Jumba hili la ajabu
Ukiingia na meli
Karibu hilo hujibu
Ni upenzi wa halali
Jengo hili la dhahabu
Ni huzuni kweli kweli
Kwaheri Bait al ajaibu
Wamepita babu zetu
Nao wamejalikuta
Na leo vizazi vyetu
Vinabakishiwa kuta
Iwapi thamani yetu
Wapi tutaitafuta
Nao utalii wetu
Ni wapi utajikita
Mtawala Barghashi
Kaacha historia
Milango yenye nakishi
Na ngazi za kuvutia
Marumaru nazo kashi
Sakafuni kazitia
Na nguzo zilizoishi
Karine na kuzidia
Hadhi yake jumba hili
Heshima halikupewa
Ukweli kuubadili
Usiasa ukatiwa
Vipi limethaminiwa
Bali limenajisiwa
Yalosemwa si halali
Mwasisi kusingiziwa
Mapenzi yakawa chuki
Jumba hili kuchukiwa
Maneno ya unafiki
Nguzo zilosimamiwa
Dhuluma na zetu dhiki
Jumba likaumbuliwa
Na jamii kwa malaki
Mambo wakisimuliwa
Walizikwa watu mule
Nguzo kusimamishiwa
Tumesomeshwa na shule
Uovu kuhadithiwa
Nawauliza wa kale
Ni kweli tuloambiwa?
Kupomoka jumba lile
Iwe ndo tusharudiwa?
Kama kweli twambieni
Mutunzao kumbukumbu
Na sasa tuelezeni
Msituache mbumbumbu
Jumba hili la zamani
Sura ya mji na ngambu
Limeshaanguka chini
Limeshuka nyambunyambu
Kweli hili litarudi
Kwa mazindiko ya watu
Tusifanye makusudi
Likaja athiri utu
Kama kwanguka ni radi
Tuliache twende zetu
Sura iliyojinadi
Hapo machoni mwetu
Nani asiyelijuwa
Aloishi Zanzibari
Namna lilivyokuwa
Mkabala na bahari
Lilikuwa letu uwa
Likipendeza vizuri
Ufundi ulotumiwa
Utabaki ni athari
Taa na mbele mizinga
Ililipambia jengo
Nguzo zilivyojipanga
Zimewekwa kwa mtungo
Chokaa rangi ya unga
Mikubwa yake milango
Meli zilotia nanga
Wageni husifu jengo
Ni turathi meanguka
Mamlaka mpo wapi
Utafiti wa hakika
Tujue chanzo ni kipi
Idara inohusika
Mnatuambia lipi
Pindi nyoyo taridhika
Beiti yetu ipo wapi
Tunalia kuondoka
Kama ilopigwa bomu
Na manowari ya vita
Lina historia tamu
Kwa mambo liloikuta
Mwenye akili timamu
Kumbukumbu hutafuta
Hasikizi yenye sumu
Ukweli hatoupata
La ajabu jengo hili
Kwenye bara ya swahili
Sifaze mefika mbali
Ukandawe wa saheli
Si sifa ya idhilali
Kwa wajuao ukweli
Hasa kusini ya mbali
Likitajwa jengo hili
Tenda mpya itangazwe
Jengo lisimame tena
Barghashi apongezwe
Asitajwe kwa laana
Mji na uendelezwe
Pasiwe kiwanja tena
Ramani na ichunguzwe
Mjenzi awe wa Maana
Haya mambo usanifu
Na waitwe waturuki
Wao watu maarufu
Nakishi wazimiliki
Wana historia ndefu
Wajenzi si wazandiki
Makka mji maarufu
Tenda wamezimiliki
Litajengwa kama kale
Tulione lilelile
Litwikwe mnara ule
Saa isiyo kelele
Umwagwe mchele tule
Siku hiyo tusilale
Waomani walewale
Riyali wazilipile
Pole beiti ajaibu
Kwa dhara ilokufika
Makovu tutayatibu
Kweli iondoe shaka
Matusi yalokuswibu
Hata ukaporomoka
Sasa yondoke sababu
Sote tuje faidika.
/Mtunzi ni Shk, Moh'd Suleiman Hibri!
No comments :
Post a Comment