Wapete pia Sakaya, Kubenea, Msigwa, Chenge, Mpina, Mbatia, Bashe, Sutta na Komu. Mrema, Ole Sendeka, Kapuya, Machali, Mkosamali wapigwa chini.
Wakati wabunge hao waliomaliza muda wao bunge lililopita wakiangukia pua, wabunge wengine machachari wamefanikiwa kutetea nafasi zao, huku sura mpya nazo zikichomoza baada ya kuwabwaga waliokuwa wakishikilia nafasi hizo kwenye majimbo yao.
WALIOBWANGWA
Sendeka ‘chali’ Simanjiro
Christopher Ole Sendeka mmoja wa wabunge vigogo wa CCM ameshindwa kutetea tena jimbo lake la Simanjiro, baada ya kuangushwa na mpinzani wake wa siku nyingi kada wa zamani wa CCM, James Ole Millya, ambaye amehamia Chadema.
Wakati Sendeka akianguka ubunge, mdogo wake Sumleck Ole Sendeka naye ameshindwa udiwani dhidi ya Haiyo Mamasita mgombea wa Chadema katika kata ya Naberera jimboni humo.
Kwa mujibu wa Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Simanjiro, Lucas Mweri, mgombea wa ACT-Wazalendo, Paulo Mwanache alipata kura 820, Ole Sendeka kura 27, 206, wakati Ole Millya ameshinda kwa kupata kura 41,420.Akizungumza mara baada ya kutangazwa kuwa mshindi, Millya aliwashukuru wakazi wa eneo hilo kwa kumchagua na akaahidi kuwalipa maendeleo waliyoyakosa kwa muda mrefu.
Alisema Jimbo la Simanjiro lina rasilimali nyingi ila jamii ni maskini, akidai hali hiyo imetokana na awali kukosa uongozi makini na kwamba atashirikiana na wananchi kuleta maendeleo.
Alisema ana deni kubwa kutokana na mapenzi makubwa waliyonayo wananchi wa jimbo hilo kwake hadi kumchagua kuwa mbunge wao.
Ole Sendeka alikubaliana na matokeo yaliyotangazwa na alimkumbatia Ole Millya baada ya kutangazwa kuwa mshindi.
Katika ngazi ya udiwani, CCM imeshinda kata saba na ukichanganya na tano ilizopita bila kupingwa inakuwa na kata 12, huku Chadema ikipata kata sita.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro aliyemaliza muda wake, Peter Tendee (CCM) ameshindwa kutetea udiwani wa kata ya Ruvu Remiti dhidi ya Dk. Ole Ranga wa Chadema.
Mtemvu ‘out’
Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Temeke, Fortunatus Kagimbo, amemtangaza Abdallah Ally Mtolea (Cuf) kuwa mshindi wa ubunge Jimbo la Temeke, baada ya kushinda kwa kura 103,231, dhidi ya mbunge wa jimbo hilo aliyemaliza muda wake, Abbasi Zuberi Mtemvu, aliyepata kura 97,557, Athumani Amiri Mcheka wa Chausta kura 5,799 na Shoo Amiri Abdi wa Chauma kura 5,375.
Wengine ni Makuwa Felix Marcus wa UPDP kura 457, Kigula Idd Kalekwa wa DP kura 1,318, Shan Ally Mussa wa AFP kura 1,878, Nancy Said Mrikaria wa TLP kura 910 na Ngulangwa Mohamed Msham wa ACT kura 7,941.
Kapuya ‘apigwa’ na Sakaya
Mbunge mkongwe kada wa CCM, Prof. Juma Kapuya, ameangushwa katika harakati za kuwania ubunge Jimbo la Urambo Magharibi na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (Cuf) Bara, Magdalena Sakaya, kwa kupata kura 21,982 dhidi ya 20,399 alizopata.
Akitangaza matokeo hayo, Msimamizi wa Uchaguzi Wilaya ya Kaliua, Athuman Kihamia, alitangaza matokeo hayo yaliyomng’oa Prof. Kapuya ambaye alishika jimbo hilo kwa kipindi cha miaka 20.
Aidha, Kihamia alisema katika Jimbo la Ulyankulu, John Kadutu wa CCM, alitangazwa mshindi kwa kupata kura 32,723, akifuatiwa na Deus Kitanyapondya wa Chadema kwa kura 9,432.
Tabora Mjini, Msimamizi wa Uchaguzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Zipola Liana, alimtangaza Emmanuel Mwakasaka (CCM) kuwa mshindi kiti cha ubunge jimbo hilo baada ya kupata kura 44,411 dhidi ya Peter Mkufya (35,452).
Shibuda, Cheyo waangukia pua
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa jana kwa nyakati tofauti, John Shibuda ambaye uchaguzi wa mwaka huu alikuwa akigombea Jimbo la Maswa Magharibi kupitia chama cha Tadea baada ya kujindoa Chadema na Sylivester Kasumbuayi (Chadema ) Jimbo la Maswa Mashariki wameangushwa katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktaba 25, mwaka huu, huku Meshack Opolukwa (Chadema) Jimbo la Meatu naye akibwagwa.
Katika wilaya ya Maswa ambayo ina majimbo mawili ya Maswa Mashariki na Maswa Magharibi, wabunge wote wawili, Shibuda na Kasulumbayi wameangushwa vibaya kwa tofauti kubwa ya kura katika uchaguzi huo.
Akitangaza matokeo ya uchagzui huo, Msimamizi wa Uchaguzi wa majimbo hayo, Trasias Kagenzi, alimtangaza Stanslaus Nyongo (CCM) kuwa mshindi kwa kupata kura 34,746 na kuwashinda Kasulumbayi aliyepata kura 19, 209, Peter Jibalya wa Tadea aliyepata kura 710 na Samuel Guya wa ACT-Wazalendo) aliyepata kura 304.
Katika Jimbo la Maswa Magharibi, mgombea wa CCM, Mashimba Ndaki, alitangazwa mshindi kwa kupata kura 76,150 na kuwashinda wagombea wenzake Shibuda, Patel Popat maarufu kwa jina la Abdalah (Chadema) na Tungu
Gasomi (ACT- Wazalendo).
WALIONG’ARA
Mnyika Kidedea
Mgombea ubunge Jimbo la Kibamba wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika, ametangazwa kuwa mshindi wa nafasi hiyo jimbo hilo, baada ya kujizolea kura 79,274, dhidi ya mpinzani wake, Dk. Fenela Mukangala wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyepata kura zaidi ya 55,000.
Ole Nangole akwaa ubunge Longido
Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Longido, Felix Kimario, amemtangaza Onesmo Ole Nangole (Chadema) kuwa ameshinda kiti cha ubunge katika jimbo hilo kwa kupata kura 20,176 na kumbwaga mpinzani wake Dk. Steven Kiruswa (CCM) aliyepata kura 19,361.
Ole Nangole alikuwa mwenyekiti wa CCM mkoa wa Arusha kabla ya kujiunga na Chadema na kisha kuwania ubunge kupitia chama hicho.
Akitangaza matokeo hayo huku akishukuru vyama vyote vya siasa kwa utulivu na kufanya kampeni za kistarabu, Kimario alisema kwa upande wa udiwani CCM imepata kata 17 na Chadema kata nane,
huku ACT -Wazalendo kikipata kata moja.
Dk. Mathayo atetea kiti chake
Mbunge aliyemaliza muda wake Jimbo la Same Magharibi, mkoani Kilimanjaro, Dk. David Mathayo David, ameibuka na ushindi na kutetea kiti chake.
Dk. Mathayo ambaye ni waziri wa zamani wa maendeleo ya mifugo na uvuvi alipata kura 21,418 dhidi ya mpinzani wake wa karibu wa Chadema, Christopher Mbajo, aliyepata kura 15, 347.
Katika toleo letu la jana tuliandika kwa makosa kwamba Dk. Mathayo ameshindwa katika kinyang’anyiro hicho. Usahihi ni kuwa ametetea kiti chake. Tunaomba radhi wote waliopata usumbufu kwa habari hiyo-Mhariri.
Msigwa ambwaga Mwakalebela
Mbunge wa Iringa Mjini aliyemaliza muda wake, Mchungaji, Peter Msigwa (Chadema) ametetea nafasi hiyo baada ya kupata kura 43,154 na kuwabwaga wapinzani wake, David Mwakalebela (CCM) aliyepata kura 32,406, mgombea wa ACT-Wazalendo, Chiku Abwao kura 411, Daud Masasi wa ADC aliyepata kura 123, Robert Kisinini wa DP aliyepata kura 26 na Pauline Chausta kura 66.
Mdee achomoza tena Kawe
Mbunge wa Jimbo la Kawe (Chadema) aliyemaliza muda wake, Halima Mdee, amefanikiwa kutetea tena jimbo hilo baada kuwabwaga wapinzani wake aliokuwa anapambana nao katika jimbo hilo.
Mdee amefanikiwa kutetea nafasi hiyo baada ya kutangazwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kinondoni, Mussa Natty, kupata kura 96,432, huku mpinzani wake mkuu kutoka CCM, Kippi Warioba akipata kura 83,061.
Bashe ang’ara Nzega Mjini
Katika Jimbo la Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), ametangazwa mshindi wa ubunge kwa kura 14,774 dhidi ya Charles Mabula (Chadema) aliyepata kura 9,658.
DK. Kigangwala ashinda Nzega Vijijini
Katika Jimbo la Nzega Vijijini, msimamizi wa uchaguzi katika jimbo hilo, Abdulrahman Mdeme, alimtangaza Dk. Hamis Kingwagala (CCM) kuwa mshindi kwa kupata kura 31,554, dhidi ya Joseph Malongo (Chadema) aliyepata kura 10,404.
Jimbo la Bukene, Selemani Zedi (CCM) alifanikiwa kutetea kiti chake kwa kuibuka kidedea baada ya kupata kura 30,998, akifuatia mgombea wa Chadema, Elias Maiko kura 13,704.
Magreth Sitta apeta
Katika Jimbo la Urambo, Magreth Sitta (CCM), alitangazwa kuwa mshindi wa ubunge kwa kupata kura 31 ,022, akifuatiwa na Samuel Ntakamulenga wa Chadema aliyepata kura 26,857.
Dk. Kafumu ashinda
Jimbo ya Igunga, Dk. Dalali Kafumu (CCM), alitetea nafasi yake ya ubunge kwa kupata kura 32,870, dhidi ya mgombea wa Chadema, Ngw’igulu Kube aliyepata kura 22,221.
Jimbo la Manonga, Seif Gulamali (CCM), alipata kura 31,485 akifuatiwa na mgombea wa Chadema 14,420
Jimbo la Igalula, mgombea wa CCM, Mussa Ntimizi alipata kura 26,369, akifuatiwa na mgombea wa Chadema, Maganga William (5,147).
Jimbo la Tabora Kaskazini, Almasi Maige wa CCM, alipata kura 32,792 dhidi ya 16,553 za Joseph Kidaha wa Chadema.
Jimbo la Sikonge, George Kakunda (CCM) alimshinda Haji Chambala wa Chadema kwa kura 31,344, dhidi ya 18,317.
Chenge, Chegeni washinda
Chama Cha Mapainduzi katika mkoa wa Simiyu kimefanikiwa kuyarejesha majimbo yote matatu yaliyokuwa chini ya Chadema katika wilaya za Maswa na Meatu.
Sura mpya za vijana zitaingia bungeni kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichotwaa majimbo yote saba ya Simiyu na Jimbo la Bariadi likibakia mikononi mwa Andrew Chenge.
Msimamizi wa Jimbo la Busega, Hamis Yunah, alimtangaza Dk, Chegeni, Raphael (CCM) kuwa mshindi kwa kupata kura 40,977 na kuwashinda wagombea Wengine, David William (Chadema) aliyepata kura 26,995 na Zangi
Robert (UDP) kura 802.
Katika Jimbo la Itilima zamani Jimbo la Bariadi Mashariki, msimamizi wa uchaguzi, John Lyimo, alimtangaza Daud Silanga (CCM) kuwa mshindi kwa kupata kura 55,850 na kuwashinda wagombea.
Wengine, Martin Makondo (Cuf) kura 28,000, Martine Magile (Chadema) kura 8,000 na John Cheyo (UDP) kura 5575.
Katika Jimbo la Bariadi, Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo, Abdalah.
Malela, alimtangaza Chenge (CCM) kuwa mshindi kwa kupata kura 79,095, Godwin Simba (Chadema) kura 63,448, Isack Cheyo (UDP) kura 621, Masunga Nghonzo (ACT- Wazalendo) kura 671 na Joseph Malis (DP) kura kura 541.
Mpina ashinda
Taarifa zaidi kutoka katika wilaya ya Meatu yenye majimbo ya Kisesa na Meatu, zinasema, Luhaga Mpina (CCM) amefanikiwa kutetea kiti cha ubunge, huku Salum Hamis (CCM) aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo hilo 2005 hadi 2010 akibuka mshindi dhidi ya mbunge anayemaliza muda wake, Opulukwa (Chadema).
Mbatia, Komu waibuka kidedea
Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, ameshinda kiti cha ubunge Jimbo la Vunjo, baada ya kupata kura 60,187, akimwacha kwa mbali wapinzani wake Innocent Shirima (CCM), aliyepata kura 16,097 na Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema, aliyepata kura 6,416.
Akitangaza matokeo hayo juzi usiku, msimamizi wa uchaguzi wa majimbo ya Moshi Vijijini na Vunjo, Fulgence Mponji, alisema Mbatia alishinda kiti hicho baada ya kuwabwaga washindani wake hao.
Aidha, akitangaza matokeo ya Jimbo la Moshi Vijijini, alisema Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Chadema, Anthony Komu, ameshinda baada ya kumwangusha waziri wa zamani wa viwanda na biashara, Dk. Cyril Chami kwa kura 55,815.
Mponji alisema Dk. Chami alipata kura 24,415 na mgombea ubunge wa chama cha DP, Obote Kimambo alipata kura 597.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment