Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Augustino Maiga akizungumza, Dar es Salaam jana wakati wa Mkutano na mabalozi wa nje wanaoziwakilisha nchi zao. Picha na Wizara ya Mambo ya Nje
Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga amekutana kwa mara ya kwanza na mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini na kusema Tanzania inaheshimu tunu za kimataifa za haki za binadamu na demokrasia na kwamba mgogoro wa Zanzibar usiwe kigezo cha baadhi ya nchi kudharau hatua kubwa za kidemokrasia zilizofikiwa.
Akizungumza na wanahabari baada ya mkutano huo jana, Balozi Mahiga aliitaka kila nchi kuheshimu na kulinda uhuru wa nyingine akisema hakuna sababu ya mataifa mengine kujiona ni makubwa au tajiri kuliko mengine.
“Wengine wanajua kabisa taratibu za kuheshimiana lakini wanaamua kwa makusudi kutumia uwezo wa kutudharau isivyopaswa. Lakini wanatakiwa kuheshimu uhuru wetu kama tunavyoheshimu wao. Uhuru wetu haujadiliki,” alisema.
Kuhusu hatua iliyofikiwa Zanzibar, Balozi Mahiga alisema mazungumzo baina ya viongozi wa visiwa hivyo yanaendelea vyema na kuitaka jumuiya ya kimataifa kuwa na subira.
Alisema msimamo wa Tanzania unafahamika katika masuala mbalimbali ya kimataifa na kwamba haitakubali uhuru wake udharauliwe kwa sababu ya umaskini.
“Katika kutatua mgogoro wa Burundi, Warundi wataanza majadiliano yao wenyewe Desemba 28 jijini Kampala, Uganda na kufuatiwa na mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Jumuiya Afrika Mashariki, Arusha Januari 8 na baadaye mkutano wa wakuu wa nchi hapo baadaye,” alisema Mahiga.
Katika mkutano, mabalozi hao walipongeza hatua za mwanzo za utendaji wa Serikali ya Rais John Magufuli wakisema unaonyesha matumaini chanya kwa siku zijazo.
Mabalozi hao walisema msimamo na kasi ya Rais Magufuli katika kupambana na rushwa, ubadhirifu, ukwepaji kodi na kuongeza uwajibikaji vinaonyesha amedhamiria kubadilisha nchi.
“Tunampongeza Rais Magufuli kwa kuanza kushughulikia masuala nyeti ya kupambana na rushwa, kuongeza uwazi na uwajibikaji na kuondoa umasikini,” alisema Balozi wa Canada nchini, Alexender Leveque.
Balozi wa Somalia nchini, Mohamed Abdi alisema kuna matumaini kwa namna Rais Dk Magufuli alivyoanza kuiendesha Serikali hasa katika kuondoa rushwa ambao ni ugonjwa sugu barani Afrika.
No comments :
Post a Comment