Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, November 14, 2021

SHAIRI: FATUMA AMSHUKURU BIDADA KWA USHAURI ALIOMPA!


Ahsante Bidada, kwa ushauri wa dhati,
Wewe kwangu kama dada, kukupata ni bahati,
Nilete huko Canada, hata kwa kupanda boti,
Sante kwa ushauri, kutoka kwako Bidada.

Ni ushauri wa haki, kweli nimeusikia,
Yote ninayaafiki, mimi bora kutulia,
Sisemi haya kwa chuki, bali nimefikiria,
Sante kwa ushauri, kutoka kwako Bidada.

Dua kweli ni muhimu, pamoja na aya kursi,
Kila siku tajihimu, kuisomea nafsi,
Natafuta na mwalimu, anitoe hi nuksi,
Sante kwa ushauri, kutoka kwako Bidada.

Nasubiri mume mwema, In Sha Allah atanijia
Mwenye wingi wa huruma, si hawa waruka njia,
Na tena aliesoma, huyo namtarajia,
Sante kwa ushauri, kutoka kwako Bidada.

Faruki hasingiziwi, kweli bangi anavuta,
Lakini hashitakiwi, rafikize ni shurta,
Sijui vipi ukimwi, ningelikuja kujuta,
Sante kwa ushauri, kutoka kwako Bidada.

Tena muongo Faruki, hana hata kampuni,
Yeye ni mtu wa dhiki, mwenye hali ile duni,
Hana anachomiliki, labda ni moja seruni,
Sante kwa ushauri, kutoka kwako Bidada.

Sasa namngoja Kaka, amrejeshee pete,
Mola mwenye madaraka, mimi sijui chochote,
Wazimu ulinishika, Bidada usikupate,
Sante kwa ushauri, kutoka kwako Bidada.

Nilizipenda tabia, za mchumba wa Haima,
Kwake nilifurahia, ngekula kuku kwa uma,
Siwezi kumjutia, ndio kazi ya Rahima,
Sante kwa ushauri, kutoka kwako Bidada.

Nitaleta mualiko, na wewe takuwa kungwi,
Harusi yangu ni yako, tutaifanyia Nungwi,
Huko Kaka ndo aliko, kufika ni kwa  mtumbwi,
Sante kwa ushauri, kutoka kwako Bidada.

Kwa leo sina zaidi, sante kwa ushauri,
Kuandikiana tuzidi, huku sasa alasiri,
Mpe salam Hemedi, na ndugu yake Bashiri,
Sante kwa ushauri, kutoka kwako Bidada.

Fatuma binti Faki / Zanzibar, November 14, 2021.


2 comments :

  1. This comment has been removed by the author.

    ReplyDelete
  2. ZanzibarNiKwetu inakaribisha mashairi na habari zozote zile za kuielimisha jamii. Lugha chafu haitostahamilika.
    If you have anything to be posted, write to us at: znzkwetu AT gmail.com
    Kila la kheri / ZNK Admin.

    ReplyDelete