.png)
Kadhalika, kimesema serikali hiyo haijajikita katika kuleta mabadiliko ya kimfumo ikiwamo kubadili mikataba ya kinyonyaji ya rasilimali, hususani madini na mafuta, kufuta posho za vikao katika mfumo wa utumishi wa umma ikiwamo Bunge na kuachana na matumizi ya magari ya anasa (mashangingi).
Kimesema katika kipindi cha siku 100 za serikali ya awamu ya tano, Rais Magufuli hajaonyesha nia ya kufumua mikataba mibovu ya madini ambayo imekuwa ni kilio kikubwa cha Watanzania, hajaonyesha nia ya kushughulikia suala la Katiba mpya na hakuna mpango wa kuifanyia mabadiliko Taasisi ya Kupambana na Kuzuia na Rushwa (Takukuru).Mbali na hilo pia kimesema, hakuna uwazi hususani kwa viongozi wake kuonyesha mali wanazomiliki na kwamba hata hali ya maisha kwa wananchi inaendelea kuwa ngumu kwa kuendelea kupanda kwa bei za bidhaa za sukari, mchele, mafuta ya kula na kuendelea kuagiza sukari nje ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, wakati akitoa maamuzi ya Kamati Kuu ya chama hicho iliyokaa juzi, Kiongozi Mkuu wa Act-Wazalendo, Zitto Kabwe, alisema kama serikali hiyo ina nia ya dhati ya kupambana na ufisadi, ni lazima ionyeshe kwanza uwazi kwa viongozi wake.
“Ukisikiliza hotuba za Rais Magufuli, mambo anayoyazungumza ni yale yale, unaposema unatumbua majipu au unapambana na ufisadi lazima uhakikishe unaboresha mfumo mzima na kuuweka katika misingi ya kisheria, bila kuweka katika mfumo wa kisheria huwezi kubadilisha chochote. Nchi ni taasisi si ya mtu mmoja, nikitolea mfano, aliyekuwa Mkurugenzi wa Takukuru, Dk. Edward Hosea, amefukuzwa Takukuru lakini hakuna jambo lolote lililobadilika,” alisema Zitto.
Kuhusu uchaguzi wa marudio Zanzibar, Zitto alisema kamati ya chama hicho imeamua chama hicho kisishiriki katika uchaguzi huo kwa madai kuwa misingi ya sheria ya kufutwa uchaguzi huo ilikiukwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, kwani hakuwa na uhalali wa kufuta uchaguzi huo kikatiba na kisheri.
Pia, aliitaka Zec kuwatambua wawakilishi na madiwani waliotangazwa tume hiyo katika uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana, na waanze kufanya kazi ya kuwatumikia wananchi.
Aidha, Zitto alitoa taarifa ya matumizi ya fedha ya chama hicho katika uchaguzi uliopita, kuwa ni Sh. milioni 656.6 na kuviomba vyama vingine vya siasa kutoa taarifa ya matumizi fedha katika uchaguzi uliopita.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment