dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, February 7, 2016

Kikwete: Uchaguzi haukuwa rahisi

Rais John Magufuli akisalimiana na Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete baada ya kuwasili katika Uwanja wa Namfua, Singida jana kwa ajili ya kilele cha maadhimisho ya miaka 39 ya kuzaliwa kwa chama hicho. Picha na Ikulu
By Waandishi Wetu, Mwananchi 
Dar/Singida. Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete amesema uchaguzi mkuu uliopita haukuwa rahisi na kuonya kwamba hakuna sababu ya kurudia makosa yaliyokisababishia chama hicho ugumu.
Akihutubia mamia ya wakazi wa Singida katika maadhimisho ya miaka 39 tangu kuanzishwa kwa CCM, Kikwete aliwataka wanaCCM kuwapuuzia na kuwanyanyapaa wenzao ambao wamekuwa wakitumia chama hicho kama ngazi za kupata uongozi na wanapoukosa huamua kuhama.
“Nikiri kwamba uchaguzi mkuu wa mwaka jana, ulikuwa ni mgumu kwa upande wa CCM. Lakini kwa vile CCM ni chama pekee chenye sura ya kitaifa, pamoja na kelele na kejeli nyingi kiliibuka na ushindi mnono,” alisema Kikwete.
Katika sherehe hizo zilizohudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa chama na Serikali akiwamo Rais John Magufuli, Kikwete aliwataka wanaCCM wajifunze kupitia uchaguzi huo na wajiandae kwa uchaguzi ujao ili kuhakikisha chama kinaendelea kushika dola.
“Uchaguzi umemalizika sasa tuchape kazi na tushirikiane kuleta maendeleo, tuvumiliane kimtazamo na kikubwa tuwasikilize wananchi wanataka nini kwa Serikali yao, tusirudie makosa yaliyojitokeza huko nyuma,” alisema.
Kusafisha chama
Rais huyo mstaafu aliwataka viongozi wenye sifa mbaya ndani ya chama hicho na ambao wamekuwa wakitumia nafasi zao kama ngazi ya kupata vyeo kujiondoa wenyewe.
Alisema wakati uliopo ni wa kujisahihisha, kujikosoa na kutumia sherehe hizo kutafakari ni wapi chama hicho kimetoka, kilipo na kinakoelekea.
CCM na utegemezi
Alirejea kauli yake kuwa wakati wa kuendelea kutegemea fedha za ruzuku na michango ya wafanyabiashara kukiendesha chama kiuchumi umepita na hivyo inahitajika mipango madhubuti itakayokiingizia mapato.
Huku akikiagiza chama hicho kuisimamia Serikali, Kikwete alisisitiza kauli yake aliyoitoa juzi alipozungumza na wazee wa Singida, kuwa sherehe hizo ni za mwisho kwake akiwa mwenyekiti wa CCM, kwani mwakani atakuwa ameshamkabidhi kijiti Rais John Magufuli.
Kamati ya Maadili
Mwenyekiti hiyo pia alikumbushia mchakato wa kumpata mgombea urais wa chama hicho akisema haukuwa rahisi na ulijaa vitisho, lakini chama kilifuatilia mienendo ya wagombea mpaka kumpata mgombea makini.
“Nilisema poeni moyo, chama kitawaletea wagombea wazuri kwa nafasi zote na nilimaliza kwa kusema ‘haliharibiki jambo chini yangu kwa chama hiki kikongwe’. Nilisema kwa kujidai kwa kuwa najua CCM ina utaratibu mzuri unaoeleweka wa kupata wagombea walio bora,” alisema.
Alitumia fursa hiyo kuwapongeza wajumbe wa kamati za usalama na maadili ngazi za wilaya, mkoa pamoja na mwenyekiti wa kamati ndogo ya maadili Taifa, Philip Mangula kwa “kufanya kazi nzuri ya kufuatilia mienendo ya wagombea.”
“Kila siku (Mangula) ananiambia leo nimefungua faili la 10, baadaye ananiambia kaa hapa wameongezeka kwa kasi wamefika 17, akisimama NEC (Halmashauri Kuu) watu wanacheka kwa sababu wanajua tayari kuna faili jingine, nampongeza kwa kazi nzuri imesaidia sana kamati ya maadili kwa kuwa mimi ndiyo mwenyekiti wake katika kufanya kazi ya uchambuzi ya nani ni nani,” alisema Kikwete.
Aliongeza: “Mapendekezo yetu yalileta nafuu ya kazi kwa Kamati Kuu katika kazi yake ngumu ya kuchuja wagombea 38 na kupata majina matano yaliyofikishwa NEC, kwa kiasi fulani ilisaidia kuongoza kikao kigumu cha Halmashauri Kuu ya Taifa mpaka kupata wagombea watatu waliofikishwa Mkutano Mkuu na kupata mgombea ambaye ndiye Rais John Magufuli.”
Uchaguzi zanzibari
Akizungumzia uchaguzi wa Zanzibar, Kikwete alisema CCM haikutamani wala kupenda uchaguzi kurudiwa bali ni kutokamilika kwa mchakato wa uchaguzi huo.
Kikwete ambaye amelaumiwa na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kwa kutumia dola kuingilia uchaguzi huo, alisema kitendo cha Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kufuta uchaguzi na kuitisha mwingine ni kinyume na matakwa ya chama hicho, kwani wanaCCM walitamani usingerudiwa.
“Lakini tutafanyaje kwa maana Tume ya Uchaguzi Zanzibar yenye mamlaka inasema kulikuwapo na dosari kubwa kiasi cha wao kulazimika kufuta uchaguzi na kuandaa upya,” alisema na kuongeza;
“Tume huru mamlaka ya mwisho baada ya kushauriana na wenzetu wa Zanzibar tumelazimika kuupokea, tumeukubali kwa shingo upande maana tulijiandaa kusherehekea, nawaomba wanaCCM wa Zanzibar wajiandae kwa ukamilifu kushiriki uchaguzi huo kama ilivyoelekeza ZEC na wajitokeze kwa wingi Machi 20 kupiga kura.”
Kikwete aliwakaribisha na kuwapongeza waliokuwa wabunge viti maalumu katika Bunge la 10 kupitia Chadema, Rachel Mashishanga na Christowaja Mtinda ambao walikabidhi kadi za vyama vyao na kujiunga rasmi na CCM.
Magufuli na elimu bure
Awali, akizungumza wakati wa sherehe hizo, Rais Magufuli alisema katika kutekeleza Ilani ya CCM, alianza na elimu bure ambayo imekumbana na changamoto kadhaa.
“Tumepata changamoto kubwa kwa sababu kabla ya hapo wanafunzi waliokuwa wanaingia darasa la kwanza walikuwa hawafiki 70 kwa darasa, lakini sasa unakuta darasa moja lina wanafunzi 600 hadi 900,” alisema.
Akirejea mchango wa madawati 1,000 yaliyotolewa na wanaCCM Singida jana, Rais Magufuli aliwaomba viongozi wote katika mikoa wakiwamo wakuu wa wilaya na wakurugenzi wapunguze safari na ulaji ili fedha hizo wakazitumie kununulia madawati ili watoto wanaokwenda shule wasikae chini.
“Hiki kitakuwa kipimo cha wakuu wa wilaya, mikoa na wakurugenzi, ikiwa sivyo itabainisha kwamba nafasi uliyonayo haikufai, kwa hiyo kila mmoja ajipange katika kuhakikisha anatoa kero kwa watu anaowaongoza,” alisema.
Imeandikwa na Tumaini Msowoya, Herieth Makwetta na Gasper Angrew
Sherehe za kubana matumizi
Mapema, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema katika kutekeleza Ilani ya CCM wameamua kuondoa hafla na mambo mengineyo katika sherehe hiyo na fedha zilizookolewa zimenunulia madawati ili kuendana na kasi ya Magufuli ya ‘Hapa Kazi Tu’.
Alisema akiwa katibu mkuu, hakutaka kujitafutia shari na Rais Magufuli hivyo, hakununua hata maji ya kunywa na kwamba kila aliyehudhuria arudi nyumbani kwake kutafuta chakula na vinywaji.
“Michango tuliyoipata tumeamua kuitumia kwa madawati tuliyonunua zaidi ya 1,000 na leo mwenyekiti wa CCM utakabidhi madawati 300 ambayo pamoja na yale mengine yatagawiwa katika shule za manispaa za Singida,” alisema Kinana.
Imeandikwa na Tumaini Msowoya, Herieth Makwetta na Gasper Angrew

No comments :

Post a Comment