Nimeona nije kwako, kueleza kirafiki,
Nipata mwaliko wako, harusi ijayo wiki,
Kaa na akili yako, mume soyule Faruki.
Faruki hachukuliki, ni bora asikuowe,
Kijana afahamiki, posa isipokelewe,
Kama keshakumiliki, shauri yako mwenyewe,
Kaa na akili yako, mume soyule Faruki.
Kufunga ndoa na yeye, ni kujitia kitanzi,
Matatizo baadaye, ya kuhusu matumizi,
Yatakuja hatimaye, kabla kutimu mwezi,
Kaa na akili yako, mume soyule Faruki.
Aitwa Kono la Chuma, hatoi hata Shilingi,
Na wengi wanamsema, kama anavuta bangi,
Sijui yake hatma, lakini sisemi mengi,
Kaa na akili yako, mume soyule Faruki.
Huyu mtu humuwezi, bora mwachilie mbali,
Kwanza si mfanyakazi, wala hana maadili,
Utakujakosa razi, zao wazee wawili,
Kaa na akili yako, mume soyule Faruki.
Hanalo shamba la miwa, labda la mitunguje,
Yaonesha kaghumiwa, na hapa bora asije,
Na kama akipokewa, basi mwisho kule nje,
Awapeleka kulima, Habibu pia Shaibu!!!
Hawatokei mrima, si wa kazi za sulubu,
Nini wanachomnyima, wakiwa wao karibu?
Kaa na akili yako, mume soyule Faruki.
Keshaacha wake sita, wewe takuwa wasaba,
Kampita hata Pita, au yule Alibaba
Maisha yako tafuta, sitegemee kahaba,
Kaa na akili yako, mume soyule Faruki.
Eti harusi haraka, na ndani hatoingia,
Huyu mtu ninashaka, tayari keshaumia,
Na sasa anakutaka, aighilibu dunia,
Kaa na akili yako, mume soyule Faruki.
Siamini Mkojani, asijeingia ndani,
Atakuwa furahani, kweli hapo harusini?
Sijui wake undani, hapa pana ulakini,
Kaa na akili yako, mume soyule Faruki.
Yeye ukimfuata, nawe atakukimbia,
Machozi atakufuta, sita aliwafanyia???
Kweli huyu ni matata, kwa anayokuambia,
Kaa na akili yako, mume soyule Faruki.
Usijeniona kaka, nimekuja kufujia,
Lazima nije haraka, kukunyooshea njia,
Shemeji ninamtaka, lakini huyu gunia,
Kaa na akili yako, mume soyule Faruki.
Wacha sasa niondoke, nipite kwa dada yako,
Nia yangu uamke, wasijepata kicheko,
Sitaki uhadaike, ukafanywa kifuniko,
Kaa na akili yako, mume soyule Faruki.
Juma Faki / Zanzibar, November 06, 2021.
No comments :
Post a Comment