.png)
Katika kipindi cha mwezi mmoja cha kuwa madarakani, tayari serikali ya Magufuli imebaini ukwepaji kodi kwa kupitisha makontena 349 yaliyolikosesha taifa Sh. bilioni 80 kabla ya baadaye kugundulika kuwa jumla ya makontena yaliyopitishwa bandarini bila kulipiwa kodi ni 2,431.
Kikwete amesema wakati wa uongozi wake hakuwahi kuagiza mtu yeyote anayestahili kulipa kodi asilipe.
Kikwete alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na wananchi wa Chalinze juu ya maadhimisho ya Siku ya Uhuru ambayo imesherehekewa kwa kufanya usafi katika maeneo mbalimbali nchini kutokana na agizo la Rais Magufuli.
Alisema haamini kama ndani ya familia yake kuna mtu alisaidia ukwepaji kodi, kwa kuwa urais ulikuwa wake na hakuwa na ubia na mtu yeyote. “Urais ulikuwa wangu, sikuwa na ubia na mke wangu, familia yangu, wala sikuwa na ubia na mtu yeyote, nilichaguliwa mie na nikatimiza wajibu wangu,” alisema na kuongeza: “Tusiondolewe kwenye mstari kwa maneno yasiyokuwa na kichwa wala miguu, narudia tena, wakati wangu sijawahi kuagiza mtu yeyote anayestahili kulipa kodi asilipe kodi, na wala siamini kuwa kwenye familia yangu kuna mtu anaweza kufanya hivyo, kama mie mwenyewe mwenye mamlaka sikufanya hivyo, siamini kama mwingine angefanya,” alifafanua.
Aidha, aliwashukuru wananchi hao na kuwaeleza amefurahishwa na kujitokeza kwao kufanya usafi na kuwataka wananchi hao kudumisha mila na tabia ya usafi.
Tangu kuanza kazi Novemba 05, mwaka huu, Rais Magufuli ‘amelia’ na wakwepaji kodi Bandarini TRA.
Novemba 27, mwaka huu, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alifanya ziara ya kushtukiza TRA na TPA, na kubaini ukwepaji kodi wa kontena 349 zenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 80.
Kutokana na kushindwa kuwajibika kwa baadhi ya watumishi wa mamlaka hizo, rais alitangaza kutengua uteuzi wa Kamishna wa TRA, Rished Bade na kumteua Dk. Phillip Mpango kukaimu nafasi hiyo. Pia, Maofisa watano ambao ni Kamishna wa Forodha, Tiagi Masamaki, Mkuu wa Kituo cha Huduma kwa Wateja, Habibu Mponezya, Mkuu wa Kitengo cha Tehama, Haruni Mpande, Hamisi Ali Omari (hakutaja ni wa Idara gani) na Mkuu wa Kitengo cha Bandari Kavu, Eliachi Mrema walisimamishwa kazi.
Watumishi hao wameshafikishwa katika Mahakama ya Kisutu na kusomewa mashtaka ya uhujumu uchumi na wako mahabusu.
Desemba 4, mwaka huu, Waziri Mkuu, alifanya ziara nyingine Bandarini kukagua mfumo wa uondoshaji mizigo Bandarini na baadaye alitoa orodha ya makontena 2,387 yaliondoshwa bandarini bila kulipiwa kodi yoyote.
Kadhalika Desemba 7, mwaka huu, uamuzi wa rais ulisomwa mbele ya waandishi wa habari kuwa ametengua uteuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Shabani Mwinjaka, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Awadhi Massawe, Mwenyekiti wa Bodi ya TPA, Profesa Joseph Msambichaka na kuvunja bodi hiyo.
Pia, Waziri Mkuu, aliwasimamisha kazi watumishi 13 wakiwamo viongozi watano wa bandarini na kuagiza wakamatwe na uchunguzi ufanyike mara moja.
Hadi sasa jumla ya watumishi waliokamatwa na Jeshi la Polisi kwa makosa ya ukwepaji kodi ni 76 na baadhi wameshafikishwa mahakamani.
Desemba 4, mwaka huu, Rais Magufuli alikutana na wafanyabiashara na wawekezaji katika mkutano uliofanyika Ikulu ulioandaliwa na Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) na Baraza la Biashara la Taifa (TNBC).
Katika mkutano huo rais aliwaomba wafanyabiashara hao kumuunga mkono kwa kulipa kodi na kuzuia mianya yote ya kodi ambayo alieleza serikali inaifahamu na inafuatilia kwa karibu.
Aidha, rais alieleza kuwa hakuchangiwa na mfanyabiashara yeyote kuingia Ikulu, kwa kuwa alijua anakwenda kufanya kazi ikiwamo ukusanyaji wa mapato.
Rais Magufuli aliwataka wafanyabiashara kuwa wazalendo na kumuogopa Mungu kwa kuwa wafanyabiashara wadogo ndiyo wanaolipa kodi, lakini wakubwa wanakwepa.
Alizitaja baadhi ya sekta ambazo zikisimamiwa vizuri zitaliwezesha taifa kupata fedha za kuendeha nchi na kuondokana na kutegemea wafadhili kila bajeti kuwa ni viwanda, uvuvi, utalii na madini.
Alisema Tanzania ni nchi tajiri lakini kuna mianya mingi ya ukwepaji kodi kwa fedha kunufaisha watu wachache badala ya Watanzania wengi.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment