THE PEOPLE'S BANK. THE PEOPLE'S CHOICE!
Mkurugenzi huyo alikuwa akiijibu barua ya tarehe 12 Machi, 2021 kutoka Jumuiya ya Zacadia ya Canada, ambayo ilikuwa ikiitaka benki hio iwaruhusu Wazanzibari wa nje wafunguwe Diaspora Accounts kwenye benki yake.
Aliianza barua yake Mkurugenzi huyo kwa kuandika..."Kwanza ningependa niwashukuru sana kwa kunipa pongezi zinazotokana na uteuzi uliofanywa na Mhe Rais wa Zanzibar kwangu kushika nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ). Na nawaahdi kwamba nitajitahidi kadri ya uwezo wangu, pamoja na kushirikiana na wafanyakazi wa benki kuyatafutia majawabu na ufafanuzi maswala mbali mbali yanayojitokeza katika mashirikiano yetu baina ya PBZ na ZACADIA".
Aliendelea Mkurugenzi huyo..." Pia ningelipenda kuwapongeza kwa juhudi zenu mbalimbali mnazozichukuwa katika kuwakumbuka ndugu na jamaa walioko huku nyumbani na kubwa zaidi kwa kusaidia maendeleo ya Zanzibar kwa kuleta misaada mbalimbali inayohitajika huku...".
"Kuhusiana na akaunti ya Diaspora, ningelipenda kuwahakikishia kwamba bado ipo katika Benki ya Watu wa Zanzibar. Akaunti hii ni kwa ajili ya Watanzania wanaoishi nje ya Tanzania. Na maana ya Watanzania ni wale wanaoishi nje lakini bado wana hati za kusafiria za Tanzania. Akaunti ya Diaspora inaweza kuwa ya akiba (Saving), ya biashara (Current), au ya muda maalum (Fixed Deposit) kwa sarafu za Dollar ya Kimarekani, Sterling Pound ya Uingereza, Euro na Shillingi ya Tanzania".
Kwanini Benki hio iliwaweka Wana-Diaspora kwenye mataa tokea 2015 bila ya majibu yoyote yale? Mkurugenzi huyo mpya wa Benki ya Watu wa Zanzibar alijibu kwa kuandika..."Kwa muda mrefu benki ya Watu wa Zanzibar ilikuwa ikisubiri mabadiliko ya Katiba ya nchi hasa ya mwaka 2015 ambako kulikuwa na mapendekezo mbalimbali ya Katiba miongoni mwa hayo ni kuruhusu raia wa Tanzania kuwa na uraia zaidi ya mmoja, lakini mchakato ule haukukamilika. Kwa hiyo tafsiri ya Mtanzania kwa wale walioko nje kikatiba iliendelea kubaki vile vile ni kwa yule mwenye pasi ya kusafiri ya Tanzania", alifafanua Mkurugenzi huyo.
Mkurugenzi huyo alimaliza barua yake kwa kuwahakikishia Wana-Zacadia na Wazanzibari wote waishio nje kuwa..." Benki ya Watu wa Zanzibar itaendelea kuwajali na kuwaunga mkono katika shughuli mbalimbali kwa mujibu wa taratibu za nchi ili kuweza kufanikisha maswala mbalimabli ya kimaendeleo", ilimalizia barua hio.
Blog la ZanzibarNiKwetu lilimtafuta kwa uvumba na udi Vice-President wa Zacadia ili atoe tafsiri ya barua hio, lakini hakupatikana kwa simu na badala yake blog likampelekea WhatsApp msg ili atoe tafsiri ya barua hio ya Mkurugenzi.
Katika majibu yake ya WhatsApp Vice-President huyo wa Zacadia aliandika na tunanukuu... "Barua ya majibu ya Mkurugenzi wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) ilikuwa self-explanatory na kwahivyo haitaki maelezo zaidi au tafsiri yoyote ile. Jambo hili tunajua lingelisaidia kuipatia fedha za kigeni Zanzibar na kwahivyo hatuwezi kustahamili pale tunapoenguliwa katika juhudi za kuchangia maendeleo ya nchi yetu ya Zanzibar. Hivyo basi, tumeamua kumuandikia barua rasmi Rais wa Zanzibar Dkt Hussein Mwinyi ili aitengue sheria hii iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania, kwasababu Zanzibar inavyanzo vichache vyakupatia fedha za kigeni", alimalizia kiongozi huyo wa Zacadia.
No comments :
Post a Comment