AirFreight

Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, August 2, 2015

CCM vituko vitupu


Uchaguzi wa Kura za maoni kuwatafuta wagombea  ubunge na udiwani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), jana uliingia dosari baada ya majimbo kadhaa kuahirisha hadi leo kutokana na baadhi ya karatasi za kura kukamatwa zikiwa zimewekwa alama ya kura kabla ya uchaguzi.


Katika majimbo mawili ya Tarime, mkoani  Mara, uchaguzi huo umehairishwa  baada  ya kukamatwa  kwa  karatasi  maalum  za  kupigiwa  kura  zikiwa  tayari  zimeandikwa  majina ya wagombea wawili.

Akizungumza  na  NIPASHE, muda  mfupi   baada  ya karatasi hizo  kukamatwa, Mwenyekiti wa CCM wa wilaya ya Tarime,  Rashid  Bugomba, alisema zaidi ya karatasi 20,000  zimekamatwa zikiwa na majina ya Gaudencia Kabaka (Tarime mjini) na  Nyambari  Nyangwine  (Tarime  vijijini).

Alisema kuwa  karatasi hizo zimepigwa kura  saa 8 usiku na baada ya vituo kufunguliwa ilipobainika kuwa zimewekewa alama za kura. Karatasi hizo, chache zilikuwa na majina ya John Gimunta na Philip Nyirabu.

“Kweli  karatasi  hizo tumezikamata zikiwa tayari zimepigwa na nyingi za mheshimiwa Kabaka na Nyangwine, hivyo  tumechukua hatua  ya kufuta  uchaguzi  hadi  kesho (leo)  Jumapili,” alisema Bugomba.

Alisema uchaguzi huo utafanyika baada ya  karatasi nyingine kuchapishwa upya.

Mmoja wa wagombea ambao  picha zao  zinaonekana katika karatasi hizo,  Kabaka,  alipotafutwa kwa njia ya simu hakupatikana kuzungumzia  sakata hilo.

Nyangwine, akizungumza kwa njia ya simu alisema kitendo hicho kimefanywa na baadhi ya watendaji wa kata kwa kushirikiana na baadhi ya wagombea ambao anadai walibaini tayari walishindwa.

Huko Same Mashariki na Same Magharibi, mkoani Kilimanjaro, mchakato umeahirishwa kwa siku moja kutokana na idadi kubwa ya wapiga kura wa CCM kutaka zoezi hili lisogezwe mbele ili kupisha ibada ya siku ya Sabato.

Katibu wa CCM Wilayani hapa, Mussa Matoroka aliambia NIPASHE kuwa Katibu Mkuu wa CCM  Taifa, Abdulrahman Kinana, alitoa kibali maalum jana cha kuruhusu kuahirishwa kwa zoezi hilo, kwa kuwa asilimia 80 ya wapiga kura wa majimbo hayo ni Wasabato.

HANANG: Baadhi ya wanachama wa CCM, Wilaya ya Hanang, wameshindwa kutumia haki ya kuwachagua wagombea udiwani na ubunge baada ya kadi zao kutoorodheshwa kwenye Daftari la Wanachama wa CCM katika matawi husika.

Nafasi ya ubunge katika Jimbo la Hanang, inagombewa na Dk. Mary Nagu ambaye anatetea tena kiti hicho, huku akikabwa koo na Wakili Duncan Mayomba, Dk. Eliamani Sedoyeka na Peter Nyalandu.

Katibu wa CCM Wilaya ya Hanang, Kajoro Vyohoroka, alithibitisha kutokea kwa changamoto hiyo, lakini alieleza kuwa walioshindwa kufanya hivyo hawakuwa na kadi halali.

Alisema baadhi walikuwa wamepata kadi kutoka matawi mengine ndani ya wilaya hiyo au nje lakini kwa vile wanaishi katika eneo jipya hawakuwa wameorodheshwa kwenye daftari hilo.

“Kwa hiyo tulishindwa kuwatambua iwapo ni wanachama halali wa tawi husika…wilaya yangu haina kadi feki na hilo ninaweza kuthibitisha,” alisema.

Alisema kwa mfano, katika Kata ya Gehandu kulikuwa na kadi halali 94 ambazo alizitoa kwa katibu kata ili awape wanachama wapya, lakini katibu kata alizifungia kabatini na kusafiri siku ya pili yake na aliporudi alichelewa kuwapatia hadi daftari lilipofungwa.

Alisema kadi hizo hazikugawiwa kwa wahusika hadi ulipofanyika uchaguzi jana, na zilihifadhiwa kwa Kamanda wa Polisi wa Wilaya na utaratibu wa kuwapatia wahusika utafanywa hapo baadaye.

Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE katika vituo kadhaa vya kupigia kura, ulionyesha kuwepo kwa idadi ndogo ya wanachama waliojitokeza kupiga kura.

Hata hivyo, wanawake ndio wanaoelezwa kujitokeza kwa wingi kwenda kupiga kura.

Msimamizi wa Kata ya Ganana, Festo Manda, alisema vituo vyote vinne katika kata hiyo vilifunguliwa kuanzia saa 8:00 asubuhi na kufungwa saa 10:00 jioni.

“Tunafanya uchaguzi kwa amani kabisa, hakuna vurugu yo yote iliyotokea tangu asubuhi hadi wakati huu tunapokaribia kufunga vituo,” alisema.

Mpiga kura aliyekutwa katika kituo cha tawi la Sokoni, alisema uchaguzi huo ulifanyika vizuri na kwa amani.

KIBAMBA: Katika Jimbo la Kibamba, uchaguzi  umeahirishwa hadi leo baada ya msimamizi wa uchaguzi kukamatwa na Takukuru, akipokea rushwa kutoka kwa mjumbe. Waliokamatwa ni Edna Kalela, Katibu wa CCM kata ya Kibamba na Babu Kimanyo, Katibu Itikadi CCM, Kata ya Kibamba.

ZANZIBAR: Uchaguzi wa kura maoni za kuwasaka wagombea wa nafasi ya uwakilishi, ubunge na udiwani umeshindwa kufanyika kwa baadhi ya maeneo kutokana mapungufu.

Akizungumza na NIPASHE Naibu Katibu Mkuu wa CCM Vuai Ali Vuai alisema katika tawi la CCM Mahonda zoezi la upigaji kura za  maoni umeahirishwa hadi leo kutokana na kuwepo kwa sitonfahamu.

“Taarifa nilizozipata hivi punde kuwa tawi la CCM Mahonda zoezi limestopishwa hadi kesho (leo)kutokana na kuwepo kwa vurugu ila bado sijajua vurugu hizo zimesababishwa na nini,” alisema Vuai.

Alisema baadhi ya maeneo ya upigaji kura hizo za maoni zoezi limechelewa kuanza kutokana na kuchelewa kufika  kwa baadhi ya vifaa ikiwemo karatasi za kupigia kura.

DODOMA: Wameshindwa kupiga kura kufuatia kuibuka changamoto mbalimbali ikiwamo majaribio ya wizi wa kura.

NIPASHE lilitembelea baadhi ya vituo katika manispaa ya Dodoma na kushuhudia changamoto hizo ikiwa ni pamoja na baadhi ya wapigakura kukosa uaminifu, dosari katika karatasi za kupigia kura, vifaa kuchelewa kufikishwa kwenye vituo vya kupigia kura na watu kukosa majina yao kwenye daftari la wapiga kura huku katika maeneo mengine majina yakiitwa na  wapigakura kukosekana.

Katika kituo cha Chang’ombe juu, uchaguzi ulisimamishwa baada ya mwanamke aliyefahamika kwa jina moja la Nasra, kukamatwa akiwa na kiasi kikubwa cha karatasi za kura, akiziweka kwenye boksi la kura la kuchagua diwani wa kata hiyo, kinyume na taratibu.

Kaimu Katibu wa CCM wa kata hiyo, Abas Salim, alisema Nasra aliwasilishwa kwenye kituo cha polisi kwa ajili ya kuhojiwa. Mpaka Saa 8 mchana zoezi lilikuwa limesitishwa  kwa maelezo kuwa mawasiliano
yalikuwa yakifanyika ili kupata namna ya kukabiliana na changamoto hizo.

MBEYA: Mchakato umeingia dosari katika baadhi ya maeneo mkoani Mbeya na kusababisha zoezi hilo kuchelewa kuanza, huku baadhi ya makada wakitimua mbio baada ya kukutwa na karatasi bandia za kupigia kura.

Dosari ya kwanza imejitokeza wilayani Ileje ambako baadhi ya wagombea walizikataa karatasi za kupigia kura zilizoandaliwa na Chama hicho kwa madai kuwa zikitumika ni rahisi kuibiwa kura na hivyo wakashinikiza kutengenezwa kwa karatasi mpya ambazo wanaamini kuwa haziwezi kusababisha waibiwe kura.

Katibu wa CCM Wilaya ya Ileje, Amida Mbogo aliliambia NIPASHE kuwa shinikizo hilo lilitolewa na wagombea ubunge wawili kati ya sita ambao walidai karatasi za kupigia kura zilizoandaliwa na chama hicho zilisababisha waibiwe kura zao katika uchaguzi kama huo uliopita mwaka 2010.

Aliwataja wagombea hao kuwa ni Godfrey Msongwe na Laison Mkondya ambao walitaka karatasi za kupigia kura mwaka huu ziwe za rangi sambamba na kusainiwa na Katibu wa CCM wilaya na mmoja wa wagombea huku pia wakitaka zigongwe muhuri wa chama pamoja na muhuri wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru).

ARUSHA: Viongozi CCM, wilayani Arusha wanadaiwa kushikiliwa na  Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kukutwa na makaratasi bandia za kupigia kura ya maoni ya Diwani wa Kata ya Mjini Kati jijini hapa.

Wanachama hao wanaodaiwa kubainika kuwa walikuwa na makaratasi hayo ni Katibu wa CCM Kata ya Kati Ally Meku na Mwenyekiti wa Tawi la Bondeni Yakubu Mkindi.

Taarifa zilizoatikana jana jijini hapa wakati zoezi la upigaji kura likiwa linaendelea ilidaiwa kuwa viongozi hao wanaodaiwa kuwa kutengeneza mpango wa kupitisha karatasi hizo ili kumuongezea kura mgombea wa udiwani wanayemuunga mkono.

Chanzo cha kuamini kutoka ndai ya CCM kilidai kwamba wanachama hao walikuwa na mpango wa kuhakikisha mgombea wao anashinda kura za maoni kinyume na utaratibu unaokubalika rasmi wa kupiga kura na kupelekwa kwa majina mbele ya kamati ya siasa ya wilaya.

Katika Kata hiyo wanachama wanaowania nafasi ya Udiwani ni Mwenyeki wa Mtaa wa Bondeni, Simba Seif Salumu na Diwani aliyemaliza muda wake Abdulrasul Tojo ambao wamekuwa na ushindani mkali kutokana na mazingira ya Kata ya Kati kuwa na nyumba zinazofahamika pamoja na wakazi wake.

Alipotafutwa kwa njia ya simu kuzungumzia suala hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Lebaratus Sabas hakuweza kupatikana kutokana na simu yake kutopatikana.

Wanachama wa CCM wanaowania nafasi ya kupeperusha bendera ni pamoja na Mustafa Panju, Justine Nyari na Thomas Munisi, Swalehe Kiluvia, Edmund Ngemela, Mosses Mwizarubi, Said Migire, Reuben Mweteni, Victor Njau, Philimon Mollel, Mohamud Omari na Emanuel ole Njoro.


CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments :

Post a Comment