada ya uteuzi kufanyika . Nanukuu “Endapo ,baada ya uteuzi kufanyika ,mgombea aliyeteuliwa kugombea nafasi ya Uenyekiti wa Mtaa atajitoa,Msimamizi msaidizi wa uchaguzi atatengua uteuzi wa mgombea huyo…..’
iiii.) Kanuni ya 20(2) inaweka wazi kuwa, ‘Endapo ,baada ya uteuzi kufanyika ,mgombea aliyeteuliwa kugombea nafasi ya Uenyekiti wa Mtaa atajitoa na kubaki mgombea mmoja wa nafasi hiyo,Msimamizi Msaidizi wa uchaguzi atamtangaza mgombea aliyebaki kuwa mshindi wa nafasi iliyoombwa kwa kupita bila kupingwa’
v.) Kanuni ya 20(3) imeweka utaratibu kama huo kwa wagombea wa nafasi za ujumbe wa serikali za Mitaa na Vijiji wa kupita bila kupingwa.
vi.) Kanuni ya 27(2) imeweka utaratibu wa kuvitaka vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi huo kuwasilisha ratiba za kampeni kwa msimamizi wa uchaguzi siku saba (7) kabla ya siku ya kampeni .Baada ya vyama vyetu kujitoa hatukuwasilisha ratiba za kampeni na hivyo hatupo kwenye ratiba hiyo.
MSIMAMO WA VYAMA VYETU
1) Hatutashiriki kwa vyovyote vile kwenye Kampeni na uchaguzi huu unaoenda kinyume na kanuni za uchaguzi, na hivyo tunawataka wanachama , wafuasi na wapenda amani wote katika taifa letu kutokushiriki katika kampeni na kinachoitwa uchaguzi .2) Uchaguzi huu ufutwe na mchakato wake uanze upya kwa mustakabali wa amani ya taifa letu.
3) Tunauomba Umma wa watanzania ujiandae kwa maelekezo yoyote yatakayotolewa baada ya mashauriano yanayoendelea miongoni mwa Vyama na makundi mengine ya kijamii .
4) Tunataka mchakato wa kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi ambayo itakuwa na jukumu la kusimamia chaguzi zote nchini uanze mara moja.
5) Tumetambua kauli na wito uliotolewa na baadhi ya viongozi wastaafu na viongozi wa dini nchini , hivyo tunawaomba wachukue hatua za kuingilia kati mapema kuinusuru amani ya Taifa letu.
Tamko hili limetolewa leo tarehe 16, Novemba 2019.
No comments :
Post a Comment