dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, October 24, 2015

Lowassa: Mwisho wa CCM kesho.

Mgombea urais wa Chadema anayeungwa mkono na Ukawa, Edward Lowassa, akihutubia wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa Temu, Kata ya Ruaha wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro jana. PICHA: MPIGAPICHA WETU
Mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, amewahimiza Watanzania kumpigia kura nyingi katika Uchaguzi Mkuu wa kesho, ili kuleta mabadiliko yanayohitimisha utawala wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
 
Lowassa aliyasema hayo katika hotuba yake kupitia vyombo mbalimbali vya habari na Nipashe kupata nakala yake.
 
“Watanzania wanataka mabadiliko ya kweli na ya uhakika, kesho tuhakikishe tunaing’oa CCM madarakani na kuanza safari mpya ya kuleta mabadiliko,”aliongeza.
 
KUIPUUZA CCM
Lowassa amewataka Watanzania kupuuza madai yanayotolewa na CCM kuwa wapinzani wataleta fujo wakati wa kupiga kura.
 
“Madai yanayotolewa na CCM kuwa Ukawa wataleta fujo wakati wa kupiga kura ni maneno ya kipuuzi,”alisisitiza.Aliwataka wafuasi wa upinzani kuwa wastaarabu, waheshimu sheria, wakusanyike na kupiga kura kwa amani na utulivu.
 
Alizipongeza kampeni za Ukawa kuwa zimedhihirisha kuwa wapinzani hawavunji na hawatajavunja sheria.
 
“Hatuna sababu ya fujo. Dhamira yetu ni kushinda na kuing’oa CCM madarakani, dhana na fikra potofu za kutuogopesha eti Watanzania wakichagua upinzani nchi itaingia kwenye machafuko, wapuuzwe,” alisema .
 
MIFANO YA MABADILIKO 
Alitaja baadhi ya nchi kama,Zambia chama tawala kilipoondolewa madarakani hapakutokea fujo.
 
“Mzee Kenneth Kaunda aliyekuwa anaongoza chama tawala wakati huo alikwenda kufurahia maisha yake wakati Wazambia wakiendelea mbele,” alisema.
 
Kadhalika alisema nchini Malawi chama cha Congress Party pia kiling’olewa na nchi hiyo imeendelea kuwa na amani.Lowassa alitoa mfano wan chi jirani ya Kenya kuwa mwaka 2002, Kanu iliondolewa madarakani na hakukuwa na tatizo.
 
“Ukweli ni kwamba matatizo yaliyojitokeza Kenya miaka mitano baadaye, hayakutokana na kuondolewa kwa Kanu. Yalikuwa ni madai yaliyotokana na udanganyifu katika matokeo ya Uchaguzi Mkuu,”alisema.
 
Aliwataka Watanzania kujifunza kuwa udanganyifu uliwaletea Wakenya matatizo hivyo uepukwe.
 
UPOTOSHAJI KUHUSU LIBYA
Lowassa alieleza kusikitishwa na kauli za kuwaogopesha Watanzania kwa kuilinganisha nchi hii na Libya.
 
“Hawa wapuuzwe na kuonewe huruma kwa kuwa wamesahau misingi na uimara wa nguzo za taifa letu… hawajui kitu kinachowafanya Libya wanapigana,” alisema.
 
“Machafuko yao hayakutokana na uchaguzi, yalisababishwa na watawala kung’ang’ania madaraka na kugawana rasilimali za nchi na familia zao,”alisema.
 
Lowassa alisisitiza kuwa kama ilivyotokea Zambia, Malawi na Kenya, Watanzania wamedhamiria kuleta mabadiliko kidemokrasia na kuiondoa CCM madarakani kupitia sanduku la kura.
 
Alisema chama tawala kimechoka na kimebaki kuonyesha jeuri na kubeza lakini pia kimeishiwa nguvu ya hoja.
 
VIPAUMBELE
Lowassa ametangaza maeneo ya kipaumbele iwapo kitachaguliwa kuongoza serikali.
 
Ameainisha maeneo hayo kuwa ni Katiba Mpya, kuboresha huduma za jamii ikiwamo kuhudumia watoto na wahitaji na kuanzisha wizara mpya ya mafuta na gesi.
 
KATIBA MPYA
Lowassa anayeungwa mkono na Umoja wa Watetea Katiba ya Wananchi (Ukawa), aliahidi kuwa endapo atachaguliwa ataanza mchakato wa kuandaa Katiba Mpya.
 
Alisema katiba hiyo italeta ukombozi kwa kuwapa watu madaraka ya kikatiba kuhusu maisha yao na kujisikia kuwa na haki na uhuru kamili nchini.
 
Alisema CCM ilikwamisha ukombozi huo baada ya kuikataa rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph.
 
“Nikichaguliwa kuwa Rais, suala hili la Katiba Mpya yenye maslahi kwa mwananchi litapewa kipaumbele,” alisema.
 
Kadhalika maeneo mengi aliyoyataja ni mapinduzi ya kilimo na kuwapa wakulima na wafugaji bei bora za mazao.
 
WATANZANIA KUKOSA FURAHA
Alinukuu taarifa ya Umoja wa Mataifa ya mwaka huu kuhusu hali ya furaha ya wananchi katika nchi mbalimbali, iliyobainisha kuwa kati ya mataifa 156 yaliyoshirikishwa katika utafiti, Tanzania ilikuwa ya 151 ikidhihirisha kuwa Watanzania hawana furaha.
 
“Serikali ya CCM imeshindwa kuwapa wananchi hali bora ya maisha na hivyo kuwanyima furaha,” alisema.
 
HUDUMA ZA JAMII
Lowassa alisema serikali inaheshimika kwa jinsi inavyowajali na kuwahudumia watoto, wazee, wagonjwa na wenye mahitaji maalum wakiwamo watu wenye ulemavu.
 
“Mwaka huu Tanzania inashika nafasi ya 91 kati ya nchi 96 zilizofanyiwa utafiti na taasisi ya kimataifa ya wazee (HelpAge) kuhusu hali ya wazee wenye umri zaidi ya miaka 60 na kubainika kuwa imeshindwa kutekeleza wajibu,”alisema.
 
Alifafanua kuwa wagonjwa hawapati dawa hospitalini na hata wanaojiweza lazima wakatibiwe nje ya nchi. Lowassa alisema huduma za walemavu ni finyu na kuendelea kwa mauaji ya albino ni jambo linaloendelea.
 
UONGOZI UNAOTHUBUTU
Kipaumbele kingine kilichotajwa na Lowassa ni kuleta mabadiliko ya uongozi na mfumo na kwamba wanataka uongozi wenye fikra mpya, utendaji wa kuaminika na uongozi wa uwajibikaji na shirikishi.
 
“Wanataka uongozi makini wenye ubunifu, upeo mpana na unaoongozwa na nidhamu hasa ile ya matumizi ya fedha za serikali,” alisema.
Katika taarifa hiyo Lowassa aliilamu  serikali ya CCM kwa kuiingiza nchi kwenye deni kubwa la historia.
 
“Deni hili ni karibu Sh trilioni 35 lililotokana na matumizi mabaya ya serikali. Ni kazi kubwa kulipa deni hili ndio maana Watanzania wanalazimika kuing’oa CCM na kuleta mabadiliko ya kiuchumi…” anasema na kuongeza;
 
“Mabadiliko yatakayowapunguzia kizazi hiki na kijacho mzigo wa madeni ambayo CCM inaendelea kuwalimbikizia kutokana na matumizi yasiyo na busara.” 
 
Alisema kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itakayoongozwa na Seif Sharif Hamad kama wakishinda katika Uchaguzi Mkuu wa kesho, wataunda uongozi wa kuthubutu na kutatua matatizo ya wananchi. Pia atawaunganisha Watanzania bila kujali madhehebu, rangi au makabila.
 
Lowassa aliwahakikishia Watanzani kuwa ataheshimu, kulinda na kutetea Katiba na kuwa mfano wa uadilifu kwa kupiga vita rushwa na ufisadi.
 
WIZARA YA MAFUTA NA GESI
Kadhalika aliahidi kuwapa Watanzania fursa za kushiriki uwekezaji katika sekta ya mafuta na gesi na kuahidi kuanzisha wizara maalum itakayosimamia rasilimali hizo.
 
VYANZO VYA AJIRA
Lowassa aliahidi kutengeneza vyanzo vipya vya ajira kwa kukuza sekta za kilimo, viwanda na utalii.
 
“Nitahakikisha tutaacha kuwa taifa ombaomba litaacha kuukubali na kuuvaa umaskini kama vile ni joho la fahari. Hakuna faraja katika umaskini, ” alionya.
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment