Bismillahir Rahmanir Rahiim
SHURA YA MAIMAMU TANZANIA _Kamatikuuyasiasa.shura@gmail.com
WARAKA [MWONGOZO]
UCHAGUZI MKUU WA TAIFA
OKTOBA 2020 TANZANIA
Umetolewa leo Tarehe 09. 07. 2020.
UTANGULIZI
Ugonjwa wa Korona – COVID-19
Sote Tunafahamu kuwa nchini mwetu na Dunia kwa ujumla kumekuwepo na taharuki kubwa ya Ugonjwa wa Korona unaosababishwa na maambukizi ya virusi vya ugonjwa huo - COVID-19. Janga hili limesababisha vifo vingi duniani, zaidi ya watu 300,000 wamefariki na zaidi ya milioni saba wameambukizwa virusi vya maradhi haya.
Wakati Taifa letu likikabiliwa na janga hili, tumeshuhudia changamoto kubwa ya ombwe la uongozi katika kukabiliana nalo. Viongozi wa kisiasa na kiserikali wamekosa msimamo wa pamoja katika jambo hili zito. Hatua zao hazikuonesha kujali maisha ya wananchi. Taarifa za wataalamu wa afya zilipuuzwa na kugeuzwa jinai dhidi yao. Taarifa kuhusu ugonjwa huo zimeachwa hewani na sasa zimeelekezwa zaidi kwenye propaganda za kujijenga kisiasa bila ya kujali ukweli na maisha ya watu. Tabia hii imekuwa ikidhoofisha Taifa na linakosa maendeleo.
Leo hii ni miaka 59, tangu tupate Uhuru lakini katika tatizo hili la Corona tumeshindwa hata kuwapa wananchi kilo 50, za unga wa dona ili watulie kwa muda majumbani wakati Taifa likiendesha mikakati ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo hatari. Tunachojali zaidi ni maslahi binafsi ya kisiasa. Itakapofika wakati wa kampeni za uchaguzi, wanasiasa watajitokeza na kuwaambia wananchi wanawajali wawachague ili wawaletee maisha bora na maendeleo ya Taifa.
Uongozi unaoweza kuwaletea wanchi maisha bora na maendeleo ya Taifa ni ule unaoshirikiana na wananchi kwa dhati katika masuala yanayo wahusu wakati wa huzuni na furaha. Vilevile unaheshimu na kulinda haki zao ikiwemo ya uhai wao.
Ugonjwa huu ni janga kubwa wala si la kuomba, lakini kwa upande mwingine, huenda ni fursa aliyotuletea Mwenyezi Mungu ya kutafakari kuhusu uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu. Mwenyezi Mungu ametupa fursa ya kutafakari ili kuona viongozi wakweli wenye hekima ya kuyaendea mambo, busara, weledi, wenye utu na wanaofaa kupewa dhamana ya maisha ya watu na kuliongoza Taifa kwa ujumla.
Sisi kama Waislamu na Watanzania, tunatahadharisha wananchi wenzetu kwamba ugonjwa huu hatari upo, na kama yalivyo magonjwa mengine utaendelea kuwepo. Tunawaomba kuchukua tahadhari wakati wote na hatua sahihi za kujilinda zilizoelekezwa na Mwenyezi Mungu Subhanahuwataala. Vilevile maelekezo ya Shirika la Afya Duniani (World Health Organization-WHO). Pia, tunawakumbusha kuzingatia maelekezo ya wataalamu wetu wa Afya nchini na baada ya hatuwa hizo, tuendelee kumomba Mwenyezi Mungu kwa rehema zake, utukufu na uweza wake atunusuru na janga hili lililoikumba dunia. Tunawapa pole wale wote waliofikwa na misiba iliyotokana na janga hili na kulitakia nusra Taifa letu.
TUNATAKA UCHAGUZI HURU NA WA HAKI
Utangulizi
Mwaka huu Oktoba 2020, ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu na sisi tutashiriki kama Watanzania (na kama Waislamu kama tutakavyoona huko mbele). Kwa hakika maelezo yetu ya nini tunataka kwa taifa letu katika uchaguzi huu yangekuwa na maana sana kama Taifa lingekuwa na KATIBA MPYA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA TUME HURU YA UCHAGUZI vinavyotokana na Wananchi wenyewe.
Kwanini Katiba Mpya na Tume ni Muhimu: Mwaka 1961, Tanganyika Huru ilipata Katiba ya kwanza. Katikba hii haikupita katika mchakato ulio wahusisha wananchi bali ilipatikana kwa makubaliano ya wakoloni na Chama cha TANU. Wakoloni kupitia Bunge lao walitunga Katiba hiyo kama kiambatanisho cha Tanganyika Constitution Oder in Council 1961. Katiba Mpya ya pili ilikuwa mwaka 1962. Iliendeleza msingi uleile wa wanasiasa kuwaamulia wananchi.
Viongozi wa TANU ndio waliofanya maamuzi yote na Bunge (lililofanywa chombo cha chama) lilielekezwa kupitisha sheria mbalimbali na hatiamaye kuketi kama Bunge la Katiba lililoipitisha. Jambo jipya katia Katiba hiyo ilikuwa ni kukusanya madaraka yaliyokuwa ya Gavana na Waziri Mkuu na kumpa Rais. Rais akawa na mamlaka makubwa yanayo funika nafasi ya uwakilishi wa wananchi kama Bunge na mamlaka za haki kama mahakama. Msingi huo ndio unaotumiwa na serikali zote za Tanganyika mpaka sasa. Matokeo ya Katiba iliyopo imekandamiza uhuru na fursa ya wananchi kujenga na kuimarisha misingi ya Taifa lao.
Katika suala la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar tatizo ni lile lile la kikatiba na wanasiasa kuwaamulia Wananchi:
Tanganyika ilipata Uhuru wake kutoka kwa Waingereza mwaka 1961. Zanzibar ilipata Uhuru wake kutoka kwa Waingereza Desemba 10, 1963. Zanzibar ilipewa Uhuru huo baada ya uchaguzi wa nne wa kidemokrasia wa vyama vingi uliofanyika Julai 1963. Muungano wa Vyama vya ZNP-ZPPP ndio ulioshinda katika uchaguzi huo na kuunda Serikali. Siku thelathini baada ya Uhuru huo na ZNP-ZPPP kuunda Serikali, chama kilichoshiriki na kushindwa katika uchaguzi huo cha Afro Shiraz Part (ASP) kilifanya Mapinduzi ya damu na kuchukuwa Dola. (Kwa mujibu wa John Okelo Wazanzibari waliouliwa na wanamapinduzi wanafika 11,995).
Ilipofika Aprili 26, 1964, ikiwa ni miezi mine baada ya Serikali ya Zanzibar kupinduliwa, Rais wa Tanganyika Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kiongozi wa Mapinduzi Mzee Abeid Amani Karume walisaini hati ya kuunganisha Tanganyika na Zanzibar. Katika hatuwa hiyo kubwa iliyokuwa inahusisha kuchukuliwa mamlaka kubwa za mataifa hayo na kuyahamishia katika vuguvugu hilo la Mwalimu Nyerere na Mzee Karume wananchi hawakushirikishwa. Mamlaka yaliyokuwa yanahamishwa ni pamoja na Majeshi ya Ulinzi wa Mipakani, Jeshi la Polisi, Hali ya Dharura (Emergence Power), Uraia, Uhamiaji, Biashara ya Kimataifa, Mikopo ya Kimataifa, Madeni ya Kimataifa, Utumishi katika Serikali, Kodi, Ushuru, Bandari, Usafiri wa Anga, Posta na Simu. (Rais Nyerere kwa madaraka ya urais Presidential Decree alibadilisha jina la Katiba ya Tanganyika kuwa Katiba ya Muungano). Baada ya kusainiwa makubaliano ya Nyerere na Karume ndipo yalipopelekwa katika Bunge la Tanganyika na kuelezwa kuwa yamepata ridhaa ya Wananchi.
Baada ya hatuwa hiyo Watanganyika na Wazanzibari wanaishi pamoja chini ya Serikali iliyoundwa katika muktadha huo. Sehemu kubwa ya maisha yao imetawaliwa na migogoro mikubwa ya Kikatiba, Kimamlaka, Kiuongozi, Kiuchumi na Kisiasa. Migogoro hiyo inawaathiri kwa kiasi kikubwa katika maisha yao na kuzuwia maendeleo ya mataifa yao. Watu wote wenye fikra kubwa wametazama Katiba Mpya inayotokana na Wananchi wenyewe kama hatuwa kubwa ya kutengeneza upya mataifa yao na mustakbali wake.
(Vuguvugu la Watanzania la kutaka Katiba Mpya lilianza miaka mingi ya nyuma. Lakini lilipata msukumo wa matumaini mwaka 2010, pale rais aliyekuwepo madarakani Jakaya Mrisho Kikwete alipo unga mkono vuguvugu hilo katika hotuba yake ya kuuaga mwaka huo:
“Tumekubali kuanzisha mchakato kutazama upya Katiba yetu ya sasa tuliyoachiwa na waasisi wa Taifa letu. Ni vema kuwa na Katiba inayoendana na mabadiliko ya matakwa ya hali ya sasa…”
Maelezo hayo ya rais yalikuwa sahihi kutokana na sababu kadhaa: Miongoni mwa hizo ni mabadiliko makubwa ya kisiasa ya nchi yetu kutoka katika mfumo wa chama kimoja na kuingia mfumo wa vyama vingi. Mabadiliko hayo yanalazimisha mabadiliko katika Siasa, Uchumi, Mgawanyo wa Madaraka katika Mihimili ya Dola, Muundo wa Muungano na Ushirikishwaji wa wananchi katika maamuzi ya mataifa yao. Katiba ya Jamhuri ya Muungano 1977, iliyopo sasa ina udhaifu wa mambo mengi ikiwemo mkanganyiko mkubwa katika mambo yanayohusu Muungano, yanayohusu Tanganyika na mambo yanayohusu Tanzania na Zanzibar.
Aidha baada ya hotuba ya Rais Kikwete, mchakato wa Katiba Mpya uliowashirikisha wananchi ulianza: Bunge lilipitisha sheria Na. 8. ya Mabadiliko ya Katiba, Rais alizitaarifu Asasi mbalimbali zikiwemo za Dini kupeleke majina ya wawakilishi wao watakaoteuliwa kuwa wajumbe wa Tume ya Kuratibu na Kukusanya Maoni na hatimaye wajumbe wa Bunge la Katiba. Asasi hizo za wananchi zilipeleka majina kwa mamlaka husika na Tume iliundwa na kupitishwa tarehe 01.05.2012. Tume hiyo ilianza kazi ya kukusanya maoni Tarehe 19.06.2012. Mamilioni ya Watanzania kupitia mabaraza na mikutano ya wazi walitoa maoni yao mbele ya Tume hiyo.
Pamoja na mambo mengine, sehemu kubwa ya maoni ya wananchi walitaka Mfumo wa Muungano wa serikali tatu. Kuwepo na Serikali ya Tanganyika Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Muungano. Katika jambo kubwa la kupata uongozi wa Serikali zao walipendekeza kuundwa Tume Huru ya Uchaguzi (Independent Electrol Commission). Maoni haya yalifika katika Mamlaka zote zilizoundwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Hata hivyo haki hiyo kubwa ya wananchi ya kuunda Katiba Mpya ya Mataifa yao imechezewa kwa kiasi kikubwa na wanasiasa na hatimaye imewekwa rehani. Hakuna Katiba Mpya hakuna Tume Huru ya Uchaguzi wala sababu zinazokidhi sheria au matakwa ya Wananchi. Kama ilivyozoweleka wanasiasa wameendelea kuwaamulia Wananchi na sasa wamepanga Uchaguzi Mkuu Oktoba 2020, bila ya Katiba Mpya wala Tume Huru ya Uchaguzi.
UMUHIMU WA MABORESHO YA KANUNI KIPINDI CHA MPITO
Utangulizi
Katika Asasi zilizoteuliwa na Waislamu kusimamia mambo yao ya Siasa, Kamati ya Kutetea Haki za Waislamu Tanzania (1993), na Shura ya Maimamu Tanzania (1998), ni Asasi muhimu sana katika utekelezaji wa yale yanayoamuliwa katika vikao vya Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania.
Utaratibu huo umewawezesha Waislamu kushiriki siasa na kutoa mchango mkubwa kwa mujibu wa sheria za nchi. Kamati Kuu ya Siasa ya Shura ya Maimamu Tanzania licha ya kuwahudumia Waislamu katika siasa, hufanya kazi za kijamii ikiwemo kuweka waangalizi wa uchaguzi, kufanya tathmini baada ya uchaguzi na kuiwasilisha katika mamlaka husika na kwa Umma. Sehemu ya tathmini ya uchaguzi wa mwaka 2000, ina maelezo yafuatayo:
“Ndugu Watanzania wenzetu, tarehe 29. 10. 2000, tulipiga kura ili tupate viongozi wa kitaifa tuliowachagua kwa ridhaa yetu. Hata hivyo, wako baadhi ya wananchi hawakupiga kura kwa sababu mbalimbali. Miongoni mwa hizo ni kuzuiwa kupiga kura, majina yao kufutwa au kukuta yametumiwa na watu wasiojulikana kwao na kadhalika. Lakini pia wapo wagombea ambao wamedhulumiwa kura zao. Baadhi yao wamelalamikia kuwepo kwa idadi kubwa ya wapiga kura kuliko idadi ya watu walioandikishwa, kuwepo kwa shahada za bandia na watu walioandaliwa waliopiga kura mara mbili.
Kabla hata ya uchaguzi kulipatikana habari za kukamatwa watu wakiwa na vitabu vya shahada za kupiga kura, maelfu ya watu kutoka Tanganyika na kupelekwa Zanzibar kujiandikisha kwa ajili ya kupiga kura na ongezeko la ghafla la wapiga kura milioni tatu (Tanzania Bara). Malalamiko yote haya hatukusikia kupatiwa ufumbuzi kabla ya uchaguzi.
Kama wasemaji wa kidini na kama Watanzania, tuliwahi kuitahadharisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi National Electrol Commission (NEC) lakini hapakuwa na mrejesho wowote kutoka kwa watendaji wake wakuu. Ukimya huo uliwafanya Watanzania walio wengi kushiriki uchaguzi wakiwa na mashaka makubwa. Waliofanya hivi wamefanya kwa makusudi na bila shaka ni watu hatari sana kwa amani ya nchi yetu. Maana unapomzuia mtu kupata haki yake kwa njia halali, unakusudia nini? Unataka nchi yetu iwe kama hizo zilizokumbwa na matokeo ya watu kudhulumiwa haki zao?… “.
Katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, Kamati Kuu ya Siasa ya Shura ya Maimamu pia ilitoa Waraka na hatimaye tathmini. Sehemu ya tathmini mwaka huo inasema:
“Katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani, watu wengi waliojiandikisha katika daftari la wapiga kura hawakuona majina yao kwenye orodha za wapiga kura zilipobandikwa vituoni. Tatizo hilo liliendelea mpaka siku ya kupiga kura ambapo wananchi hao hawakupata haki ya kuchagua viongozi wa nchi."
Baadhi ya vyombo vya habari viliandika kilio cha Wananchi hao kama ifuatavyo:
“Wengi walilalamika kuyakuta majina yao nje lakini walipoingia ndani hawakuyaona katika orodha ya daftari la wapiga kura”.
Chombo kingine cha Habari kiliandika:
_
“Karibu maeneo yote, vifaa vya kupigia kura vilikuwepo lakini lililojitokeza ni mkanganyiko wa majina ya wapiga kura. Baadhi ya majina yalihamishwa kutoka sehemu walizojiandikisha na kupelekwa vituo vingine. Hali kama hiyo ilijitokeza eneo la Mpanda, Arusha ambako watu zaidi ya 100, walihangaika kutafuta majina yao na walipoyapata muda wa kupiga kura ukawa umekwisha. Polisi wa kutuliza ghasia FFU, walitumia nguvu kuwafukuza ilihali wao wakiwa wanabembeleza waweze kupiga kura”_
Tathmini hizi za Waislamu (ambazo hupatikana kutokana na waangalizi wake katika uchaguzi), huwa na mchango mkubwa katika kutambulisha mambo muhimu yaliyojitokeza wakati wa chaguzi hizo).
Tukiingia katika usuli wa kichwa cha mada hii “Umuhimu wa kuboresha Kanuni Kipindi cha Mpito” pamoja na kutokuwepo kwa Tume Huru ya Uchaguzi Serikali imesema uchaguzi Oktoba 2020, utafanyika. Na wale watakaotangazwa na Tume za Taifa za Uchaguzi (NEC na ZEC) watapewa mamlaka ya kuongoza Taifa. Kwa Watanzania wanaotaka Tume Huru ya Uchaguzi, Uchaguzi huu kwao ni tukio la kipindi cha mpito katika vuguvugu la madai ya Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi. (Waislamu ni miongoni mwa tabaka hilo). (Hata Serikali yenyewe pia imekuwa ikidai kuwa suala hilo ni muhimu kwa sasa lakini tatizo kwao ni fedha).
Katika muktadha huo wito wetu ni kuboreshwa Kanuni za Uchaguzi na Uendeshaji wa zoezi la Uchaguzi ili kuwezesha kufanyika Uchaguzi Huru na wa Haki. Mamlaka za Uchaguzi Tanzania Bara na Visiwani NEC na ZEC zione dharua iliyopo ziitishe mabaraza (au au au) ya kutunga Kanuni za Uchaguzi. Katika hatuwa hiyo muhimu Serikali zishirikishe makundi muhimu vikiwemo vyama vya Siasa. Huo pia ni wito wa Watanzania mbali mbali wamekuwa wakipendekeza maboresho (shirikishi) ya kanuni katika kipindi hiki cha mpito. Miongoni mwa maboresho tunayoyaunga mkono na kupendekeza ni:
1) Kanuni ya Uchaguzi itamke wazi vyama vya Siasa vitapewa nakala ya Daftari la Wapiga kura mapema kabla ya kampeni kuanza.
2) Kanuni itamke na kuweka msisitizo wa hatuwa za kisheria kuwa viongozi wa Serikali kama Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Watumishi wa Umma wasitumike kisiasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi.
3) Kanuni itamke Mashirika na Taasisi za Umma hwairuhusiwi kufanya kampeni ya mgombea yoyote au chama chochote cha siasa.
4) Aidha kanuni ya zamani ilikuwa inaagiza Wakala wa chama apewe nakala yake ya kiapo mara tu baada ya kuapishwa. Upo mchakato batili unaolenga mabadiliko ya kanuni hiyo ili itamke; atapewa nakala yake siku ya kupiga kura nje ya kituo. Kwakuwa nakala hii ndio tiketi ya wakala ya kuingia ndani ya chumba cha kupigia kura, kanuni itamke wazi kuwa wakala wa chama cha siasa atapewa nakala yake ya kioapo mara tu baada ya kuapishwa.
5) Kanuni itamke Kura zitapigwa na kuhesabiwe katika kituo husika cha kupigia kura. Itamke wazi baada ya kuhesabiwa hazitahamishwa katika kituo hicho na kupelekwa katika kituo kingine chochote kwaajili ya kuhesabiwa upya.
6) Kanuni itamke Mawakala wapewe nakala za Matokeo ya kura katika vituo vyao bila kubabaishwa wala kutishwa.
7) Kanuni itamke Matokeo ya wagombea yatangazwe pale pale katika kituo cha kupigia kura.
8) Kanuni itamke idhini ya Asasi za Ndani na nje kuweka Waangalizi wa uchaguzi na uhuru wa kutoa ripoti zao.
9) Kanuni itamke Vyombo vya dola kama vile Jeshi la Polisi, Usalama wa Taifa na Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haviruhusiwi kuingilia mambo ya uchaguzi. Itamke kuwa askari waliovaa sare na kubeba silaha watakaa mita miamoja kutoka kituo cha kupigia kura.
10) Kanuni iwakumbushe Majaji na Mahakimu pamoja na Maofisa wengine wa Mahakama wajibu wa kutenda haki kwa Mashauri yote ya uchaguzi.
Mapendekezo hayo yatapunguza kwa kiasi kikubwa ombwe la kukosekana Tume Huru ya Uchaguzi na yanaleta matumaini ya Uchaguzi Huru na wa Haki katika kipindi hiki cha mpito cha madai ya Wananchi ya Tume Huru (Independent Electrol Commission).
WAISLAMU TUNATAKA HAKI NA USAWA
Hapo nyuma tumezungumza kama Watanzania. Maelezo yetu yamejadili na kupigania maslahi ya Taifa na Watanzania kwa ujumla. Lakini pia sisi ni Waislamu na kama yalivyo makundi mengine ya kijamii tunao wajibu wa kutafakari, kujitazama na kutazamwa kwa maslahi yetu. Waislamu wanatambua kuwa siasa ni sehemu muhimu ya maisha yao na hawawezi kujitenga na siasa. Kwasababu hiyo wanaelewa mfumo wa siasa usio wa haki na usawa unaweza kuathiri ustawi wa maisha yao ya kila siku kidini, kijamii, kiuchumi, kiusalama, kiutamaduni na kadhalika. Tunaweza kusema siasa inanafasi kubwa katika mustakbali wa ustawi wao. Waislamu tumeshiriki ipasavyo chaguzi za nyuma ukiwemo uliounda serikali iliopo madarakani. Lengo likiwa ni kushiriki katika ujenzi wa Taifa bora, huru na lenye maendeleo. Taifa la wote linalotenda Haki, Usawa na Uadilifu kwa wote. Tukitaraji tuwe na Uongozi wa nchi unaowatendea haki wananchi wote bila ubaguzi wa Kidini, Kikabila, Jinsia, Rangi au eneo analotoka mtu.
Mpaka sasa Waislamu wameshindwa kuona nafuu yao katika matokeo ya siasa hizo. Hawaoni nafuu katika Uhuru wa kuabudu, Uhuru wa Kujiamulia mambo yao wenyewe (hata yale ya kidini), Usalama wa Viongozi wao, Madrasa zao, Misikiti na Watu wao. Hawaoni usawa wowote katika madaraka na ajira za serikali. Mfumo wa Elimu wa Taifa hautoi fursa sawa wala kutenda haki kwa wote. Orodha ya viashiria vya tatizo hilo ni kubwa mno lakini tunaweza kupitia hivi vichache:
Uadilifu I
Januari 11, 2019, serikali ilifanya uhamisho mkubwa wa kushitukiza kwa wahadhiri na watumishi wandamizi katika Chuo Kikuu cha Serikali cha Dodoma-UDOM. Waliohamishwa walikuwa 11, lakini wote walikuwa Waislamu: Dk. Maryam Khamis (Director of Graduate Studies), Dk. Ibun Kombo (Political Science), Dk. Mwinyikombo Amir (Mwalimu wa Udaktari wa Binadamu), Dk. Yusuf Kambuga (College of Education), Dk. Masoud Masoud (Informatics) , Bw. Subira Sawasawa (Mkurugenzi Mkuu Rasilimali Watu), Bw. Mohamed Mwandege (Bursar/Mhasibu Mkuu), Bi. Aziza Gendo (Seniour Estate Oficer), Bw. Simba Omary (Senior Supplies Oficer), Bw. Wema Mbegu (Legal Oficer), Bw. Khamis Mkanachi (Mwalimu wa Idara ya Historia).
Barua zao za uhamisho hazikuonesha makosa katika utendaji wao wa kazi au uongozi. Pamoja na kutokuwa wakosaji, uhamisho wao uliambatana na udhalilishaji mkubwa, kunyimwa haki stahiki za uhamisho, kuhamishiwa katika nafasi za chini kinyume na hadhi zao.
Baada ya uhamisho huo, Serikali ilifanya uteuzi mwingine katika chuo hicho hicho cha Serikali. Katika uteuzi huo walioteuliwa walikuwa 11, wote Wakristo: Prof. Leonard James Mselle, Prof. Adam B. Swebe Mwakalobo, Prof. Julius William Nyahongo, Prof. Justin Ntalikwa, Prof. Frowing Paul Nyoni, Prof. Odass Bilame, Prof. Ainory Piter Gasese, Dkt. Victor George Mareale, Dkt. Alex Shayo, Dkt. Calvin Swai, Dkt. Augustine Mwakipesile.
Kuhamisha wahadhiri 11, katika Chuo Kikuu si jambo dogo. Vilevile kuhamisha Wahadhiri 11, wa dini moja (Waislamu) katika Chuo Kikuu ukaingiza wahadhiri 11 wa dini moja (Wakristo), na hao Waislamu 11, baadhi yao ukawatoa kabisa katika mfumo wa elimu kwa kuwapeleka sekta nyingine na zisizo lingana na hadhi zao si jambo dogo. Wala si hatua ya kitaalamu ya kuboresha mfumo wa Elimu wa Taifa. Na wala si hatua ya kijinga bali ya werevu uliofurutu ada dhidi ya maslahi ya Taifa. Hatuwa hiyo ni salamu nzito kwa jamii yao na Taifa kwa ujumla. (Ndio maana katika maoni yetu ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tulipendekeza Katiba Mpya imtambuwa Mwenyezi Mungu na Dini liwe suala rasmi na la wazi katika uendeshaji wa nchi).
Uadilifu II
Serikali ya awamu ya tano ilipoingia madarakani Mwaka (2015), Rais alifanya uteuzi wa Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Wilaya na Wakurugenzi mbalimbali. Uteuzi wake ulikuwa kama ifuatavyo:
Mawaziri na Manaibu: 30.
Waislamu 10, sawa na asilimia 33%.
Wakristo 20, sawa na asilimia 67%.
Makatibu Wakuu na Manaibu: 50.
Waislamu 10, sawa na asilimia 20%.
Wakristo 40, sawa na asilimia 80%.
Wakuu wa Mikoa na Wilaya: 166.
Waislamu 41, sawa na asilimia 25%.
Wakristo 125, sawa na asilimia 75%.
Makatibu Tawala wa Mikoa na Wilaya: 163.
Waislamu 24, sawa na asilimia 15%.
Wakristo 139, sawa na asilimia 85%.
Wakurugenzi mbalimbali: 249.
Waislamu 45, sawa na asilimia 18%.
Wakristo 204, sawa na asilimia 82%.
Manaibu Kamishna wa Polisi: 25.
Waislamu 5, sawa na asilimia 20%.
Wakristo 20, sawa na asilimia 80%.
Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Polisi: 33
Waislamu 7, sawa na asilimia 21%.
Wakristo 26, sawa na asilimia 79%.
Jumla Kuu ya Uteuzi:
Waislamu asilimia 20%.
Wakristo asilimia 80%.
Uteuzi huo umekuwa kama Sera kwa teuzi zinazoendelea ndani ya miaka yote mitano. Vilevile kama Mwongozo kwa wateule wenye mamlaka ya kuteuwa. Mwelekeo huo unakinzana na Katiba ya nchi ibara ya 13(4)(5), inayokataza ubaguzi wa aina zote. Kwa hakika Taifa halihitaji kiongozi wa nchi akiwa Muislamu basi ateuwe idadi kubwa ya Waislamu wenzake katika nafasi mbalimbali za uongozi wa nchi au akiwa Mkristo atumie uongozi wake kuteua idadi kubwa ya Wakristo wenzake katika uongozi nchini. Au akiwa Mzanaki ateuwe idadi kubwa ya Wazanaki wenzake katika nafasi mbalimbali za uongozi na mfano wa hayo.
Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, Rais ana mamlaka makubwa kuliko chombo chochote. Baraza la Mawaziri jukumu lake ni kumshauri tu na Katiba inampa uhuru wa kufuata au kutofuata ushauri wa chombo hicho au mtu yoyote. Mamlaka ya Rais pia yako juu kuliko ya Bunge. Rais anateuwa sehemu ya wabunge na ana mamlaka ya kulivunja Bunge. Rais pia anateuwa Majaji wa Mahakama na watendaji wengine wa kitaifa. Kwa kifupi Rais wa Tanzania ndiye muhandisi mkuu na mwenye kutengeneza shakhsia (Personality) ya Taifa.
Katika jukumu hilo la kutengeneza shakhsia ya Taifa, miongoni mwa watumishi wa umma 1269, wanaoteuliwa na mamlaka ya Rais ambao ni pamoja na: Waziri Mkuu, Jaji Mkuu, Mawaziri na Manaibu, Majaji, Mkuu wa Majeshi, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Mabalozi wa Nchi za Nje, Makatibu Wakuu na Manaibu Katibu Wakuu wa Wizara, Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala Wilaya (DAS), Makatibu Tawala Mikoa (RAS), Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Majiji, Manispaa, na Wilaya, Wakuu wa Bodi na Tume mbalimbali, Makamishna, Wakuu wa Mashirika ya Umma, Wakuu wa Vyuo Vikuu na kadhalika, asilimia 80 ya uteuzi huo unafanyika kwa Watanzania wa imani moja.
Na hao wateuliwa na wao wana mamlaka ya uteuzi katika maeneo yao au kusimamia masuala ya uteuzi, ajira, na kufanya maamuzi mbalimbali ya utendaji na uendeshaji kwa niaba ya Taifa. Wakitaka na wao wanaweza kufanya uteuzi ule wa asilimia 80 ya watu wa imani moja (au kabila moja).
Lingine la kuzingatiwa, uteuzi huo unawapa wateule hao Mamlaka, uwezo wa kufanya Maamuzi na Utawala. Lingine kubwa ni kwamba uteuzi huo unatoa fursa za mapato, maana yake ni kuwa, zaidi ya asilimia 80 ya pato la Taifa linalohudumia malipo na stahiki za watumishi wa umma linakwenda kwa kundi moja la kijamii na kuliacha kundi jingine.
Tunachotaka ni sera za Uwiano sahihi. Katiba za Kanya na ya Nigeria ni mfano mzuri wa dhana hii ya Uwiano sahihi. Ukurasa wa 75, Sura ya 9, sehemu ya kwanza, ibara ya 130 (1)(2), na uk 151 Sura 15, ibara ya 250 (4), ya Katiba ya Kenya inaelekeza, nafasi za Uteuzi za wafanya Maamuzi (Executives) na nafasi nyengine nyeti kama vile Mawaziri na Manaibu Waziri, Makatibu na Manaibu Katibu, Makamishna na Wakurugenzi, kuwepo Uwiano ulio Sawa na Ujumuishi (yaani pamoja na kuangalia weledi, uzoefu na uadilifu, lakin pia kuwepo na uwiano wa watu kwa kuzingatia walemavu, rangi, jinsia, Dini, makabila na mfano wa hayo) .
Katiba hiyo pia uk 143, sura ya 14, sehemu I, ibara ya 238 2(d), na uk 146, sura ya 14, sehemu ya II, ibara ya 241 (4), uk 149, sehemu ya IV, ibara ya 246 (4) inaelekeza mihimili ya Serikali ikiwa ni pamoja na Majaji, Majeshi yote ya Ulinzi na Usalama kama: Jeshi la Wananchi, Jeshi la Polisi, teuzi na ajira pamoja na kuangalia weledi, uzoefu na uadilifu kuwepo uwiano kama tulivyoona katika vifungu vya hapo nyuma.
Halikadhalika Katiba ya Nigeria, uk 8 Sura 2, ibara ya 4, maudhui yake yanaelekeza, Serikali Kuu, Serikali za Majimbo, Halmashauri za Miji, Mawakala (wanaofanya kazi kwa niaba ya Serikali, Vyama vya siasa) ni sharti ajira zao kuzingatia suala la uwiano wa mahala husika na Ujumuishi wa makabila na Dini.
Jambo muhimu ni mabadiliko ya fikra kwa viongozi wetu. Kama Isiwe Rais akiwa Muislamu ateuwe Waislamu wengi kwenye serikali yake, au akiwa Mkristo ateuwe Wakristo wengi kwenye serikali yake. Hakuna sababu yoyote ya msingi ya uteuzi huo.
Uadilifu III
Waislamu wamekuwa wakilalamikia sera zinazowaondolea Uhuru wao wa kiimani na kijamii. Wanapotekeleza haki yao za kiimani na kushiriki mambo mbalimbali ya kijamii ikiwemo siasa huchukuliwa hatua dhidi yao na kubambikiwa kesi zikiwemo za Ugaidi na kuwekwa magerezani bila haki kutendeka. Katika hili tunao mfano wa Masheikh na mamia ya wafuasi wao waliowekwa magerezani na serikali kwa miaka zaidi ya sita bila ya kupewa haki ya kujitetea wala kuhukumiwa:
JINA LA MAHABUSU NA NAMBA YA KESI.
Ali Othman Rashid (PI 18/2013). Faraji Ali Ramadhani (PI 18/2013). Musa Daudi (PI 18/2013). Shabani Bakari Waziri Mtweve (PI 18/2013). Farid Hadi Ahmed (PI 29/2014).
Jamali Nurudin Swalehe (PI 29/2014). Nassoro Hamadi Abdallah (PI 29/2014). Saidi Amour Salum (PI 29/2014). Rashid Ali Nyange (PI 29/2014). Hassan Bakari Suleiman (PI 29/2014).
Antar Hamoud Ahmed (PI 29/2014).
Juma Sadallah Juma (PI 29/2014). Allawi Othman Amir (PI 29/2014). Msellem Ali Msellem (PI 29/2014). Amir Hamis Juma (PI 29/2014). Said Kassima Ali (PI 29/2014). Salum Amour Salum (PI 29/2014). Salum Ali Salum (PI 29/2014).
Abdallah Said Ali (PI 29/2014). Ali Khamisi Ali (PI 29/2014). Kassim Salum Nassor (PI 29/2014).
Abdallah Hassan Hassan (PI 29/2014).
Mohamed Is-haka Yusufu (PI 29/2014). Said Shehe Sharifu (PI 29/2014).
Hussein Mohamed Ali (PI 29/2014). Hamisi Amour Salum (PI 29/2014). Abubakar Abdalla Mgodo (PI 29/2014). Suleiman Othman Maulid (PI 41/2014). Hassan Hamis Hamis (PI 41/2014). Haroub Rashid Ali (PI 41/2014). Abdallah Amari Mzee (PI 41/2014). Kassim Mukadam hamis (PI 41/2014).
Salum Ali Salum (PI 41/2014). Mgeni Alio Omari (PI 41/2014). Khamis Mohamed Khamis (PI 41/2014). Haruna Mussa Lugeye (PI 8/2015). Mwajuma Wendo Bakari (PI 8/2015). Ali Khalid Tagalile (PI 8/2015). Jihad Gaibon Swalehe 9PI 31/2015). Juma Zuber Othman (PI 32/2015). Ali Nassoro Omari (PI 32/2015). Khamisi Fundi Kamaka (PI 33/2015). Ilyasa Kalinda Kazana (PI 33/2015).
Issa Mussa Mustafa (PI 33/2015). Othman Hamis Abeid (PI 33/2015). Juma Rajab Mbonde (PI 33/2015). Sharifu Suleiman Sharifu (PI 34/2015). Sadiki Shaban Mdoe (PI 45/2015). Hamadi Omari Hamisi (PI 45/2015). Saidi Waziri Nkuro (PI 45/2015). Hassan Abdllah Mandiki (PI 45/2015). Hamadi Yusufu Ndulele (PI 45/2015). Shomari Saidi Ngwambi (PI 45/2015). Salum Hamisi Bakari (PI 45/2015).
Issa Hassan Jabir (PI 45/2015). Khatibu Hassan Khamis (PI 45/2015). Saidi Hamisi Mtulya (PI 45/2015). Jafari Hassan Mdoe (PI 45/2015). Shaibu Sam Mkungu (PI 45/2015). Hamis Miraji Hussein (PI 45/2015). Nurdin Salum Mhagama (PI 45/2015). Abdurashid Said Sadiki (PI 45/2015). Ali Ayoub Ngingo (PI 45/2015). Abdillah Ismail Ndibalema (PI 45/2015). Hamisi Hussein Ramadhan (PI 45/2015). Juma Ali Hassan (PI 45/2015).
Ibrahim Abdalla Masufuria (PI 45/2015). Seif Ramadhani Mbwate (PI 45/2015). Abdalla Hamis Lupindo (PI 45/2015). Ali Juma Ngachoka (PI 45/2015). Abbasi Ayoub Mkanda (PI 47/2015). Shafii Shaibu Mputeni (PI 47/2015). Mohamed Ali Omari (PI 47/2015). Twalha Ahmad Mwaluka (PI 47/2015). Nassoro Hemed Saidi (PI 47/2015). Rajab Suleiman Chijeta (PI 47/2015). Abubakari Paulo Mgita (PI 47/2015).
Said Mwinchande Mandanda (PI 47/2015). Abdalla Fakhii mohamed (PI 47/2015). Abdallah Mwitike Abdalla (PI 49/2015). Nurudin Hafidh Ndawaine (PI 49/2015). Abdukarim Evarist Msofe (PI 49/2015). Muhamed Said Nassoro (PI 49/2015). Abdurashid Thabit Bihaki (PI 49/2015). Juma Yassin Ali (PI 55/2015). Nassoro Said Amour (PI 55/2015). Mabruck abdul-wahid (PI 55/2015). Ali Mwinchande said (PI 55/2015).
Amran Ramadhan Mpondo (PI 55/2015). Abdalla Juma Omari (PI 55/2015). Shaban Juma Habiru (PI 55/2015). Ismail ali Asuni (PI 55/2015). Hamisi Haji Machano (PI 55/2015). Mohamed Miraji Ibrahim (PI 55/2015). Shaban Juma Shaban (PI 55/2015). Athuman Jumanne Nassoro (PI 60/2015). Salehe Suleiman Salehe (PI 61/2015). Sadam Said Ali (PI 02/2016). Hamis Amir Mkumba (PI 03/2016).
Hamis Shabani Hamis (PI 03/2016). Buheti Yusuf Buheti (PI 07/2016). Yusufu Issa Rajab (PI 07/2016). Seif Shah Jongo (PI 07/2016). Hassan Bakari Mnele (PI 50/2015). Ramia Shaban Salehe (PI 50/2015). Zahaki Rashid Ngai (PI 52/2015). Dua Said Linyama (PI 52/2015). Chande Rashid Njawi (PI 52/2015). Rashid Omari Mmigwa (PI 52/2015). Issa Abdalla Kokoko (PI 52/2015). Idd Suleiman Nyange (PI 17/2015).
Said Bakari Mkumba (PI 17/2015). Said Maulid Rajab (PI 17/2015). Salum Halidi Mputa (PI 17/2015). Rajab Salum Dondora (PI 19/2015). Juma Mohamed Mtitu (PI 19/2015). Saidi Ali Faki (PI 08/2016). Mahamud Mwinchande (PI 08/2016). Kasim Abdurahman Mahdi (PI 08/2016). Ali Makomba Ali (PI 08/2016). Kulthum Iddi Mussa (PI 15/2016). Said Salum Mbai (PI 13/2016). Hamisi Saidi Mkundi (PI 13/2016).
Sultan Shaibu Mtandika (PI 13/2016). Is-haka Rashid Mtutula (PI 13/2016). Mahmud Abdalla Ramadhan (PI 13/2016). Abdul Yusuf Nambunga (PI 13/2016). Abuu Masudi Mwalim (PI 13/2016). Haji Hamisi Chitwanga (PI 13/2016). Khalid Zuberi Ame (PI 13/2016). Sultan Salum Muhani (PI 15/2017). Rashid Saidi Abdalla Ulunga (PI 15/2017). Ali Mchepe (PI 15/2017). Othman Ali Mzee (PI 15/2017). Hamis Hemed Khambale (PI 15/2017). Athumani Salum Mbonjoro (PI 15/2017).
Shabani Salehe Kawambwa (PI 15/2017). Sultan Salum Muhani (PI 15/2017). Rashid Ali Mchepe (PI 15/2017). Saidi Abdalla Ulunga (PI 15/2017). Othman Ali Mzee (PI 15/2017). Hamis Hemed Khambale (PI 15/2017). Athumani Salum Mbonjoro (PI 15/2017). Shabani Salehe Kawambwa (PI 15/2017). Ramadhan Athuman Ali (PI 18/2017). Mrisho Suleiman Daud (PI 18/2017). Hamisi Yunus Abdallah (PI 18/2017).
Waislamu hao wako jela kwa zaidi ya miaka sita na hawajui hatma yao. Baadhi yao wamefariki dunia katika magereza mbalimbali nchini. Ingawa hatupendi mtu yoyote atendewe hivyo lakini hatuoni watu wa dini nyingine yoyote wakitendewa hayo ila Waislamu. Hata kama wanapoyasema hayo hawasikilizwi na badala yake hupewa majina mabaya ya uchochezi, ugaidi, lakini wana haki ya kusema. Hivi karibuni baadhi ya viongozi (wa dini wa Kikristo) wa kabila la Rais walitangaza hadharani mpango wao wa kuunda vikundi vya kikabila vya kuimarisha utawala wa Rais aliopo madarakani hawakuitwa wachochezi wala kuchanganya kabila, siasa na dini.
Taifa letu linahitaji Viongozi waadilifu sawa na Mfalme Najash wa Ethiopia (Habash). Najash (Mkristo) alipelekewa fitna na wasaidizi wake ya kuwanyima haki ya uhuru na kuwadhuru Waislamu alikataa. Alisikia hoja za Waislamu aliwapa haki ya uhuru na kuwatendea haki sawa na ndugu zao Wakristo katika utawala wake. Kwa muktadha huo Waislamu kama binadamu na watu wenye haki zote za kitaifa hawawezi kufurahishwa na mfumo wa utawala usio wajali na kuheshimu haki zao za msingi.
SIFA ZA MGOMBEA
1. Mgombea awe Mkweli na mwenye Utu.
2. Awe mwenye kuheshimu KIAPO.
Awe mwenye sifa ya kupiga vita ubaguzi wa aina zote.
Awe na elimu kubwa au wastani, mwenye maarifa ya kutosha ya kuongoza watu na serikali.
Awe mtu mwenye mtazamo wa maendeleo kwa Taifa na Watanzania wote.
Awe mwenye kuheshimu Uhuru wa Mawazo ya Watu wengine.
Awe mwenye kuzijua Haki za binaadamu na kuzilinda.
Asiwe mwenye kutumia vibaya madaraka na kuvunja sheria za nchi.
Awe ni mwenye kupenda Umoja wa Taifa na dhamira ya Muungano wa kweli.
Asiwe fisadi na mwenye kuficha ukweli.
Awe Mwenye kumtambua Mwenyezi Mungu wa Walimwengu wote.
Asiwe Kibri, Dikteta Mkandamizaji na Mdhalilishaji wa watu anaowaongoza.
Asiwe mtu mwenye kujali maslahi yake na kundi lake sambamba na kufikiria sheria za kujilinda
dhidi ya mkondo wa sheria kwa tuhuma za ufisadi na uvunjaji wa Haki za Binadamu.
SIFA ZA CHAMA CHA MGOMBEA
1. Mgombea awe anatoka katika chama (au muungano wa vyama) kinachokidhi matakwa ya sheria za nchi kushika uongozi Tanzanzia Bara na Zanzibar.
2. Awe anatoka katika chama ambacho kinaamini KWA DHATI usawa baina ya Tanganyika na Zanzibar.
3. Awe anatoka katika chama ambacho hakina historia ya ubaguzi wa kidini, Kikabila, wala jinsia.
4. Awe anatoka katika chama chenye dhamira ya kweli ya kuwepo mfumo wa vyama vingi vya Siasa Tanzania.
5. Chama chake kiwe kina sera za kweli na mipango thabiti ya kuwaletea wananchi hali nzuri ya maisha katika masuala ya msingi kama Chakula, Matibabu, Ada, Kilimo, Kukuza Ustawi wa Uchumi, Ajira, Elimu bora kwa wote na mfano wa hayo.
6. (Katika suala muhimu la usalama wananchi wa Tanzania wana tatizo kubwa. Matukio ni mengi lakini moja la hivi karibuni linakidhi kwa mfano. Tarehe 27. 04. 2020 watu wapatao kumi wakiwa na bunduki (SMG) na magari mawili Landrover Defender walifika katika Kata ya Kilolambwani Jimbo la Mchinga Wilayani Lindi Mkoani Lindi na kuwateka raia wapatao watano. Raia hao ni Saidi Sasi Wajihi, Rashidi Mangala Mapua, Rashid Ahmad Mlombile, Hassan Saidi Sabuyetu na Ahmad Khamisi Malanda na kutoweka nao. Mbunge wa Jimbo hilo (wa Chama cha upinzani) alifuatilia katika ngazi zote zenye dhamana ya usalama wa raia na mali zao alijibiwa kuwa hazijui lolote kuhusu kutekwa raia hao. Ingawa watu hao baada ya siku chache walipatikana baadhi yao wakiwa na majeraha makubwa ya mateso, wapo raia wengi Tanzania waliotekwa na kupotezwa kabisa kwa utaratibu huo. Baadhi yao ni Sheikh Habib Mohamed Gora, Sheikh Khatibu Yunus, Azory Gwanda, Ben Sanane, Sheikh Salim Mohamed (huyu maiti yake ilipatikana): Kwa muktadha huo kiwe chama kitakacholeta usalama wa raia na mali zao.
7. Kiwe chama kitakachoweka utaratibu makhsusi wa kuwafidia, na kuwafariji Wajane, Watoto mayatima na wanajamii ambao waume zao, wazazi wao na ndugu zao wametekwa na wengine kuuawa kikatili kinyume cha haki na sheria.
8. Chama kitakachoweza kuisimamia Serikali na uwajibikaji kwa watendaji wake wanaovunja Haki za raia.
9. Kiwe chama kitakacho heshimi uhuru wa kibiashara na kutambua nafasi na mchango wa Wafanyabiashara wadogo na wakubwa, katika ustawi wa jamii na pato la Taifa. Chama kitakachowapa watumishi wastaafu malipo yao ya uzeeni bila kuwadharau, kuwahangaisha na kuwadhulumu.
10. Kiwe Chama kinachojali Elimu na sera ya elimu endelevu na mitaala sahihi. Chama kisichowapuuza wanafunzi na kupambana na juhudi za sekta binafsi katika kukuza maendeleo ya Elimu nchini.
11. Kiwe chama kinachojali maslahi ya watumishi wa serikali na Asasi za Umma hakitawajengea mazingira magumu ya kazi na kuheshimu sheria za utumishi wa umma.
12. (Mwaka 2016, wakulima wa Korosho waliwaomba wanunuzi wao wa nje kutoa kiasi cha fedha (ruzuku) ili iwasaidie kuzalisha zaidi. Wafanyabiashara hao walikubali na Wakulima kupitia chama chao cha ushirika walifunga mkataba na Tanzania Revenue Authority (TRA), ili wawakusanyie fedha hizo. (TRA) katika utaratibu wake, fedha hizo waliziita (Export Levy). Msimu wa mavuno 2017/2018, mavuno yao yaliwaingiza shilingi Trilioni moja na billioni miatatu (1,3 Trilioni). Mwaka 2018, serikali ilipitisha sheria ya kuchukuwa Export Levy (fedha za wakulima) kuwa mali yake. Serikali pia ilidhibiti mashamba ya wakulima na maghala yao ikajitangaza kuwa mnunuzi pekee kwa bei watakayo. Mwisho wa tukio hilo wakulima walipata hasara kubwa na kuzidi kudidimia katika lindi la umaskini): Kwa muktadha huo kiwe chama kitakacho heshimu jitihada za wakulima chenye sera bora za kilimo na kuwasaidia Wakulima kupata pembejeo kwa bei nafuu na soko huru la kuuza mali zao.
13. Kiwe chama ambacho serikali yake itazingatia vipaumbele vya wananchi badala ya kutumia pato dogo la Taifa kufanya matumizi kwa mambo yasiyokuwa na tija na yasiyokuwa na mrejesho wa maana kwa maisha ya mwananchi wa kawaida.
14. Kiwe chama kitakachojenga nidhamu ya utendaji kwa watumishi wa umma na kujenga uhusiano mzuri baina ya vyombo vya dola na raia.
15. Kiwe chama chenye dhamira ya kuibakisha Tanzania kuwa nchi inayoongozwa kiraia badala ya kijeshi.
16. Kiwe chama kitakacho heshimu mgawanyo wa madaraka na mihimili mingine ya Bunge na Mahakama, badala ya kugeuza mihimili hiyo kuwa Idara za Serikali yake na kuua dhana ya uangalizi (Checks and Balance).
17. Kiwe Chama kitakachowaletea watanzania viongozi mahiri, wajuzi wa siasa za ndani na Kimataifa, wakweli, waadilifu, wenye busara, nidhamu ya utendaji, huruma ambao wananchi wanafurahishwa na haiba zao katika utendaji na kujisikia huru wanapowasikia au kuwa pamoja nao.
18. Kiwe Chama ambacho Serikali yake itaanza awamu ya sita kwa kuzindua Mchakato wa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kitakachounda Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Kitakachofuta Sheria zote zinazovunja Haki za Binadamu.
19. Sifa kubwa ya mwisho ni yule mgombea wa chama ambacho kimedhihirisha kutekekeza sera za pamoja. Huyo ndiye anafaa kupewa dhamana ya uongozi wa Kata, Jimbo na Taifa.
HITIMISHO
Mwongozo huu unakusudia kuwatanabaisha Watanzania wenye dhamira njema kuzinduka na kushiriki uchaguzi huu kwa umakini ili Uadilifu, Haki, Usawa, Utu, Amani, Umoja wa kweli na Maendeleo katika Taifa letu vipatikane. Katika Taifa letu pasiwepo na vitendo vya Ufisadi, Siasa za Uongo, Ukandamizaji na Ubaguzi.
Tunatoa wito kwa Waislamu walinde heshma ya dini yao, heshma yao na ya Taifa kwa ujumla. Wajali maslahi makubwa ya Umma. Wasikubali kudanganywa kwa mambo ya kijinga kama Taasisi moja kupewa kiwanja (tena cha Waislamu wenzao) ili watumiwe kisiasa. Au Masheikh wao kupewa vijisenti hadharani sambamba na maneno ya kejeli. Kuchezwa shere kuwa wameombewa Msikiti mkubwa. Waislamu washiriki uchaguzi huu kwa lengo la maendeleo yao ya kweli na taifa kwa kuondosha Sera za Ulaghai, Ubaguzi na Ukandamizaji.
Vilevile tunatoa wito kwa waumini wa dini zote, washiriki uchaguzi kwa lengo la maendeleo na umoja wa kweli wa kitaifa. Tunawaomba kutowapa ridhaa wagombea na Vyama vyenye sera za kuwagawa Wanzania kwa mizania tofauti ya Haki na Uhuru.
Tunatoa wito kwa vyama vya siasa vikutane na makundi ya kijamii yakiwemo ya kidini kujadili kwa pamoja mustakbali wa makundi hayo na Taifa kwa ujumla. Hiyo ni Sera SHIRIKISHI ambayo maana yake ni kuangalia dosari zilizopo kwa pamoja na namna ya kuzirekebisha kwa namna bora kabisa. Vilevile ni kuweka mkataba ili kudhibiti udhaifu wakati wa utekelezaji na kuleta ufanisi wa maslahi ya kundi husika na Taifa.
Tunataraji hayo kwa sababu tunaamini watanzania wenye sifa na dhamira ya kulitumikia Taifa kwa uadilifu, ufanisi, maendeleo, kuleta usawa, matumizi sahihi ya rasilimali za Taifa na Rasiimali watu uwiano wa kijamii katika nyanja mbalimbali wapo. Na wana haki ya kikatiba ya kupewa ridhaa ya kuongoza na kuwatumikia watanzania. Waislamu tupo mamilioni tutashiriki uchaguzi kwa sura mbili: Mosi kama Watanzania na pili kama kundi la Jamii linalotaraji maslahi makubwa katika Siasa.
TUNAWATAKIA WATANZANIA WOTE UCHAGUZI WA HAKI NA AMANI.
No comments :
Post a Comment