.png)
Hospitali ya Rufaa ya Manispaa ya Ilala Amana, inahitaji mashine za MRI na CT-Scan ili kusaidia madaktari kutambua matatizo ya wagonjwa kwa undani.
Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Meshack Shimwela, alisema hayo jana wakati akipokea msaada wa vitanda, mashuka, mashine za hewa ya Oxgen na viti ya kutembelea wagonjwa vyenye thamani ya Sh. Milioni 10 kutoka Benki ya DTB jijini Dar es Salaam.
Alisema kutokana na kukosekana kwa vipimo hivyo vikubwa, wamekuwa wakiwapeleka wagonjwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa ajili ya matibabu.
“Kwa sababu hatuna vipimo hivi inatuwia vigumu kufahamu kwa urahisi mgonjwa anaugua nini hivyo unakuta tunatumia zaidi ya dawa kumi kutibu ugonjwa ambao mwisho wa siku unapona kwa dawa moja,” alisema.Shimwela pia aliiomba serikali kuwapatia vifaa hivyo ili kutoa huduma hizo muhimu kwa wagonjwa wanaofika hospitalini hapo pamoja na kurahisisha utoaji huduma.
Pia aliishukuru benki hiyo kuwa moja ya wadhamini wao ambao wanasaidia kuendesha huduma za matibabu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Maendeleo ya Bidhaa na Masoko, Sylvester Bahati, alisema Benki hiyo itaendelea kutoa huduma kwa jamii katika sekta ya Afya, Elimu na Huduma za Jamii.
“Tunaahidi kuwa sehemu ya watoa huduma katika hospitali hii kwa sababu benki hii imeamua kuwa sehemu ya kuhudumia jamii katika sekta ya Afya, Elimu na huduma za jamii,” alisema Bahati.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment