Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, November 20, 2021

SHAIRI: BIDADA AAMBIWA NA FATUMA..."KAMA WEWE HUNA KAKA, BASI NIWE WAKO MWENZA"!

Yaliopita sindwele, sisi tugange yajayo,
Nakuamini milele, Bidada uyasemayo,
Wewe ni mtu wa kale, tafuata zako nyayo,
Ahsante Bidada, nasaha zako nzuri.

Nangoja hio neema, taipokea kwa hamu,
Namuomba ya Karima, nipate muislamu,
Kama yule wa Haima, liejaa tabasamu,
Ahsante Bidada, nasaha zako nzuri.

Yakale sio maisha, sitaki kuyakumbuka,
Babu wamuhangaisha, pia Omani kafika,
Kataka kupatanisha, rafiki hakuridhika,
Ahsante Bidada, nasaha zako nzuri.

Kupatanisha kataka, rafiki hakuridhika,
Kamtoa muhusika, akaenda Jamaika,
Na ikawa patashika, hata nguo kuchanika,
Ahsante Bidada, nasaha zako nzuri.

Ukichangia harusi, kweli nitafurahia,
Wewe lete mifulusi, hio ya ki-Kanadia,
Wala sitokufilisi, we huko milionia,
Ahsante Bidada, nasaha zako nzuri.

Hivyo huna hata ndugu, mimi kujakuniposa?
Tukaujenga udugu, siwe ni mwanasiasa,
Kwani sitaki vurugu, ninapoanza kurasa,
Ahsante Bidada, nasaha zako nzuri.

Nikisema nisubiri, tachukuwa hadi mwaka,
Nani mwenye kufikiri, kila mtu aepuka,
Mahari chache dinari, elfu hazitofika,
Ahsante Bidada, nasaha zako nzuri.

Utakuwa wangu wifi, muhimize wako kaka,
Mtie hata vikofi, aje kuposa haraka,
Wanaume wakorofi, wa kwanza alitoroka,
Ahsante Bidada, nasaha zako nzuri.

Na kama hunae kaka, basi niwe wako mwenza,
Sisemi kukudhihaka, hatutokuwa wa kwanza,
Nina kazi ya hakika, kwahivyo ninajiweza,
Ahsante Bidada, nasaha zako nzuri.

Mwenza sina wasiwasi, najua umetulia,
Bwana kila Jumamosi, garini atakutia,
Siku ya Alkhamisi, na kwangu atapitia,
Ahsante Bidada, nasaha zako nzuri.

Bidada unayaweza, kwani nakujua mie,
Najua tanisikiza, sote tuwe mabibie,
Haya ukiyatimiza, PEPO SHAKA USITIE,
Ahsante Bidada, nasaha zako nzuri.

Kushea ni wislamu, kuchepuka ni haramu,
Ndoa ni kitu adhimu, kwa sote wanaadamu,
Inafaa tufahamu, wivu mwingi ni wazimu,
Ahsante Bidada, nasaha zako nzuri.

Inafaa tufahamu, wivu mwingi ni wazimu,
Bidada ushahitimu, kwangu takuwa mwalimu,
Kutokana na takwimu, mke mmoja ni sumu,
Ahsante Bidada, nasaha zako nzuri.

Kutokana na takwimu, mke mmoja ni sumu,
Utamtakia sumu, huyo wako muadhamu?
Bidada kweli muhimu, tuje kuwa na nidhamu,
Ahsante Bidada, nasaha zako nzuri.

Siku sita kwako wewe, siku moja kwangu mimi,
Mkarimu ndio niwe,  tusije pigana ngumi,
Mimi nawe tuelewe, sisi sote ni wasomi,
Ahsante Bidada, nasaha zako nzuri.

Sasa bora nasimama, namngoja wako kaka,
We ni mtu wa huruma, kwako sinayo mashaka,
Najua hutonisema,  kuolewa ni baraka,
Ahsante Bidada, nasaha zako nzuri.

Fatuma binti Faki / Zanzibar, November 19, 2021.


1 comment :

  1. Nakubaliana na huyu dada Fatma kuwa;
    "Kutokana na takwimu, mke mmoja ni sumu".
    Ni kweli kabisa mke mmoja ni sumu. Ukitaka kuitoa sumu kwenye nyumba engeza wapili!

    ReplyDelete