
Asilimia kubwa ya vijana jijini Dar es Salaam wamejitokeza kwa wingi kufanya usafi katika maeneo yao, huku wakitamka kauli ya Rais Dk. John Magufuli ya ‘Hapa kazi tu’.
Nipashe jana ilitembelea baadhi ya maeneo ya jiji hilo na kukuta vijana, wa kike na wa kiume wakishiriki kwa hamasa kubwa kufanya usafi kwa vitendo.
Katika eneo la Kimara Bonyokwa kwa Mashilingi, Nipashe ilizungumza na baadhi ya vijana hao akiwamo, Juma Iddy, ambaye alisema kama vijana watabeba dhana ya usafi katika maisha yao katika kila jambo wanalofanya, itabadilisha maisha yao na taifa kwa ujumla.
“Sisi kama vijana tunaohitaji maisha yenye mabadiliko yatakayoleta hali chanya kwetu na taifa zima, basi hatuna budi kumuunga mkono Rais wetu kwani ameonyesha njia na mabadiliko ya kweli,” alisema na kuongeza:
“Rais Magufuli anaendelea kutumbua majipu katika mioyo yetu kwa vitendo kama alivyokuwa akisema wakati wa kampeni; “Nichagueni mimi Magufuli ili niwatumikie, nawaahidi sitawaangusha.”
Alisema uamuzi wa Watanzania kumchagua Magufuli kuwa Rais wao ni sahihi, ndiyo maana wameitikia kwa wingi hasa vijana agizo lake la siku ya Uhuru Desemba 9 iwe ya kufanya usafi wa mazingira katika maeneo yao.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment