
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ameuagiza uongozi wa soko la Kariakoo na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwenda kujieleza ofisini kwake Jumatatu ijayo, baada ya kushuhudia bidhaa zikiwa zimepangwa chini sokoni hapo.
Majaliwa alichukua hatua hiyo baada ya kushiriki kufanya usafi katika soko hilo kuadhimisha Siku ya Uhuru wa Tanganyika inayoadhimishwa Desemba 9 kila mwaka.
Akizungumza baada ya kufanya ukaguzi sehemu ya chini ya soko hilo maarufu kama Shimoni na kuona bidhaa zimepangwa chini, Majaliwa alisema ni muhimu kukutana na viongozi hao ili kujadili na kujua mipango endelevu juu ya soko hilo.
“Nataka siku ya Jumatatu saa 4:00 asubuhi viongozi wa soko na mkuu wa mkoa mje ofisini kwangu mnieleze mikakati yenu au kama kupanga bidhaa chini ndio moja ya maendeleo ili nijue,” alisema na kushangiliwa na wananchi waliokuwapo eneo hilo.
Alisema lengo la kuifanya siku hiyo kuwa maalum kwa usafi ni kuwajengea wananchi nidhamu na uwajibikaji katika kuijenga nchi yao.
Majaliwa alisema yeye na Rais Dk. John Magufuli, wataendelea kutekeleza kauli mbiu ya ‘Hapa kazi tu’ kwa ajili ya kubadilisha mfumo wa utendaji kazi serikalini na jamii nzima ili uendane na kasi ya matarajio ya wananchi.
Majaliwa alisema yeye na Rais Dk. John Magufuli, wataendelea kutekeleza kauli mbiu ya ‘Hapa kazi tu’ kwa ajili ya kubadilisha mfumo wa utendaji kazi serikalini na jamii nzima ili uendane na kasi ya matarajio ya wananchi.
“Tunaposema hapa kazi tu, tuna maanisha kila mtu awawajibike sehemu yake, wanapolala na wanapoamka wafanye kazi tu na ndio maana tunasema sasa ni kazi tu,” alisema.
Aliagiza wafanyabiashara wajengewe mpango maalum wa kufanya shughuli zao bila usumbufu kutoka kwa askari mgambo.
Aidha, alisema mawaziri watakaochaguliwa na wakurugenzi wa halmashauri watakaa pamoja kuangalia njia bora za kuboresha biashara za wafanyabiashara wadogo kukomesha kusumbuliwa.
KUNA HUJUMA
Waziri Mkuu Majaliwa alisema serikali ya awamu ya tano inaendelea na operesheni ya kupambana na watu wanaohujumu uchumi wa nchi na kuanza kwa kusafisha Mamlaka ya Bandari (TPA), kampuni ya Reli (TRL) na Mamlaka ya Mapato (TRA).
“Tumeanza operesheni hiyo kwa nguvu tumegundua kuna hujuma kubwa, lakini tunawadhibiti wote wanaohusika pamoja na kuwachukulia hatua kali,” aliongeza kusema bila kufafanua.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment