NA MWANDISHI WETU
5th October 2013
.jpeg)
Katika mazungumzo hayo Dk Shein ameishukuru Serikali ya Uingereza kwa misaada yake kwa Zanzibar na kueleza matumaini yake kuendeleza ushirikiano zaidi katika kusaidia Zanzibar kutimiza ndoto yake ya kuwa taifa lenye uchumi wa kipato cha kati ifikapo mwaka 2020.
Alimueleza Mathews kuwa uwekezaji ni sehemu muhimu ya kupanua ushirikiano kati ya Uingereza na Zanzibar na kutoa wito kwa wawekezaji wa nchi hiyo kuzitumia fursa za uwekezaji zilizopo nchini hasa katika sekta ya Utalii na Uvuvi wa Bahari Kuu.
Alisema pamoja na kuwepo fursa katika sekta nyingi za uchumi, sekta ya uvuvi wa bahari kuu ni eneo ambalo likipata uwekezaji muafaka lina kila uwezo wa kubadili maisha ya wananchi wengi wa Zanzibar.
Dk. Shein alieleza kuwa eneo hilo linagusa maisha ya wananchi wengi na anaamini kuwa linaweza kusaidia kufikia malengo ya Serikali sio tu ya kuinua kiwango cha ukuaji wa uchumi wa nchi bali hata kuinua kiwango cha maisha ya wananchi wa Zanzibar kwa kutoa ajira nyingi.
Kwa upande wake, Mathews alisema Uingereza itaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutekeleza mipango yake ya maendeleo ili kunyanyua kiwango cha maisha cha wananchi wake.
Alisema Serikali ya nchi yake inaiona Zanzibar kuwa mshiriki muhimu katika mpango wa ushirikiano kati ya Uingereza na Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kusaidia kufikia malengo ya maendeleo.
“Zanzibar ni mshiriki muhimu katika Mpango wetu wa Ushirikiano kati ya Uingereza na Afrika Mashariki ili hatimae iweze kufikia lengo lake la kuingia katika nchi zenye uchumi wa kipato cha kati,” alisema Mathews.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment