
Wabunge mbalimbali walilieleza Nipashe jana kuwa fedha hizo za mikopo bado hawajazipata licha ya kuwa walijaza fomu muda mrefu.
Kila Mbunge anakoposhwa Sh. milioni 90 kwa ajili ya kununulia magari, na wengi wao wamekuwa wakichukua Toyota Landcruiser VX.
Mbunge wa jimbo la Mtera, Livingstone Lusinde (CCM), alisema yeye hajaona fedha hiyo kwenye akaunti licha ya kwamba alijaza fomu za maombi muda mrefu.
Alisema kwa sasa amekuwa akitumia fedha zake katika kufanikisha majukumu yake mpaka atakapopewa mkopo huo ambao "haujulikani utatolewa lini."
Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini (Chadema), Pauline Gekul, alisema fedha hizo bado hazijaingia kwenye akaunti yake licha ya kwamba alishajaza fomu za maombi.Nipashe lilizungumza na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Ofisi ya Bunge, Owen Mwandumbya na kusema "mchakato unaendelea wa kuwapatia wabunge fedha hizo."
Alisema wabunge wengi wako majimboni hivyo bado hawajapata fedha hizo kutokana na wengine kutojaza fomu zinazotakiwa kwa jili ya kupata mkopo huo.
"Naamini wakirudi watajaza fomu na wanachotakiwa ni kufuata taratibu za maombi ya fedha hizo na sehemu ya maombi hayo yanaidhinishwa na Ofisi ya bunge na kupelekwa ofisi ya Hazina ili kupewa fedha," alisema Mwandumbya.
Alisema utaratibu wa kawaida wa kila Bunge jipya ni kwamba serikali huwapa wabunge ruzuku ya Sh milioni 45 na mkopo wa Sh. milioni 45 hivyo kufikia jumla ya Sh. milioni 90.
Hata hivyo kumekuwepo na mvutano katika fedha hiyo ambapo wabunge wametaka walipwe kulingana na bei ya soko kutokana na Dola ya Marekani kupanda na hivyo kusababisha shilingi kuporomoka.
Baadhi ya wabunge wanataka walipwe Sh. milioni 130 ambazo wanadai ndiyo bei ya magari wanayotakiwa kutumia huku serikali ikiendelea na msimamo wake wa kutoa Sh.milioni 90.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment