Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Tuesday, February 16, 2016

MAFURIKO: Wanafunzi 200 ndani ya darasa moja


Achana na shule zilizoko maelfu ya kilomita kutoka jijini Dar es Salaam kulikojaa taasisi zote zinazosimamia sekta ya elimu, takribani kilometa 25 kutoka zilipo ofisi za Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, shule mbili za msingi ziko hoi kimiundombinu.
Ona mfano huu; shule ya wanafunzi 5078 ina vyumba vya madarasa 16 na matundu ya vyoo 20!
Wakati kanuni za Serikali zikitaka darasa kuwa na wanafunzi wasiozidi 45, katika Shule ya Msingi Mbande katika Wilaya ya Temeke Jijini Dar es Salaam, darasa moja lina wanafunzi 200.
Wingi wa wanafunzi hao kwa mujibu wa Mwalimu Mkuu, Dauden Mwakambiki unachangiwa na kukua kwa wakazi katika eneo hilo wakiwamo wakazi waliovunjiwa nyumba maeneo ya Shimo la Udongo, Mivinjeni na Kota za Reli.
‘’Bado tunawasiliana na viongozi wetu wa juu kuhakikisha tunazitatua hizi changamoto ikiwamo ya kuongezewa matundu ya vyoo, ‘’ anasema. 
Mwalimu wa Hisabati shuleni hapo Sara Peter, anasema analazimika kusahihisha madaftari zaidi ya 500.
“Tunafanya kazi ya ziada kwa kuwagawa wanaoelewa haraka na wanaochelewa kuelewa ili kuwasaidia kirahisi kwa kuwafundisha peke yao katika muda wa ziada ambao mwalimu mkuu anakuwa ameutenga, hilo linafanywa na walimu wote bila kuwalipisha wazazi kwa sababu hatuna budi kwenda sambamba na ongezeko la wanafunzi kama wanavyokuja, ”anasema.
Naye, Mwalimu wa taaluma, Kassim Imam anasema kuwa pamoja na mazingira haya magumu, kiwango cha ufaulu darasa la saba kinavutia. Katika matokeo ya mwaka2015 shule hiyo ilipata ufaulu wa asilimia 72 na kushika nafasi ya 22 kati ya shule 44 za Temeke Vijijini ikiwa na wastani wa 126, huku katika Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa ikiwa katika kundi la ‘bendi’ ya sita.

Shule ya Msingi Chamazi
Ukiona kwako kunafuka moshi, kwa mwenzako kunaungua. Kadhia ya Mbande ipo pia katika Shule jirani ya Chamazi yenye wanafunzi 3507, lakini ina vyumba vya madarasa 11 pekee.
Kwa mujibu wa Mwalimu Mkuu, Aniseti Shayo, vyumba hivyo vinapaswa kuchukua wanafunzi 311 pekee na ili kuwafundisha wamelazimika kuwagawa kwa awamu kwa siku, huku wengine wakisomea chini ya miti.
Anaeleza kuwa shule hiyo ina madawati 322 ambayo hayatoshi, lakini wanalazimika kuyatoa madarasani ili kuwe na nafasi kwa sababu yakiingia ndani wanaweza kukaa wanafunzi 45 tu.
“Umekuja kipindi hiki cha kiangazi angalau wanaweza kuvumilia jua huko nje, lakini wakati wa mvua hawasomi kabisa na hata pa kukaa kujikinga mvua hakuna tunalazimika kubanana madarasani, ”anasema Shayo.
Wakizungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotaja majina yao kwa madai kuwa watachekwa na wenzao, baadhi ya wanafunzi wa Mbande wanasema wakisoma nje ya darasa wanaelewa kuliko ndani kwa kuwa kuna joto kali.
Wanafunzi wa darasa la saba waliokutwa wakijisomea nje ya darasa katika shule ya Chamazi, walisema wanatumia muda mwingi kujisomea wenyewe hata wa mapumziko kutokana na kuwawia vigumu kuelewa darasani kutokana na kujazana.
“Eeh sema darasani kuna wanafunzi wengine, ungeenda uone, kuna joto halafu tumejaa hadi mlangoni. Huwa nahisi ipo siku nitazimia kwa joto, hata mwalimu akiwa anafundisha namhurumia, najisomea mwenyewe, nawashawishi wenzangu wengine tujisomee nje ya darasa, ”anasema mmoja wa wanafunzi shuleni hapo.
“Wakati mwingine ukikaa nyumbani na kusoma vitabu unaelewa kuliko ukija shule, tunasoma nje wakati mwingine jua kali, mvua ikinyesha hatusomi, ”anasema Mohammed Issa anayesoma shule ya Mbande.

Kauli ya Serikali
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki anasema kuwa anafahamu kinachoendelea katika shule hizo na juhudi za kuhakikisha tatizo hilo linatatuliwa zinafanyika.
Anasema kuwa kwa maeneo ya pembezoni siyo shule hizo tu bali zipo nyingi zenye uhaba wa vyumba vya madarasa na madawati, ingawa tatizo kati ya shule na shule huzidiana.
‘’ Kuna uhaba wa madarasa 461, ambayo thamani yake ni Sh. 11.198 bilioni , kiasi hiki cha fedha ni kikubwa, kulingana na fedha zilizotengwa kwa ajili ya Halmashauri za Jiji la Dar es Salaam, ambazo ni Sh. 2.367 bilioni zitakazotosha kujenga madarasa 95, ” anasema.

No comments :

Post a Comment