AirFreight

Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Thursday, March 19, 2020

TAARIFA MPYA KUHUSIANA NA UGONJWA WA CORONA ZANZIBAR!



Tunasisitiza tena wananchi wapunguze hofu na badala yake wachukue tahadhari stahiki za kinga kwa kufanya yafuatayo:- · Kuendelea kunawa mikono mara kwa mra kwa maji ya kutiririka na sabuni au kutumia senitizer.. Kuziba pua na mdomo kwa kutumia kitambaa, tissue au kiwiko cha mkono pindi mtu anapopiga chafya au kukohoa halkadhalika wakati wa kupenga mafua. Naomba Jamii itoe taarifa kwa mtu yoyote mwenye dalili za maambukizi kwa wataalamu wa Afya.

SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR

OFISI YA MAKAMU WA PILI WA RAIS

Tel. 024 22 31126

Fax. 024 22 33788

P. O. Box 239

Vuga Street

Zanzibar-Tanzania

Taarifa kwa umma

Ndugu wananchi,

Kama mnayvoelewa hali ya mripuko wa Virusi vya Corona umeleta taharuki
kubwa duniani. Hadi sasa zaidi ya nchi 160 duniani zimesharipoti uwepo
wa virusi hivyo ambapo Bara la Afrika tayari zaidi ya nchi 25
zimeripoti uwepo wa virusi hivyo.

Kwa upande Afrika Mashariki tayari nchi tatu zimeshatangaza kuwa na
ugonjwa huo, kwa upande wa Tanzania Bara tayari tokea juzi wametangaza
kuwa na mgonjwa wa kwanza na leo mgonjwa mwengine Raia wa Marekani
naye amegundulika kuwa na virusi hivyo.

Hapa kwetu Zanzibar, siku ya jana tarehe 17 Machi, 2020, tulipata
washukiwa watatu wa ugonjwa huo, wawili wakiwa ni raia wa kigeni ambae
ni Mghana na Mjerumani na mwengine ni Mtanzania. Watu wote hao watatu
walikuwa na dalili ya ugonjwa huo na kama ilivyo kawaida hatua
zilichukuliwa za kuchukua sampuli kwa uchunguzi wa kimaabara.

Alfajir ya leo tulipokea majibu ya sampuli hizo ambapo kwa bahati
mbaya mmoja kati ya hao amekutwa akiwa ameathirika na maambukizo ya
kirusi cha COVID 19 ambaye ni Raia wa Ghana aliyeingia nchini kutokea
Ujerumani na Shirika la Ndege la Kenya Air way tarehe 11/3/2020 muda
wa saa 3:20 asubuhi. Mtu huyo ni mwanamme mwenye umri wa miaka 24.
Kwa sasa, mgonjwa huyu amelazwa katika kituo maalum kilichotengwa kwa
ajili ya maradhi ya mripuko huko Kidimni wilaya ya Kati Unguja kwa
ajili ya matibabu na hali yake inaendelea vizuri.
Kufuatia hali hiyo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekutana na
kuchukua hatua zifuatazo:-
1) Serikali inazifunga skuli zote za maandalizi, msingi, sekondari,
vyuo Vikuu pamoja na madrasa ili kupunguza uwezekano wa maambukizi ya
maradhi haya hadi hapo serikali itakapotoa tangazo jengine.

2) Serikali inazuia mikusanyiko inayokutanisha watu wengi kwa wakati
mmoja ikiwemo mikutano, makongamano, semina, warsha, michezo ya ligi
kuu, ligi za kanda pamoja na burudani za ngoma na shughuli za harusi
mpaka hali ya maradhi haya itakapotengemaa. Na kuhusu maziko utaratibu
utatolewa na viongozi wa taasisi za dini. Hata hivyo wito unatolewa
shughuli za maziko zihusishe watu wachache kadri iwezekanavyo

3) Serikali inawataka watu wote wanaoingia nchini kutoka nchi
zilizoathirika na maradhi hayo kufuata utaratibu wa kujitenga kwa
hiari kwa muda wa siku 14 kwa gharama zao wenyewe pamoja na kufuata
masharti ya afya.

4) Serikali inakataza na inakemea vikali utumiaji wa bandari zisizo rasmi kwa ajili ya kuchukua abiria na mizigo hivyo watu wote
wanatakiwa kutumia bandari rasmi, kama vile bandari ya Malindi, Mkokotoni kwa upande wa Unguja na Mkoani, Wete na Wesha kwa upande wa Pemba. Hata hivyo vyombo vitakavyotumika nje ya bandari zilizo rasmi
zitataifishwa na Serikali

5) Serikali inalaani vikali vitendo vya wafanyabiashara kutumia ugonjwa huu kwa faida zao kwa kupandisha bei za vifaa vya kinga, bidhaa na huduma nyengine na hatua kali zitachukuliwa kwa watakaobainika kufanya hivyo na tayari taasisi ya kumlinda mlaji imepewa agizo la kufuatilia suala hilo.

6) Serikali inazuia safari zote za nje ya nchi kwa watendaji wake na pia kwa wale watakaokuwa na ulazima wa kusafiri wanapaswa kuchukua hatua za kujilinda na maradhi hayo. Aidha, Serikali inawashauri
wananchi kwa wakati huu kuepuka safari zisizo za lazima za nje ya Zanzibar.

7) Serikali inawataka wananchi wote kuacha kusikiliza taarifa zisizo rasmi na badala yake wasikilize taarifa rasmi zitakazotolewa na
Serikali. kusikiliza utaratibu na taarifa zitakazotolewa na Serikali juu ya mripuko wa maradhi hayo ambazo zitakuwa zikitolewa mara kwa mara.

8) Serikali inashauri wananchi wanaokwenda masokoni na maeneo mengine ya kutafuta huduma kuepuka mikusanyiko na baada ya kupata huduma warudi majumbani.

9) Serikali inawataka wananchi kupunguza msongamano katika hospitali zetu badala yake watu wasiozidi wawili wataruhusiwa kumuona mgonjwa kwa siku na inashauriwa wananchi watumie vituo vya afya vilivyokuwa
karibu nao ili kuepuka msongamano katika hospitali kuu.

Kwa sasa tunawaomba wananchi kuendelea kuwa watulivu na kufuata miongozo inayotolewa na wataalamu wetu wa afya juu ya njia bora za kujikinga na ugonjwa huo, hasa ukizingatia ugonjwa huo umeshaingia nchini.

Tunasisitiza tena wananchi wapunguze hofu na badala yake wachukue tahadhari stahiki za kinga kwa kufanya yafuatayo:-

· Kuendelea kunawa mikono mara kwa mra kwa maji ya kutiririka na sabuni au kutumia senitizer.

· Kuziba pua na mdomo kwa kutumia kitambaa, tissue au kiwiko cha
mkono pindi mtu anapopiga chafya au kukohoa halkadhalika wakati wa kupenga mafua.

· Naomba Jamii itoe taarifa kwa mtu yoyote mwenye dalili za maambukizi kwa wataalamu wa Afya.

· Nasisitiza tena kama mtu atakuwa na dalili za ugonjwa huu tafadhali naomba abaki nyumani na apige namba ya simu zifuatazo; 0777454675, 0777 948426, 0777 461230 na 0773 787749.

Naomba wanahabari na wazanzibari wenzangu tushikamane na miongozo yote
inayotolewa na wataalamu wa Afya ili tubaki salama. MUNGU TUSAIDIE.

Imetolewa na Mhe. Hamad Rashid Mohammed,

Waziri wa Afya, Zanzibar.

18 Machi, 2020

No comments :

Post a Comment