NA MUHIBU SAID
13th March 2013
Pia Mkuu wa Usalama wa Taifa, Hoseah
Kwa msingi huo, wamekubaliana kuunda kamati ya watu 16 kwa ajili ya kukutana na wakuu wa vyombo vya usalama kuzungumzia undani wa usalama wa waandishi wa habari na wanaharakati wengine, ambao wamekuwa wakishambuliwa, kuumizwa na hata kuuawa nchini.
Pia wameitaka serikali kuunda tume huru ya wapelelezi kuchunguza undani wa masuala hayo.
Makubaliano hayo ambayo ni moja ya matamko matano, yalipitishwa na wadau hao katika kikao chao kilichofanyika jijini Dar es Salaam jana, kujadili hali ya kuzorota kwa mazingira ya usalama ya waandishi wa habari na wanaharakati wengine nchini.
Wadau hao waliongozwa katika kikao hicho na Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (Moat), Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika-Tawi la Tanzania (Misa Tan), Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Baraza la Habari Tanzania (MCT) na TEF.
Matamko hayo yalisomwa na wakurugenzi wa kampuni, taasisi na wahariri watendaji wa vyombo vya habari tofauti, ambao kila mmoja alisoma azimio moja na kumpisha mwenzake kusoma azimio lingine, katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.
Akisoma tamko la tano la kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa Gazeti la MwanaHalisi, Saed Kubenea, alisema wakuu wa vyombo vya usalama, ambao wadau wamekubaliana kukutana nao kwa ajili ya mazungumzo hayo, ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi.
Wengine ni Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, Inspekta Jenerali (IGP) Said Mwema; Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Othman Rashid, na Naibu wake, Jack Zoka; na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), Dk. Edward Hoseah.
Akisoma tamko la kwanza, mwakilishi wa Kampuni ya Business Times Limited, Adam Mbughuni, alisema wadau wa vyombo vya habari wanaamini kuwa kutekwa na kuteswa kwa Kibanda, ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006), kumetokana na msimamo imara wa kalamu yake.
“Kwamba shambulio lililofanywa dhidi ya Kibanda halikutokana na kitu kingine chochote, zaidi ya kazi yake ya uandishi wa habari,” alisema Mbughuni.
Alisema kutokana na hali hiyo, wadau hao wamelichukulia suala hilo kuwa ni shambulizi dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari nchini na kuwajengea hofu wahariri, waandishi na wanaharakati wote ili wasitekeleze wajibu wao kwa umma.
Akisoma tamko la pili, Mkurugenzi wa Misa Tan, Tumaini Mwailenge, alisema wadau wa vyombo vya habari wanaona tukio hilo ni mfululizo wa mashambulizi ya namna hiyo.
“Kwamba, katika mazingira hayo wamejiona na kutambua kuwa hakuna aliye salama. Ilianza kwa waandishi wa habari wa gazeti la MwanaHalisi, Saed Kubenea na Ndimara Tegambwage, kutekwa kwa Dk. Steven Ulimboka, kuuawa kwa mwandishi wa kituo cha Channel Ten, Daudi Mwangosi na sasa mashambulizi dhidi ya Kibanda,” alisema Mwailenge na kuongeza:
“Haya ni baadhi tu ya matukio yanaonyesha hali kuzidi kuzorota kwa mazingira ya utendaji kazi wa wanahabari na wanaharakati.”
Akisoma tamko la tatu, Mhariri Mtendaji wa Gazeti la NIPASHE, Jesse Kwayu, alisema wadau wa vyombo vya habari wamesikitishwa na hatua ya baadhi ya maofisa na watumishi wa vyombo vya usalama, kutumiwa kutekeleza vitendo vya uhalifu ambavyo vinatishia usalama wa waandishi wa habari na wananchi kwa jumla. Alitoa mfano, akisema usumbufu alioupata mwandishi wa habari, Eric Kabendera, na familia yake, ambaye wazazi wake walihojiwa na waliojiita watumishi wa Idara ya Uhamiaji, ulifanywa kwa shinikizo na watu wanaotumia watumishi wa umma kutekeleza matakwa yao ya kuleta hali ya kuzorota kwa usalama wa waandishi wa habari.
Akisoma tamko la nne, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006), Hussein Bashe, alisema wanaitaka serikali kuunda tume huru ya wapelelezi kuchunguza undani wa masuala hayo kwa kuwa kasi ya uchunguzi wa vyombo vya usalama nchini hairidhishi na pia baadhi ya watendaji ndani ya vyombo hivyo wanahusishwa na kadhia hizo.
Awali, Mwenyekiti wa Moat, ambaye aliongoza kikao hicho jana, Reginald Mengi, aliwataja wajumbe wanaounda kamati hiyo ya watu 16 kuwa ni pamoja na Bashe, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mwananchi Limited, Tido Mhando; Mbughuni, Abdallah Mrisho, na Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Freemedia, Ansbert Ngurumo.
Wengine ni Kwayu, Mikidadi Mahmoud, Japhet Sanga (TMF), Pili Mtambalike (MCT), Godfrida Jora (Tamwa), Mwailenge, Deodatus Balile (Jamhuri), Neville Meena (TEF), Samson Kamalamo (Changamoto), Henry Muhanika (Moat) na Mengi (Moat).
“Ni matumaini yetu kwamba, tutakubaliwa na hao wahusika tukutane nao haraka iwezekanavyo,” alisema Mengi, ambaye pia ni Mwenyekiti Mtendaji wa IPP Limited.
Akijibu maswali mbalimbali ya waandishi wa habari, Mengi alisema amepata ushahidi kwamba, kuna watumishi katika vyombo mbalimbali vya serikali, ambao wametumiwa kufanya uhalifu wa aina fulani kwa shinikizo la fedha.
Alitoa mfano wa yaliyomkuta mwandishi Kabendera, ambaye yeye na familia yake waliona kuwa iliyowasumbua ni serikali.
Hata hivyo, Mengi alisema kinyume cha Kabendera na familia yake walivyoona, wanachoamini na kukifahamu wadau wa vyombo vya habari ni kwamba, watumishi wa serikali waliokwenda kwa mwanahabari huyo walitoka Idara ya Uhamiaji, lakini fedha iliyotumika kufanikisha kazi hiyo, haikutoka kwenye mkondo wa fedha za wizara, bali zilitoka nje ya mkondo wa fedha za serikali.
“Kwa hiyo, kuna mtu aliyefadhili shughuli hiyo. Nina hakika kwa manufaa yake. Sasa hatujui ni kwanini. Lakini aliyefadhili anajulikana na aliyetumiwa kuchunguza wanapoishi wazazi wake Kabendera kwa bahati nzuri pia tunamfahamu, na kwa bahati mbaya alikuwa mwandishi wa habari. Sasa haya ni matumizi mabaya ya fedha,” alisema Mengi.
Alisema wana imani kwamba, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inamfahamu mtu huyo na pia wana imani kwamba, wizara hiyo inawafahamu kwa kina maofisa wa Uhamiaji waliotumiwa kwenda wilayani Bukoba, mkoani Kagera, ili kumtesa baba yake na Kabendera.
“Lakini kwa kuangalia kwa haraka haraka utasema ni serikali, lakini ni watumishi wa serikali walitumiwa na mtu, ambaye ametoa fedha zake. Na siyo ajabu hizo fedha ametuibia katika hali katika mambo ya ufisadi. Kwa hiyo, anatuibia, halafu fedha hizo hizo anazitumia kutuchapa. Hakuna tofauti na kibaka anakuibia simu yako ya mkononi halafu akakukimbiza. Mwizi ni yeye, lakini anakukimbiza wewe,” alisema Mengi.
Alisema kwa kuwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wanamfahamu mtu aliyetoa fedha hizo, wanatakiwa kumtaja na kwamba, wasipomtaja basi watamtaja wadau wa vyombo vya habari licha ya kwamba, wasingependa kuiumbua wizara hiyo.
Mengi alisema iwapo wizara hiyo itashindwa kumtaja mtu huyo itakuwa inamaanisha kwamba inamthamini mtu mmoja kuliko nchi yote ya Tanzania.
“Tunaitwa wauaji kumbe ni mtu mmoja anasababisha jambo Fulani, ambalo linachafua nchi yetu. Sasa Wizara ya Mambo ya Ndani iamue, muhimu ni huyo mtu mmoja au nchi yake. Kama wanaamua ni nchi yake, basi wachukue hatua za kisheria kumtaja ni fulani tumjue,” alisema Mengi.
Aliwaomba Watanzania kutoishi kwenye woga kutokana na matukio hayo, akisema kuwa mlinzi mkuu ni Mwenyezi Mungu, hivyo akawataka waombe na kusali. Naye Bashe alisema wiki tatu kabla ya tukio lililomkuta Kibanda, walitoka ofisini saa tano usiku, ambako nje ya ofisi kulikuwa kumeegeshwa gari dogo aina Golf ya Polisi namba PT 180 kwa muda mrefu.
Alisema walipotoka, waliofuatana na Kibanda kwa kuwa wote wanaishi Mbezi.
Bashe alisema gari hilo la Polisi lilikuwa limeegeshwa, huku likielekea Shekilango, lakini liligeuza na kuanza kuwafuata nyuma hadi eneo la Sinza Makaburini na kuzuia gari lake.
Alisema Kibanda akaegesha upande wa kulia na yeye (Bashe) akaegesha upande kushoto na gari lile la Polisi likasimama nyuma ya gari la Bashe, lakini askari waliokuwamo hawakushuka. “Akashuka askari mmoja. Nikawasha taa za gari ndani kwa sababu sikuwa peke yangu nilikuwa na mwenzangu. Nikamuuliza mnataka nini, akasema tunaitilia shaka gari yako, Kibanda akaniambia usishuke usifanye nini, kunaweza kukatokea missing of identity, hatujui hao watu wanataka nini.”
“nikawaambia kwamba nyinyi tumewaona nje ya ofisi yetu, mmetufuata, mnachotaka ni kitu gani? Lile tukio tuliliripoti. Na mimi personal niliongea na Waziri wa Mambo ya Ndani kumueleza lile tukio akasema Hussein nimesikia nalifanyia kazi.”
Alisema mbali ya hilo, wapo wanasiasa wameshatangaza hadharani kwamba, wana maadui kwenye nchi hii na wana maadui wanahabari, lakini taasisi hizi hazijawahi kuwaita wanasiasa hao na kuwauliza hao maadui zenu kwenye vyombo vya habari ni kina nani?
Hivyo, akasema hapa nchini, baadhi ya watu wameanza kuwagawa watu kwenye madaraja kwamba, kuna mtu tu anaweza kuamua kufanya lolote na mwingine kufanyiwa na kuachwa.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment