NA CHRISTINA MWAKANGALE
15th February 2016.

Pensheni hiyo itatolewa kwa hata ambao hawakuwa watumishi wa serikali, ili kuwawezesha kujikimu.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, alisema hayo jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa kitabu cha ‘Ninastaafu Kazi, Sistaafu Maisha’ ambacho kimelenga kuwaandaa Watanzania kustaafu.
Alisema kwa sasa maisha ya wastaafu na wazee yana changamoto kubwa kwa kuwa baadhi yao wanashindwa kujikimu kimaisha hasa katika upatikanaji wa huduma za afya.
Alisema hali hiyo inatokana na ukosefu wa fedha baada ya kustaafu na uzeeni, huku wengi wao wakiwa si wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii.
“Wastaafu wengi muda kustaafu ukikaribia na baada ya kustaafu huwa wanyonge kutokana ukweli kwamba maandalizi wakiwa wameajiriwa huwa madogo. Kitabu hiki tukisome na kitatusaidia kujiandaa,” alisema Dk. Kijaji.
Alisema serikali inatambua pensheni inayolipwa sasa ni ndogo, lakini inakidhi mahitaji kidogo, huku akisisitiza kuwa kundi kubwa la wastaafu ambao hawakuwa watumishi wana changamoto kubwa zaidi.
“Pensheni ya Sh.100,000 inaweza kuwa ndogo kulingana hali ya uchumi, lakini ambao walijiajiri, tumeona nao wawekwa katika mfumo wa pensheni,” alisema.
Naye mtunzi wa kitabu hicho, Mkurugenzi wa taasisi ya PS Counseling and Consultants, Mchungaji Mkumbo Mitula, alisema wazee ni historia, hazina na zawadi, hivyo wanapaswa kutambuliwa umuhimu wao katika jamii.
Alisema kipato kidogo baada ya kustaafu na uzee ni changamoto kubwa, hivyo maandalizi ya kisayansi hutumika duniani kote ili kukabiliana na changamoto hizo.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment