dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, October 24, 2015

Magufuli afunika Dar.

Mgombea urais wa CCM, Dk. John Pombe Magufuli akihutubia wananchi katika mkutano wa kampeni wa hitimisho kwa mkoa wa Dar es Salaam uliofanyika kwenye viwanja vya Jangwani jijini humo jana. PICHA: MPIGAPICHA WETU
Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amefunika jiji la Dar es Salaam akifanya mkutano wa mwisho jijini humo, kabla ya Uchaguzi Mkuu wa kesho.
 
Akizungumza katika mkutano huo, Dk. Magufuli alisema Rais Jakaya Kikwete aliteua baadhi ya wasaidizi ambao hawafai hivyo wakawa sababu ya kukwama kwa shughuli mbalimbali nchini.
 
Dk Magufuli akaibua vicheko kwa maelfu ya watu waliohudhuria aliposema anatamani  kuanza kazi ya urais hata jana, ili kuyamaliza mafisadi yaliyosalia serikalini kwani watanzania wamechoka na mateso. Mkutano huo wa mwisho kwa jijini humo ulifanyika kwenye viwanja vya Jangwani.
 
Miongoni mwa watu waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Rais Jakaya Kikwete, Jaji Joseph Warioba, Salim Ahmed Salim na Katibu Mkuu wa CCM, Abdurahman Kinana.
 
Dk Magufuli alisema alipoteuliwa kuwania urais watuhumiwa wa kashfa za ufisadi waliingiwa hofu kiasi kwamba wengine wakaanza kuondoka ndani ya CCM.Aliyasema hayo wakati akiwashambulia waliokuwa mawaziri wakuu ambao wamekuwa wakizunguka na kuisimanga serikali ya Rais Kikwete kwamba haijafanya jambo lolote la maendeleo ya nchi.
 
Dk. Magufuli alisema watu hao walikuwa washauri wakubwa wa Rais lakini wanashangaza kugeuka na kuanza kuirushia makombora kwamba hakuna lolote lililofanyika.
 
“Wanaposema hivyo wanamaanisha kwamba walikuwa wanamshauri Rais  mambo ya uongo, sasa kama hakuna kilichofanyika kwanini walikaa madarakani kwa muda mrefu, huo ni uongo na uzushi na washindee na walegee huko huko waliko,” alisema Dk. Magufuli na kuongeza.
 
“Lazima niseme ukweli na msema kweli mpenzi wa Mungu, Rais Kikwete aliweka watu wengine ambao hawafai  na ndio hao wanazunguka na kuisimanga serikali kwamba hakuna ilichofanya.” 
 
Alisema  sehemu zote alipopita kwa kampeni, wananchi walimjulisha kwamba anafaa kuwa Rais wa awamu ya tano, hivyo aliwataka kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi kupiga kura ya ndiyo ili ashinde kwa kishindo.
 
Dk. Magufuli aliahidi kuzijenga kwa lami barabara nyingi za jijini humo na kutatua kero ya maji kwa kuhakikisha mradi mkubwa wa kutoka Ruvu Juu na Ruvu Chini unakamilika kwa wakati.
 
Alisema mradi huo ambao ukikamilika utazalisha lita milioni 780 za maji kwa siku, umekwama  kutokana na mtu mmoja kuipeleka serikali mahakamani akipinga kubomolewa kwa nyumba yake ili kupisha ujenzi wa bomba kubwa.
 
Mgombea urais huyo alisema anaheshimu taratibu za mahakama, lakini angekuwa Waziri wa Maji angebomoa nyumba hiyo ili kupisha ujenzi wa bomba hilo kwa manufaa ya Watanzania walio wengi.
 
Aliwataka Watanzania kuwachagua wabunge watakaowajibika kwa kuwabana mawaziri kupeleka miradi kwenye majimbo yao badala ya wale wenye kawaida ya kususia vikao vya Bunge.
 
Dk. Magufuli alisema baadhi ya wabunge wamekuwa wakichukua posho na kutohudhuria vikao kwa kususa, huku mijadala mbalimbali yenye maslahi kwa wananchi ikijadiliwa.
 
Mke wa Rais Kikwete, Salma Kikwete aliwataka Watanzania kumchagua Dk Magufulim kwa maelezo kuwa ana sifa na uwezo wa kuiongoza nchi.
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment