Viongozi wa Jumiki
16th January 2013
Viongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki), wamefungua kesi tena Mahakama Kuu wakipinga dhamana yao kufungwa na Mkurugenzi wa Mashitaka dhidi ya kesi inayowakabili ya uharibifu wa mali na kuhatarisha usalama wa taifa.
Kesi hiyo imefunguliwa na Wakili anayewatetea washtakiwa hao, Abdallah Juma Mohamed, baada ya awali kesi hiyo kufunguliwa kinyume cha sheria na kulazimika kutupwa na Jaji wa Mahakama Kuu, Mkusa Isaack Sepetu Desemba 19, mwaka jana.
Akizungumza na NIPASHE ofisini kwake Vuga Mjini hapa jana, Mrajisi wa Mahakama Kuu, George Kazi, alisema kesi hiyo imepangwa kusikilizwa na Jaji Abraham Mwapashi, mwaka huu.
Alisema viongozi wa Uamsho wanataka Mahakama Kuu ifanye mapitio kuhusu uamuzi wa Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar, Ibrahim Mzee Ibrahim, kutoa kibali cha kufunga dhamana dhidi ya washtakiwa 10 katika kesi hiyo.
Hata hivyo, Mrajisi Kazi, alisema kutokana na kufungua kesi hiyo, kesi ya msingi inayowakabili viongozi wa Uamsho inalazimika kusimama hadi maamuzi yatakapotoka dhidi ya kesi waliyofungua viongozi hao.
Alisema kesi ya msingi ya viongozi hao imepagwa Januari 28, mwaka huu kwa kutajwa kabla ya kuanza kusikilizwa kesi waliyofungua baada ya Jaji Mwapashi, aliyepagwa kusikiliza kesi hiyo kumaliza likizo yake.
Viongozi waliofungua kesi hiyo ni Farid Hadi Ahmed, Mselem Ali Mselem, Mussa Juma Issa, Azani Khalid Hamdani na Suleiman Juma Suleiman.
Wengine ni Khamis Ali Suleiman, Hassan Bakari Suleiman, Gharib Ahmada Omar, Abdallah Said Ali na Fikirini Majaliwa Fikirini.
Viongozi wa Uamsho wapo mahabusu katika Gereza la Kinua Miguu tangu Oktoba 21, mwaka jana, baada ya dhamana yao kufungwa.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment