Uchambuzi Urais Zanzibar 2020: Nafasi ya Maalim Seif Sharif Hamad!
Na Zanzibar Daily
Historia ya siasa za Zanzibar haiwezi kuandikwa ikakamilika bila kulitaja jina la Seif Sharif Hamad. Maalim ni mtu mmoja mwenye sehemu kubwa katika historia hiyo na kamwe hapuuziki.
Maalim alizaliwa tarehe 22 Oktoba mwaka 1943 huko Mtambwe Nyali kisiwani Pemba. Yeye ni mtoto wa pekee kwa mama yake Bi Time Seif Haji. Elimu yake ya awali kaipata katika Skuli za Uondwe na Wete Boys kabla ya kuhamia Sekondari ya King George VI Unguja ambako alihitimu mwaka 1963. Katika moja ya mahojiano yake na Kituo cha ITV tarehe 14 Novemba mwaka jana, Maalim ameeleza kuwa ndoto yake haikuwa siasa bali kufanya kazi serikalini kama mtumishi wa umma.
Hata hivyo maisha yana mipango yake kwani mwaka 1975 baada ya kuhitimu Shahada yake ya Kwanza katika Sayansi ya Siasa, Utawala wa Umma na Uhusiano wa Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Maalim akateuliwa kuwa msaidizi wa Rais Aboud Jumbe, na hapo safari yake ya siasa ikawa imeanza. Miaka miwili baadaye TANU na ASP viliungana kuanzisha CCM na Maalim akateuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM.
Ameshika nafasi nyingi katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar hadi kufikia ngazi ya Waziri Kiongozi, na katika CCM alifikia ngazi ya Mjumbe wa Kamati Kuu kabla ya kuvuliwa nafasi zote za uongozi na kufukuzwa katika chama hicho mwaka 1988. Maalim anaamini kufukuzwa kwake CCM kulitokana na majungu na tuhuma zisizo za kweli kumhusu yeye ambazo alipewa Mwalimu Nyerere (akiwa Mwenyekiti wa CCM).
Nyota ya Maalim ilianza kung’ara mapema sana kwenye uongozi Zanzibar na hilo huenda lilikuwa laana kwake badala ya baraka.Kilele cha fitna zilizomwondoa Maalim CCM na SMZ zilianza na Uchaguzi wa Rais Zanzibar mwaka 1985. Maalim akiwa na umri mdogo kisiasa wa miaka 42 akawa mmoja ya wagombea wenye nguvu katika uchaguzi huo na kushindanishwa na Idris Abdul Wakil. Katika kura za Halmashauri Kuu ya CCM, Maalim alipishana kwa kura chache sana na mzee Wakil. Mwenyewe Maalim anaeleza hakutaka jina lake kwenda Halmashauri Kuu kwani alimwambia Mwalimu Nyerere yeye anajitoa ili kumuunga mkono Wakil, hata hivyo Mwalimu alikataa. Uchaguzi ule inaelezwa ulizaa makundi makubwa mawili, moja la wazee walokuwa wakimuunga mkono Abdul Wakil wao wakaitwa The Liberators na jingine la vijana walokuwa wakimuunga mkono Seif, wakaitwa Frontliners.
Makundi haya mawili hayakuwa tu kuhusu uchaguzi huo lakini pia nguvu ya kila kundi katika siasa za Tanzania na Zanzibar baada ya Mwalimu kutangaza kuwa angeondoka madarakani mwaka huo wa 1985. Liberators wao walitaka Mwinyi kuwa Rais Bara badala ya chaguo la Mwalimu ambaye alikuwa Dk Salim Ahmed Salim, lakini pia kwa Urais Zanzibar hawakumtaka Maalim Seif.
Mvutano huo ukaendelea ambapo baada ya Abdul Wakil kupitishwa na CCM badala ya Maalim, Maalim kuonyesha umoja akatakiwa kufungua kampeni za Urais Zanzibar 1985 akimuunga mkono mzee Wakil, na hakika akafanya hivyo. Wakil alishinda lakini matokeo yalionesha wazi wananchi walimkataa mgombea huyo wa CCM. Maalim anaeleza kwamba Liberators waliamini yeye ndiye kahujumu chama Zanzibar na kuleta matokeo hayo mabaya hivyo Mwalimu alipomtaka kuwa Waziri Kiongozi kwenye serikali ya Wakil Maalim akataka kugoma kwani alidhani si vyema kufanya kazi na Rais asiyekuwa na imani nawe. Hata hivyo inaelezwa Mwalimu Nyerere alimlazimisha Maalim na akakubali.
Mwaka 1988 akiwa Waziri Kiongozi na Mjumbe wa Kamati Kuu CCM akaundiwa tume kuchunguwza tuhuma kwamba anakihujumu chama Zanzibar na yeye na wenzake nane wakatimuliwa CCM. Akatiwa misukosuko ya kutosha ikiwemo kesi ya uhaini na kufungwa gerezani kwa muda kabla ya kutolewa.
Toka hapo Maalim amekuwa kinara wa siasa za mageuzi Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Akiwa na CUF amegombea Urais Zanzibar mara tano mfululizo, 1995, 2000, 2005, 2010 na 2015 na mara zote amesema kwamba ameshinda uchaguzi lakini CCM na serikali wamempora ushindi. 2010 hali ikawa mbaya kiasi kamba ili kuzuia umwagaji damu Zanzibar ikabidi Maalim akubali serikali ya umoja wa Kitaifa na yeye kuchukua nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kabla ya kujiondoa baada ya Uchaguzi wa 2015.
Miaka ya karibuni Maalim akiwa Katibu Mkuu CUF na Mwenyekiti wake Profesa Lipumba wakaingia katika mgogoro mkubwa, Maalim akimtuhumu Lipumba kuwa kibaraka wa CCM anayelipwa kuitumia CUF kwa maslahi ya CCM. Baada ya tafakari ya muda Maalim na timu yake wakabwaga manyanga na kuhamia chama kipya kilichoanzishwa na Zitto Kabwe cha ACT Wazalendo.
Kama vile kubadili nguo, tukashuhudia asilimia kubwa ya CUF Zanzibar ikibadilika na kuwa ACT Wazalendo kuanzia wanachama hadi majengo. Bendera za CUF zikapotea Zanzibar zikapandishwa za ACT. Hivi sasa Maalim ni Mshauri Mkuu wa ACT Wazalendo. Swali kubwa wengi wanalojiuliza ni je, Maalim ana nafasi gani katika Uchaguzi Mkuu Zanzibar mwaka huu? Kiuhalisia hili ni swali lisiloepukika lakini pia gumu kuwa na jibu la moja kwa moja. Hapa chini tuchambue mambo machache yanayotoa mwanga wa majibu ya swali hilo.
Jambo la kwanza kutazama ni kwamba Maalim ameshiriki Uchaguzi Mkuu Zanzibar kama Mgombea Urais kwa mara 5 sasa, mwaka 1995, 2000, 2005, 2010 na 2015. Huu ni muda mrefu katika siasa na pengine mjadala mpana unaendelea ndani ya chama chake na nafsi yake iwapo ni sahihi kwake kugombea tena mwaka huu, kwa mara ya 6. Yaweza kuamuliwa Maalim agombee lakini kuna athari mbili, moja hii inaweza kutafsiriwa kama mapungufu kuwa haamini wako wengine wenye uwezo wa kuchukua nafasi yake na kwamba yeye ndiye mkuu mwenye uwezo na si mwingine yeyote (messiah mentality), pili inaweza kutafsiriwa kwamba katika miaka yote kakosa uwezo wa kukuza mtu anayeweza kuchukua nafasi yake na huo ni udhaifu kwani, kiongozi mwenye maono anapaswa kuzalisha pia viongozi wenye maono kwa kizazi kijacho (great leaders create leaders).
Jambo la pili ni umri wa Maalim Seif. Tarehe 22 Oktoba mwaka huu anatimiza umri wa miaka 77. Huu ni umri mkubwa kwa vipimo vya maisha yetu binadamu na pengine ni umri wenye changamoto nyingi kiafya. Miaka ya karibuni Maalim amekuwa akiugua hapa na pale na kulazwa hospitalini kabla ya kuruhusiwa. Japo haijawekwa wazi nini kinamsumbua lakini magonjwa mbalimbali ya uzeeni yaweza kuwa sababu. Maalim akigombea na kushinda mwaka huu akaapishwa kuongoza zanzibar atatoka madarakani akiwa na miaka kati ya 82 au 87. Mchambuzi yeyote mwenye akili timamu lazima kuona kwamba umri huu wa Maalim ni kikwazo kwake katika siasa mchakamchaka za Zanzibar kuanzia sasa na kuendelea.
Tatu, Maalim na timu yake wako katika chama kipya. Kuna dhana ya kutoaminiana kwa kiasi fulani hasa kwa wapiga kura. Wapo wanaohoji kama ni sahihi kwao kuwa ACT baada ya kuhama CUF. Suala la kuhamia ACT halihakikishi kwamba sasa kura zote za CUF nazo zitahamia ACT. Katika hili uhalisia ni kwamba Maalim kuondoka CUF kuna kura kaenda nazo ACT, zipo zilizorudi CCM, zipo zilizobaki CUF, na zipo ambazo bado hazijaamua wapi kwenda (swing).
Katika mambo haya matatu tunaona nafasi ya Maalim Seif katika siasa za mchakamchaka Zanzibar inaanza kupungua makali japo ushawishi wake unabaki kuwa mkubwa. ACT inaweza kuamua Maalim agombee lakini lazima itambue athari hasi zitakazoambatana na uamuzi huo. Iwapo itaamua hivyo uchaguzi huu utakuwa wa mwisho kwa Maalim Seif na utakuwa mgumu kwa pande zote. Mafanikio makubwa kwenye matokeo ya uchaguzi huo kwa ACT haitakuwa ushindi wa kiti cha Rais bali nafasi ya kuingia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kutawala Baraza la Wawakilishi. Hilo likitokea, ACT inaweza kujenga imani mbele ya mifumo na wananchi na ikaiondoa rasmi CCM Zanzibar 2025.
Inaweza pia ACT kuamua Maalim asigombee ikawekeza nguvu kwa makada wake kama Mansour Yussuf Himid au Othman Masoud Othman. Hawa hawawezi kushinda wala kufikia kishindo cha Maalim Seif lakini matokeo yake yataelezea hali ya siku za mbeleni za upinzani Zanzibar.
Iwapo hilo litatokea basi Maalim anaelekea kung’atuka walau katika siasa za kuwa mbele (active politics) za Zanzibar na kubaki kama mshauri mwongozo njia. Yote kwa yote ni kusubiri kuona mambo yatakavyokuwa.
No comments :
Post a Comment