Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, October 23, 2021

SHAIRI - "Yuwapi yule kijana, alietaka kuoa?"


YUWAPI YULE KIJANA, ALIETAKA KUOA?

Namshukuru Jalala, nimetuwa Maskati,
Nitafika na Salalah, pamoja na Kharfati,
Saa hizi mmelala, ngoja ufike wakati,
Yuwapi yule kijana, alietaka kuoa?

Alikuja kule kwetu, akaanzia Unguja,
Akapelekwa Tumbatu, kutafuta wa faraja,
Kule hakupata kitu, alikosa yake haja,
Yuwapi yule kijana, alietaka kuoa?

Alifika na Kiboje, wengi aliwaahidi,
Sijui ilikuwaje, kwasababu hakurudi,
Nimeona bora nije, kimya chake kinazidi,
Yuwapi yule kijana, alietaka kuoa?

Alietaka kuoa, yuwapi yule kijana,
Alikwenda na Uroa, kutafuta msichana,
Karibu afunge ndoa, Shekhe hakupatikana,
Yuwapi yule kijana, alietaka kuoa?

Alipita Mchangani, akitokea Koani,
Akasimama Mtoni, na kulala Mazizini,
Ghafla hatumuoni, ameingia gizani,
Yuwapi yule kijana, alietaka kuoa?

Unguja akatoroka, kaibukia Kojani,
Na sote tukashituka, kafika vipi jamani?
Kumbe kavushwa na Jaka, mpaka kule Pujini,
Yuwapi yule kijana, alietaka kuoa?

Tukaa vichwa kushika, roho zetu hamkani,
Mbona anahangaika, huyu mwanetu mgeni?
Tukaamua haraka, atafutiwe mwandani,
Yuwapi yule kijana, alietaka kuoa?

Kajulishwa na Fatuma, alikuwa mwari ndani,
Na pete akaituma, na tukawa furahani,
Mara karudi nyuma, akarejea Omani,
Yuwapi yule kijana, alietaka kuoa?

Maskati nimefika, kujua yuhali gani,
Na kama kakasirika, kwa mahari bilioni, 
Kwa mkwewe nitafika, kumuomba afuweni, 
Yuwapi yule kijana, alietaka kuoa?

Kwa kila asikiae, mjulisheni jamani,
Nataka onana nae, mimi nipo hotelini,
Na sina nimjuae, Maskati ni mgeni,
Yuwapi yule kijana, alietaka kuoa?



1 comment :

  1. Tunakaribisha mashairi (bila ya inappropriate words) ili ku-enjoy utamu wa lugha yetu.
    ZNK - Admin.

    ReplyDelete