
Rais mstaafu wa awamu ya pili, Alhaji Hassan Mwinyi, ametoboa siri ya ukakamavu alionao licha ya umri mkubwa na kuwaasa vijana kuacha kuendekeza anasa kama wanataka kufika umri wake.
Mwinyi ambaye alitimiza miaka 90 Mei 8, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki, wakati wa mahafali ya nane ya Chuo Kikuu cha Tina na Teknolojia (IMTU), ambapo alikuwa mgeni rasmi.
Alisema aligundua mapema aina ya maisha anayopaswa kuishi, hivyo aliamua kuachana na vitu visivyo vya lazima katika maisha na ndiyo sababu bado ni mkakamavu licha ya umri wake mkubwa.
Alisema katika maisha yake hajawahi kunywa pombe wala kuvuta sigara.
“Hivi nilivyo msidhani ni kwa bahati tu, hapana nimefika hapa kwa mipango, sikujihusisha kabisa na anasa kama unywaji wa pombe na uvutaji sigara na ndiyo sababu unaona naweza kusoma bila hata kutumia miwani,” alisema Mwinyi na kuwafanya wageni kuangua kicheko.Aidha, aliwaambia wahitimu hao kuwa wanapaswa kufuata nyayo zake kama wanataka kuwa na afya njema hata watakapokuwa na umri mkubwa kama yeye.
“Mkawaambie na wenzenu kwamba ulevi wa pombe na uvutaji wa sigara unadhoofisha afya zao, hayo ni mambo mnayoweza kujiepusha nayo na mkaishi salama,” alisisitiza.
Mwinyi pia aliwataka kuwa na kawaida ya kufanya mazoezi mara kwa mara ili kujenga mwili hali ambayo itawawezesha kuendelea kuwa wakakamavu hata watakapokuwa watu wazima.
“Mimi jogging ni kawaida yangu, msikae bila kufanya mazoezi ambayo yanawafanya muwe na afya njema,” alisema mzee Mwinyi.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment