Written by abdulwaheed // 21/11/2012 // Habari // 2 Comments
Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari, jana walizuiwa kufuatilia kesi inayowakabili viongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu (Jumiki) katika Mahakama Kuu mjini Zanzibar.
Kesi hiyo ilifikishwa mbele ya Mrajis wa Mahakama Zanzibar, George Joseph Kazi, kwa ajili ya kutolewa uamuzi wa ombi la washtakiwa kutaka kuruhusiwa pamoja na mambo mengine, kuonana na jamaa zao.
Katika ombi hilo washtakiwa, pia wanataka mahakama iwaruhusu kupelekewa chakula, kusoma vitabu, vikiwamo vya dini, kuswali na kuchanganyika na mahubusu wengine badala ya kuwekwa kila mmoja katika chumba maalum peke yake.
Viongozi hao, ambao kesi yao ya msingi inasikilizwa na Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Mwanakwerekwe, Ame Masaraka Pinja, ni pamoja na Kiongozi wa Jumiki, Sheikh Farid Hadi Ahmed.
Wengine ni Mselem Ally Mselem, Mussa Juma Issa, Suleiman Juma Suleiman, Azan Khalid Hamdan, Khamis Ali Suleiman, Hassan Bakar Suleiman na Ghalib Ahmada Omar.
Kwa pamoja viongozi hao wanatuhumiwa kuchochea vurugu na kusababisha uvunjifu wa amani na uharibifu wa mali mbalimbali mjini Zanzibar kati ya Oktoba 17 na 18, mwaka huu.
Wote walikana mashtaka hayo kesi hiyo ilipofikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Oktoba 22, mwaka huu na kupatiwa dhamana, lakini walishindwa kutoka mahabusu kwa kuwa wana kesi nyingine katika Mahakama Kuu, ambayo dhamana yake imewekewa pingamizi na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).
Lakini wakati kesi hiyo ilipofikishwa mbele ya Mrajis huyo wa Mahakama Kuu Zanzibar jana kwa ajili ya kutoa uamuzi juu ya ombi la washitakiwa kuruhusiwa kufanya ibada, kupelekewa chakula na kukaa na mahabusu wengine, waandishi wa habari hawakuruhusiwa kuingia katika chumba cha mahakama.
Askari polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) walitumia magongo kama kizuizi kilichowalenga waandishi wa habari waliotaka kufuatilia kesi hiyo katika Mahakama Kuu iliyopo maeneo ya Vuga mjini hapa.
Badala yake, waandishi pekee walioruhusiwa kuingia katika chumba cha mahakama hiyo ni wa gazeti la serikali la Zanzibar Leo na mwingine kutoka vyombo vya ulinzi.
Hata hivyo, mwandishi kutoka vyombo vya binafsi, Munir Zakaria, wa Channel Ten, alifanikiwa kuingia katika chumba hicho baada ya kuwazidi ujanja maofisa wa FFU kwa kupenya na kuingia bila kugunduliwa.
Baada ya mawakili wa upande wa utetezi kusoma maombi ya washtakiwa, Mrajis huyo anayesikiliza kesi hiyo aliiahirisha hadi Novemba 29, mwaka huu na washitakiwa wote walirudishwa rumande baada ya maelelzo ya waendesha mashtaka kwamba, upelelezi bado haujakamilika.
Akiahirisha kesi hiyo, Mrajis huyo aliwashauri washitakiwa kufungua kesi ya madai juu ya madai yao kwamba, hawatendewi haki, ikiwa ni pamoja na kunyolewa ndevu kabla hawajatiwa hatiani na kuhukumiwa kwa kesi inayowakabili.
Sababu za Jeshi la Polisi kuwazuia waandishi wa habari kuingia katika chumba cha mahakama hazikufahamika mara moja, lakini baadhi ya maofisa wa mahakama walidai kuwa chumba ni kidogo.
Chanzo: Mzalendo
No comments :
Post a Comment