NA EDITOR
28th October 2015.
Shughuli za kawaida za wananchi zilisimama katika baadhi ya sehemu kutokana na ofisi na maduka kufungwa.
Polisi na askari wa Jeshi la Wananchi wa Watanzania (JWTZ), walikuwa wameweka ulinzi katika sehemu mbalimbali za Zanzibar.
Hali hiyo hiyo ya wasiwasi iliongezeka zaidi baada ya mgombea wa Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha CUF, Seif Sharrif Hamad, kutangaza matokeo ya uchaguzi huo, kabla ya kutolewa rasmi na Tume ya Uchaguzi Zanzibar.
Mambo yanayotokea Zanzibar ni ya kusikitisha kutokana na ukweli yanaibua maswali kuwa kwanini kila ikitokea uchaguzi visiwani humo basi kunakuwa na hali ya wasiwasi ya kiusalama.
Hii sii mara ya kwanza kwa hali hiyo kutokea, kwani hali ya sintofahamu imekuwa ikitokea tangu uchaguzi wa chini ya mfumo wa vyama vingi uliporudishwa nchini mwaka 1995.Pamoja na jitihada nyingi za ndani ya nje ya nchi, lakini bado inaonekana wanasiasa wa Zanzibar wameshindwa kuweka misingi ya kuhakikisha kuwa watu wa Zanzibar wanachagua viongozi wao kwa amani na utulivu.
Inasikitisha kuona kuwa kila inapotokea suala la uchaguzi huko Zanzibar basi joto la kisiasa hupanda kiasi cha kutishia amani.
Mvutano zaidi huhusisha vyama viwili vya CCM na CUF, ambavyo viongozi wake wamekuwa wakivutana kiasi cha kusababisha sintofahamu miongoni mwa wananchi wa Zanzibar.
Hali ya Zanzibar siyo shwari kwa jumla na hasa kutokana na mvutano huu wa sasa wa matokeo na jambo la kusikitisha zaidi ni kuwa viiongozi wa Tume ya Uchaguzi wa Zanzibar (Zec) wamekuwa kimya.
Hata hivyo, tatizo kubwa la uchaguzi wa Zanzibar limekuwa linasababishwa zaidi na ucheleweshaji wa kutangaza matokeo yake.
Ni jambo la kushangaza kuona kuwa, uchaguzi umefanyika Jumapili iliyopita lakini Zec ilishindwa kutangaza mapema matokeo ya uchaguzi wa rais, wawakilishi na wabunge.
Hali hiyo kwa kiasi kikubwa imekuwa ikiongeza joto la kisiasa huko na hata kufikia kutishia amani.
Hivi sasa askari wengi wamejaa kwenye mitaa mbalimbali ya Zanzibar kiasi cha kuleta hali ya wasiwasi bila ya lazima.
Ilitegemewa kuwa kutokana na Zanzibar kuongozwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa miaka mitano kuwa bila shaka ingesaidia kupunguza mivutano lakini hali imekuwa tete.
Ni jambo la kushangaza kuwa kuna baadhi ya viongozi wamekuwa wakitumia historia ya kisiasa kujaribu kupandikiza chuki na mgawanyiko miongoni mwa wananchi wa Zanzibar.
Mathalani, baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakikumbushia siasa za vyama vya zamani vya ASP, ZNP na ZPPP, ambavyo vilikuwa na mvutano mkubwa katika miaka ya 1950 na 1960 na kuleta mambo hayo katika kipindi hiki.
Tunatoa wito kuwapo kwa busara na miongoni mwa viongozi wa Zec, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na viongozi wa CCM na CUF.
Pia wanaisasa wa Zanzibar wanapaswa kujifunza kuvumiliana na kufahamu katika masuala ya uchaguzi lazima wawepo wanaoshindwa na wanaoshinda.
Matumizi ya vyombo vya dola katika harakati za kuendesha uchaguzi wa demokrasia kunaongeza chuki tu na kupunguza nafasi ya demokrasia kuchukua mkondo wake.
Pia viongozi wa vyama vya CCM na CUF wanapaswa kuchunga kauli zao ili kutochochea chuki za kisiasa na kuacha demokrasia
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment