Ahmed Rajab Toleo la 329 11 Dec 2013
JUMAPILI ya tarehe 11 Februari, 1990 nilishinda mchana kutwa kwenye studio za televisheni za Sky News nilikoitwa kwenda kuzungumzia siasa za Afrika Kusini na kukaa chonjo kusubiri dakika Nelson Mandela atapofunguliwa na kutoka gerezani.
JUMAPILI ya tarehe 11 Februari, 1990 nilishinda mchana kutwa kwenye studio za televisheni za Sky News nilikoitwa kwenda kuzungumzia siasa za Afrika Kusini na kukaa chonjo kusubiri dakika Nelson Mandela atapofunguliwa na kutoka gerezani.
Siku hiyo nilikuwa na mgeni, waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Comoro, Salim Hadji Himidi, aliyejitolea kufuatana nami. Wakati huo hakujuwa kwamba miaka michache tu baadaye atakuwa akikutana naye Mandela mara kwa mara zaidi ya zangu mbili alipoupata uwaziri wa mambo ya nje wa nchi yake.
Nilikaa kwa muda mrefu katika studio za Sky News siku hiyo kila baada ya muda nikijibu maswali na kueleza mambo kuhusu Afrika Kusini na Mandela.
Lakini sikujali hata chembe kwani ilikuwa ni siku ya kihistoria, ya kiongozi wa kihistoria, nikishuhudia tukio la kihistoria na nikisaidia kulichambua.
Saa chache baadaye waliingia studio marafiki zangu wawili wazalendo wa Afrika Kusini wenye asili ya Kihindi, Paul Joseph na mkewe Adelaide. Tulijuwana kwa miaka mingi na tuliingiliana sana pamoja na Daso Joseph, nduguye Paul.
Wote walikuwa wakiishi uhamishoni London kwa sababu ya misimamo yao ya kupinga ubaguzi wa rangi wa Afrika Kusini. Huko kwako Paul Joseph alikuwa Mkomunisti nambari 642. Walipokuwa kwao Afrika Kusini, Paul na Adelaide walikuwa marafiki wakubwa wa Nelson Mandela.
Paul alikuwa mmoja wa washtakiwa katika kesi ya uhaini ya miaka ya 1950. Alipokamatwa aliteswa sana. Kwa mfano, akining’inizwa juu chini nje ya dirisha la chumba cha ghorofa ya juu kabisa.
Baada ya kukimbia Afrika Kusini na kuja kuishi uhamishoni walikuwa wakiandikiana barua na wenzao waliokuwa wamefungwa kwenye Kisiwa cha Robben kina Mac Maharaj, Billy Nair, Laloo Chiba, Raymond Mhlaba, Nelson Mandela na Mike Mkwayi.
Walialikwa kwenye studio za Sky News waje waueleze ulimwengu kuhusu Mandela waliokuwa wakimjua.
Walieleza mengi. Ya jinsi Mandela alivyokuwa akikutana na wenzake kwa siri nyumbani kwao kina Paul na Adelaide. Jinsi Mandela alivyokuwa akipenda kula chakula kizuri. Jinsi Mandela alivyokuwa akiandikiana nao alipokuwa mfungwa kwenye kisiwa cha Robben na jinsi alivyokuwa hasahau siku za kuzaliwa za watoto wao na mambo kama hayo. Mambo ambayo mtu mkubwa kama Mandela utadhani alikuwa hayatii maanani.
Lakini Mandela alikuwa ni kiumbe aina yake. Alizaliwa binadamu, baadaye akawa wazo na sasa, baada ya kufariki, amegeuka kuwa ndoto.
Mandela ndoto ni zile ndoto za Mandela, zile ahadi zisizotimizwa, ni yale matumaini waliokuwa nayo walala hoi wa Afrika Kusini, matumaini yaliogeuka kiu kisichoweza kukatwa na watawala wa leo wa Afrika Kusini.
Mamilioni ya walalahoi hao hawana umeme vibandani mwao — kwani humo ndimo wanamoishi, kwenye vibanda vya mabati — wala hawana maji safi, siya kupikia, siya kuogea. Kweli wana kura, na wanamshukuru Mandela kwa kuipata haki hiyo, lakini wamegundua mapema kwamba hawawezi kuila kura, kwamba hata kama wakiweza kuila haitojaza tumbo.
Na kuna jengine ambalo wameligundua. Nalo ni kwamba ingawa ukaburu asilia umeondoka pamoja na utawala wake hivi sasa kuna ukaburu wa aina nyingine, ukaburu mamboleo.
Kuna alama nyingi za ukaburu huu mpya. Nitazitaja mbili tu. Ya kwanza ni kuibuka kwa kundi dogo sana la Waafrika wenye kuhodhi madaraka ya kisiasa. Hawa wameungana na watawala wa kale wa Kizungu pamoja na Wazungu wenye kuzishikilia hadi leo nyenzo za kiuchumi.
Waafrika waliomo kwenye kundi hilo wanaishi maisha yanayopindukia yale ya watawala wa hadithi za Elfu Leila u Leila. Ni maisha ya anasa zinazokirihisha, anasa za kufru. Ndio maana Waafrika walio maskini, na wengi nchini humo, wana ghadhabu. Na kila siku wakiamka asubuhi wanazidi kuwa na ghadhabu. Na wana ghadhabu kwa sababu maisha yao yalivyo sasa ni sawa na yalivyokuwa katika siku za ukaburu asilia.
Si ajabu kuona kwamba wanasiasa wa chama kinachotawala cha African National Congress (ANC) wamekuwa wakiuana kama nzi, kila mmoja akiwa anautapia utajiri. Inahuzunisha kwamba hawa ni wanasiasa wa chama cha Mandela.
Alama nyingine ya ukaburu mamboleo ni ubaguzi mpya uliopo, ubaguzi wanaofanyiwa Waafrika walio wageni Afrika Kusini. Wenye kuufanya ubaguzi huo ni Waafrika wa Afrika Kusini. Wao walibaguliwa na makaburu na sasa wao wanajifanya makaburu kuwabagua Waafrika wenzao walio wageni.
Ubaguzi wao ni muovu kwa sababu wanaua; wanawaua Wasomali, Wamsumbiji na wafanyakazi wengine wa Kiafrika kutoka nchi nyingine. Wabaguzi hawa wapya wa Afrika Kusini hawana ukarimu wala uungwana wa Mandela.
Wala hawamwezi. Si wao hao wabaguzi wala wale waliozitumia siasa za ANC kujitajirisha. Ni wazi Mandela alikuwa na siri fulani. Na ndio maana akaweza, japokuwa si kwa urahisi kuwapatanisha Wazungu na Waafrika wa nchi yake na kuwafanya wazungu hao wajihisi kwamba wao pia ni Waafrika, wa kabila la Waafrika wenye ngozi nyeupe.
Lakini ni siri gani hiyo iliyomfanya afanikiwe kuleta mapatano baina ya Wazungu na Waafrika wa Afrika Kusini? Nadhani siri yake ni kwamba alikuwa akijiamini. Hakujishusha hadhi na kujifanya mdogo mbele ya Wazungu.
Mandela alikuwa pia mwadilifu na aliutumia uadilifu kama kiboko cha kuwatandika wapinzani wake.
Kwa upande mwingine, Mandela alikuwa na kibri — tena kibri cha hali ya juu — lakini ilikuwa vigumu kukiona kwa sababu alikuwa akikivisha joho kubwa la unyenyekevu. Alikuwa akikionyesha kibri hicho pale alipokuwa ana hakika kwamba msimamo wake kuhusu suala fulani ni sahihi, na si msimamo uliosahihi tu lakini pale alipokuwa ana hakika kwamba msimamo huo ulikuwa umesimama juu ya msingi wa uadilifu.
Mandela alikuwa na uadilifu na unyenyekevu wa kukiri mara kadha wa kadha, kwenye hotuba na maandishi yake, kwamba alikuwa na dosari zake. Hakuwa amekamilika wala hakuwa Mtakatifu kama maadui zake wa zamani wanavyomfanya sasa akiwa amefariki.
Inastaajabisha kuwaona maadui wa Mandela na wa ANC wakiwa safu ya mbele miongoni mwa wanaoomboleza kifo cha Mandela. Ghafla amekuwa Mwema kwao na kwa ulimwengu na wamekuwa wakimsifu mpaka mbinguni.
Mmoja wa wanafiki wakubwa ni waziri mkuu wa Israel, Benjamin ‘Bibi’ Netanyahu. Amemuelezea Mandela kuwa ‘mpiganiaji uhuru, aliyekanya matumizi ya nguvu’. Si kweli. Mandela hakuwa Gandhi, na alikuwa tayari nguvu zitumiwe kufikia lengo la ukombozi. Lakini alisema kwamba alishauriwa na Rais Ahmed Ben Bella wa Algeria alipoizuru nchi hiyo mwaka 1962 aifuate njia ya mashauriano kwani ile ya mapigano itakuwa ngumu. Tena Netanyahu anasahau kwamba Israel ilijitolea wakati mmoja kuipa serikali ya makaburu moja ya silaha zake za kinyuklia.
Marekani nayo kwa muda mrefu imekuwa ikikiona chama cha ANC kuwa ni chama cha kigaidi na kwamba wafuasi wake ni Wakomunisti. Serikali ya nchi hiyo ililiweka jina la Mandela kwenye orodha ya magaidi na ililiondosha kwenye orodha hiyo mwaka 2008.
Hata wakina Tony Blair na David Cameroon, Mawaziri Wakuu wa zamani na wa sasa wa Uingereza, nao pia wamejitokeza uwanjani kumtukuza Mandela.
Wote hao wanafanya hivyo kwa akili zao. Wanajua kwamba udhaifu mmoja wa Mandela ni ule uliomfanya akubali mapatano ya kisiasa yaliouacha uchumi wa Afrika Kusini sio tu mikononi mwa Wazungu wachache lakini pia katika mfumo ambao utaendelea kuyanufaisha madola ya Magharibi. Kama Mandela mtu alikuwa na udhaifu huo, ile ndoto yake itaendelea kuwahamasisha vijana wa Afrika kwa muda mrefu ujao na huenda ikasaidia kuibuka kwa Mandela wa karne ya 21 atayeitimiza ndoto ya Mandela wa karne ya 20.
Chanzo: Raia Mwema
No comments :
Post a Comment