Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, February 2, 2020

JUMA DUNI HAJJI ATOA MSIMAMO MZITO WA ACT WAZALENDO!


*VITISHO DHIDI YA NDUGU ZITTO KABWE.*

Chama cha ACT Wazalendo kimefadhaishwa na pia  kimesikitishwa sana na kitendo cha matumizi mabaya ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania dhidi ya Kiongozi wa Chama chetu cha ACT Wazalendo Ndugu Zitto Kabwe na tunachukulia kila neno lilotoka dhidi yake kwa tahadhari mno.

Juzi tarehe 31 Januari 2020 Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ndugu Job Ndugai aliwaongoza wabunge wa Chama cha Mapinduzi kutumia Bunge kumjadili, kumkejeli na kumdhihaki Ndugu Zitto Kabwe kwa kitendo chake cha kishujaa cha kuiandikia Benki ya Dunia kuitaka izuie mkopo kwa Serikali ya Tanzania wa kusaidia elimu hadi hapo itapohakikisha kuwa inaweka mazingira ya wanafunzi wa kike wanaopata ujauzito kuendelea na masomo.  Mbunge wa kuteuliwa na Rais Ndugu Abdallah Bulembo alikwenda mbali zaidi na kupendekeza kuwa Ndugu Zitto Kabwe auwawe.

Sisi ACT Wazalendo tumejiridhisha bila shaka kuwa kulikuwa na nia ovu, kwani bila hata Mbunge yoyote yule kupendekeza au walau kutamka tu kuwa suala hilo liende nje ya Bunge, Spika Ndugai alimpa maelekezo Mwanasheria Mkuu Professa Adeladus Kilangi kwa kusema kuwa suala hilo lina ujinai na kumtaka kulifanyia kazi, kwa maana ya kumuundia mashtaka Ndugu Zitto.

Kitendo cha Spika Ndugai kutoa maelekezo kwa Mwanasheria Mkuu ni kuingilia kazi isiyokuwa yake na kuvuka mipaka ya mamlaka yake na kuingilia muhimili mwengine, lakini pia ni dhihirisho kuwa hapatakuwa tena na haki katika suala hilo.

CCM inatumia nguvu kubwa katika suala hili la elimu ya mtoto wa kike ambaye pengine si kwa hiari na matakwa yake amepata uja uzito, jambo ambalo lilikuwa ndani ya Ilani ya chama hicho, lakini ikapindishwa na matamshi ya Rais John Pombe Magufuli na sasa wanaona kuwa hawana kabisa uwezo wa  kuitetea kwa sababu umma hauoni mantiki wala hoja ya kumzuia mtoto asipate fursa ya elimu, maana Tanzania haitakuwa nchi ya kwanza kufanya hivyo, na mfano halisi tunao hapa hapa Tanzania huko Zanzibar.

CCM imetambua kuwa hoja hii itawaandama kisiasa kwa sababu akili na mantiki inakataa kuwanyima fursa ya elimu watoto wa kike ambao ndio msingi wa taifa hili katika kuondoa ujinga na msingi katika ujenzi wa taifa kiuchumi na kimandeleo. ACT Wazalendo tutalisimamia jambo hili kwa gharama yoyote.

MSIMAMO WETU:

1. Spika Ndugai amelidhalilisha Bunge. Kwa mara nyingine, Spika wa Bunge Ndugu Job Ndugai amedhihirisha UDHAIFU wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ndugu Zitto Kabwe amefanya kazi ya kizalendo katika kuiwajibisha Serikali ambayo kimsingi ndiyo kazi ya Bunge. Badala ya kumsakama Ndugu Zitto kwa sababu za kuokoteza, Bunge lilipaswa kupitisha azimio la kumpongeza kwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo. 

ACT Wazalendo tunajivunia kwa jinsi Kiongozi wetu alivyojitolea kupigania elimu ya mtoto wa kike. Kwenye barua yake, Ndugu Zitto hajazuia mkopo wa Benki ya Dunia bali ameweka bayana kuwa Benki hiyo isiidhinishe mkopo kwa Tanzania hadi hapo itapohakikisha uwepo wa mfumo madhubuti wa wanafunzi wa kike wanaopata ujauzito kuendelea na masomo na kuzingatia haki za binadamu na demokrasia. Jee hili ni kosa la kuitwa msaliti, mhaini na malaya wa kisiasa?

Kama kweli Serikali inautaka mkopo wa Benki ya Dunia imeshindwaje kuzingatia madai ya Ndugu Zitto? Hoja hujibiwa kwa hoja na hoja haipigwi nyundo wala kujipanga kwa nia ovu. Serikali, ambayo mpaka mjadala huo ukifanyika Bunge ikiwa bado haijatoa tamko lolote lile, bila ya shaka ina nafasi ya kukutana na Benki ya Dunia na kutoa majibu ya kuridhisha ili mkopo huo utoke.

Tena hapo ikumbukwe kuwa Ndugu Zitto kama ingekuwa anataka kulifanya jambo hilo ni la kisiasa angeweza kuibua suala la madai ya Tume Huru ya Uchaguzi, Serikali kukinzana na Katiba na Sheria kwa kuzuia mikutano ya kisiasa, kuibua masuala ya kuandamwa na kudhuriwa viongozi wa kisiasa, haki za kiraia na fursa huru za kutoa maoni kukandamizwa, raia wa nchi hii kutekwa na kupotea bila kauli yoyote ile ya Serikali matendo ambayo yanahusishwa na wanaoitwa Watu Wasiojulikana, na hata Serikali kulifunga lango la Bunge kusikika kwa wananchi, na badala yake Bunge lenye kumsakama Ndugu Zitto, halisikiki kwa umma mpaka katika matukio ya kuchagua ndio huwa live.

 2. Chama cha ACT Wazalendo kimevichukulia kwa uzito mkubwa vitisho vya Wabunge wa CCM dhidi ya Kiongozi wetu Ndugu Zitto Kabwe. Tunawaeleza kuwa lolote lile baya likimkuta, watawajibika kikamilifu.

Chama chetu kimewaweka katika hali ya tahadhari wanachama wetu nchi nzima kumlinda Kiongozi wao kwa lolote.

3. Chama cha ACT Wazalendo kimefurahishwa na mshikamano mkubwa unaooneshwa na wanaharakati, asasi za kiraia, wanasiasa na wananchi kwa ujumla katika ajenda hii ya kuhakikisha elimu kwa watoto wa kike wanaopata mimba shuleni. Mshikamano huu uendelee hadi haki ya elimu ya mtoto wa kike ipatikane.

Juma Duni Haji,
Naibu Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo.
02 Februari 2020

No comments :

Post a Comment