Barua ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa CHADEMA si barua ya kawaida ya kiutawala.
Ni kioo cha tatizo kubwa zaidi linaloitesa Tanzania: sheria inapogeuzwa kuwa rungu kwa wapinzani, lakini inapogeuka blanketi la kuwafunika watawala.
Msajili anapoiita CHADEMA kutoa maelezo kwa kauli zake za kisiasa, hasa kuhusu “No Reforms No Election”, madai ya kuachiwa kwa Tundu Lissu na msimamo wake juu ya Tume ya Chande, swali la kwanza si kama Msajili ana ofisi.
Swali ni kama ofisi hiyo inasimama juu ya Katiba au juu ya hofu ya chama tawala.
Kwa mujibu wa nyaraka za CHADEMA, chama hicho kilizuiwa kufanya shughuli zake kwa siku 309 hadi Mahakama ya Rufaa ilipoondoa zuio hilo. CHADEMA pia inasema zuio hilo liliwanyima mamilioni ya wanachama, wafuasi na wapenzi wake haki ya kufanya siasa chini ya Ibara ya 20, 21 na 29 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Huo si mgogoro mdogo wa chama,ila ni mgogoro wa haki ya wananchi kushiriki katika maisha ya kisiasa ya nchi yao. 
Sasa chama kilichofungiwa karibu mwaka mzima, kikafunguliwa na Mahakama, kinaanza tena kutishiwa kwa barua ya Msajili.
Hii si bahati mbaya.
Ni mwendelezo wa utaratibu ule ule: fungia, chelewesha, tisha, kamua, halafu dai nchi ina demokrasia ya vyama vingi.
Lakini jambo linalofanya barua ya Msajili iwe fedheha zaidi ni unafiki wake.
Kama kweli Ofisi ya Msajili inasimamia sheria kwa usawa, CCM ilishawahi kuitwa lini kutoa maelezo kwa kauli ya Mwenyekiti wa UVCCM Kagera, Faris Buruhan, aliyeripotiwa kusema watu wanaomtukana Rais wakipotezwa Polisi wasiwatafute?
Kauli hiyo iliripotiwa na vyombo vya habari na hata Ngara TV ikaandika kuwa Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Dkt. Emanuel Nchimbi, aliikemea kama kauli ya kijinga. 
Sasa tujiulize kwa sauti ya juu: kama “No Reforms No Election” ni uchochezi, basi “tukiwapoteza Polisi msiwatafute” ni nini?
Kama kudai mageuzi ya uchaguzi ni hatari kwa amani, basi kutishia kupoteza watu ni nini?
Kama kuhoji kesi ya Tundu Lissu ni kuvuruga utaratibu, basi lugha ya kupoteza wakosoaji wa Rais inaitwaje katika nchi yenye Katiba, Polisi na sheria?
Hapo ndipo Ofisi ya Msajili inapoonekana si mlezi wa vyama vya siasa, bali mlinzi wa usawa bandia. Kwenye ukurasa wa taarifa za hadharani wa Ofisi ya Msajili, kuna taarifa ya Mei 28, 2025 kuhusu msimamo dhidi ya CHADEMA, lakini katika rekodi hiyo hiyo ya hadharani haionekani taarifa inayolingana ikiitaka CCM kujibu kwa kauli ya UVCCM Kagera.  Kama barua hiyo ipo, iwekwe hadharani.
Kama haipo, basi Msajili aache kuhubiri sheria kwa jicho moja.
Kwa sababu hapa si hoja ya CHADEMA tu. Hapa ni hoja ya Ibara ya 13 ya Katiba kuhusu usawa mbele ya sheria.
Ni hoja ya Ibara ya 14 kuhusu haki ya kuishi. Ni hoja ya Ibara ya 18 kuhusu uhuru wa maoni. Ni hoja ya Ibara ya 20 kuhusu haki ya kushiriki vyama vya siasa.
Ni hoja ya Ibara ya 21 kuhusu wananchi kushiriki katika uongozi wa nchi yao.
Sheria ya Vyama vya Siasa haiwezi kuwa juu ya Katiba.
Na Msajili hawezi kuitumia sheria hiyo kama pingu kwa wapinzani huku akiacha chama tawala na vijana wake wakitoa lugha ya vitisho kwa kifua mbele.
Hii ndiyo sababu hoja ya CHADEMA kuhusu Tume ya Chande haiwezi kufutwa kwa barua ya vitisho.
Tume hiyo ilitakiwa kujibu maswali mazito: nani alitoa amri? Nani alitumia nguvu kupita kiasi? Kwa nini ripoti kamili haijawekwa hadharani? Kwa nini wananchi waambiwe wakubali hitimisho la hotuba badala ya kusoma ushahidi? Kwa nini familia za waliopoteza wapendwa wao ziamini maridhiano bila ukweli?
UDASA, si CHADEMA, imesema baada ya kupitia wasilisho la Jaji Chande, imebaini zaidi ya mambo hamsini yanayokera wananchi na yanayopaswa kufanyiwa kazi ili kuepuka machafuko mengine. Miongoni mwa hayo ni kukosekana kwa Katiba Mpya, Tume ya Uchaguzi kutokuwa huru, Jeshi la Polisi kutokutenda haki, watu kutekwa na kupotezwa, kukosekana kwa uwanja sawa wa kisiasa na Msajili wa Vyama pamoja na Tume ya Uchaguzi kushindwa kushughulikia kero na malalamiko ya vyama na wananchi. 
Hiyo ndiyo hoja kubwa. Msajili si mtazamaji nje ya mgogoro. Ametajwa kama sehemu ya tatizo. Ofisi yake inapaswa kujitazama, si kuandika barua za kutisha wale wanaolalamika kuhusu mfumo uliokwama.
TLS nayo imeweka kidole kwenye jeraha. Imesema, kwa tathmini yake, yaliyotokea kwa sehemu kubwa yamechangiwa na taasisi kama Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jeshi la Polisi, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, marekebisho ya sheria za uchaguzi yasiyozingatia maoni ya wadau, na Mahakama kushindwa kutekeleza wajibu wake wa kuzuia matumizi mabaya ya madaraka.
Hili si tamko la mitaani.
Ni sauti ya wanasheria wanaoitazama nchi kwa jicho la utawala wa sheria.
Na kama bado watawala wanadhani haya ni maneno ya “wapinzani wenye hasira,” basi wamsikilize Jaji Joseph Sinde Warioba.
Warioba si mwanaharakati wa mitandao. Si kijana wa hasira. Si msemaji wa CHADEMA.
Ni Waziri Mkuu mstaafu, Mwanasheria Mkuu wa zamani, mwenyekiti wa Tume ya Katiba, na mmoja wa wazee wachache wa taifa wenye historia, uadilifu na ujasiri wa kusema ukweli hata ukiwaumiza watu wa nyumbani kwake kisiasa.
Katika mahojiano marefu na The Chanzo na The Jenerali Ulimwengu Post, Warioba alisema uchaguzi wa Oktoba 2025 ulifanyika kwa namna iliyoiletea nchi aibu, na kwamba vurugu zilizofuata zilisababisha wananchi wengi kupoteza maisha. Alisema pia Watanzania walitarajia kuona ripoti ya Tume ya Chande, si kusikia kuwa ni mali ya Rais. 
Hapo ndipo hoja ya Warioba inakuwa nyundo ya kimaadili. Kama Tume iliundwa kwa ajili ya taifa, kuhusu majeraha ya taifa, kwa gharama za taifa, basi ripoti yake haiwezi kufungwa kama mali binafsi ya Ikulu.
Warioba amesisitiza kuwa ripoti kamili na viambatanisho vyake vinapaswa kutolewa ili wananchi wajue kilichotokea na sababu zake. 
Huo ndio msingi wa maridhiano.
Si hotuba. Si vitisho. Si barua za Msajili. Si kumwambia aliyeumizwa anyamaze ili nchi ionekane imetulia.
Maridhiano huanza na ukweli. Ukweli huzaa uwajibikaji. Uwajibikaji huzaa imani.
Imani huzaa amani.
Bila hayo, kinachoitwa amani ni ukimya wa kulazimishwa.
Warioba amekumbusha pia misingi ya taifa: usawa, haki, umoja, mshikamano, uzalendo na amani.
The Chanzo imeripoti kuwa alihusisha misingi hiyo na TANU ya 1954 na ahadi za awali za kujenga taifa lisiloongozwa na ubaguzi, rushwa, hofu na madaraka binafsi.  Hii ndiyo sehemu inayowaumiza zaidi CCM wa sasa.
Warioba haihukumu CCM kwa lugha ya upinzani. Anaihukumu CCM kwa kutumia mizani ya TANU na CCM ya mwanzo.
Kwa lugha rahisi: CCM ya sasa haishindwi na CHADEMA tu. Inashindwa na kivuli cha asili yake yenyewe.
CCM ya TANU ilijenga hadithi ya ukombozi, umoja na uadilifu. CCM ya sasa inatuhumiwa kujenga utamaduni wa “dola kubaki na dola,” uchaguzi usioaminika, viongozi wanaotoa vitisho, vyombo vya dola vinavyotazamwa kwa hofu, na taasisi zinazotumika kubana upande mmoja wa siasa.
Hapo ndipo taifa linapaswa kusimama na kusema: hili si jambo la kawaida.
Kuna viongozi wa CCM na dola ambao kwa miaka kadhaa wamezungumza lugha za kutisha, lugha za kuadhibu, lugha za “kuanza nao,” lugha za “kupoteza,” lugha za kuonya watu wasali sala zao kabla ya kuandamana.
Baadhi ya kauli hizo zimenukuliwa kwenye tamko la CHADEMA, ikiwemo ile inayodaiwa kutolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, kabla ya Oktoba 29.
Sasa swali ni hili: kwa nini lugha hizo haziionekani kama tishio kwa amani mbele ya Msajili, lakini madai ya Katiba Mpya yanaonekana kama hatari?
Kuna kitu kimeharibika sana pale serikali inapoogopa kaulimbiu ya mageuzi kuliko lugha ya kupoteza watu.
Kuna kitu kimeharibika sana pale Ofisi ya Msajili inapomwona mpinzani anayesema “No Reforms No Election” kama tatizo, lakini inashindwa kuonyesha kwa uwazi hatua sawia dhidi ya wale wanaozungumza lugha inayogusa uhai wa raia.
Kuna kitu kimeharibika sana pale Jaji Warioba, UDASA, TLS na CHADEMA wote kwa njia tofauti wanagusa mzizi mmoja, lakini serikali inachagua kushughulika na matawi ya maneno badala ya mizizi ya udhalimu.
Na mzizi ni huu: Tanzania imefikishwa mahali ambapo taasisi zimeanza kutumiwa kulinda madaraka badala ya kulinda wananchi.
Polisi wanapaswa kulinda raia, si kuogopwa na raia. Tume ya Uchaguzi inapaswa kulinda kura, si kulinda ushindi wa walioko madarakani.
Msajili wa Vyama anapaswa kulinda mfumo wa vyama vingi, si kudhibiti chama kikuu cha upinzani.
Mahakama zinapaswa kuwa kimbilio la haki, si sehemu ambayo wananchi wanaiangalia kwa mashaka. Serikali inapaswa kusikiliza, si kutisha.
Tukisema haya, hatusemi kwa sababu tunaichukia Tanzania. Tunasema kwa sababu hatutaki Tanzania iendelee kugeuzwa nchi ya watu wenye hofu.
Taifa halijengwi kwa raia kunong’ona. Taifa halijengwi kwa vijana kuogopa kusema. Taifa halijengwi kwa vyama vya siasa kuishi kwa ruhusa ya mhemko wa Msajili.
Taifa halijengwi kwa ripoti za umma kufichwa kwenye makabati ya Ikulu.
Ikiwa serikali inaamini CHADEMA inakosea, ijibu kwa hoja. Ikiwa inaamini Tume ya Chande ilifanya kazi nzuri, iweke ripoti yote hadharani. Ikiwa inaamini uchaguzi ulikuwa halali, iruhusu mjadala huru wa kitaifa kuhusu uchaguzi huo.
Ikiwa inaamini Msajili anasimamia sheria kwa usawa, ionyeshe hatua alizochukua dhidi ya CCM kwa kauli za viongozi wake zilizotishia wananchi.
Ikiwa hakuna hatua hizo, basi waache kututukana kiakili.
Sheria si sheria ikiwa inawakaba wapinzani na kuwaacha watawala.
Amani si amani ikiwa inajengwa juu ya woga.
Maridhiano si maridhiano ikiwa yanaanza kwa kuficha ripoti na kuwatisha wanaouliza maswali.
Na hapa ndipo Warioba anaposimama kama dhamiri ya taifa. Anachosema ni rahisi lakini kizito: turudi kwenye misingi.
Misingi ya ukweli.
Misingi ya haki.
Misingi ya uongozi kama dhamana.
Misingi ya uchaguzi unaotokana na ridhaa ya wananchi.
Misingi ya taifa ambalo mtu hasemi kwa kuangalia nyuma kama kuna gari linamfuata.
Kwa hiyo, barua ya Msajili kwa CHADEMA ni zaidi ya barua. Ni jaribio la kuamua kama Tanzania itaendelea kuwa nchi ya Katiba au nchi ya vitisho vilivyopakwa wino wa sheria.
Na jibu letu linapaswa kuwa wazi: kama kuna chama kinapaswa kuitwa kutoa maelezo, si CHADEMA peke yake.
CCM iitwe pia.
UVCCM iitwe.
Viongozi wote waliotoa lugha za vitisho waitwe.
Wote waliochochea chuki, hofu, utekaji, udhalilishaji au matumizi ya nguvu dhidi ya wapinzani waitwe.
Sheria ikianza na mpinzani pekee, hiyo si sheria.
Huo ni upendeleo.
Tanzania haitapona kwa kufuta sauti ya CHADEMA. Haitapona kwa kumtisha Lissu. Haitapona kwa kuficha ripoti ya Chande. Haitapona kwa kumpuuza Warioba. Haitapona kwa kugeuza Msajili kuwa mlinzi wa watawala.
Tanzania itapona pale ukweli utakapoacha kuonekana kama uchochezi.
Itapona pale dola itakapoogopa kupoteza raia kuliko inavyoogopa kupoteza uchaguzi.
Itapona pale CCM itakapokumbuka kuwa TANU haikujengwa ili siku moja chama tawala kigeuke kivuli cha hofu yake yenyewe.
Na itapona pale Katiba itakapokuwa juu ya chama,
juu ya Msajili, juu ya Polisi, juu ya Tume, na juu ya Ikulu.
Mpaka hapo, barua yoyote dhidi ya CHADEMA haitasomwa kama ulinzi wa sheria.
Itasomwa kama ushahidi mwingine wa mfumo unaoogopa haki.

No comments :
Post a Comment