
Wengi walia, kuna operesheni hadi wa M10/-
Hali hiyo imelalamikiwa na wengi kwa madai kuwa ni mzigo usiobebeka kwa Watanzania walio wengi.
Uchunguzi uliofanywa na Nipashe umebaini kuwa hivi sasa, licha ya mabadiliko makubwa ya utoaji huduma kwenye taasisi hiyo yanayotokana na kuwapo kwa miundombinu inayowezesha kila mgonjwa kulala kwenye kitanda chake, bado kiasi cha fedha kinachotozwa kwa wagonjwa huwasumbua wengi kutokana na kutoendana na uwezo wao.
Katika uchunguzi wake, Nipashe imebaini kuwa baadhi ya upasuaji humlazimu mgonjwa kulipa hadi Sh. milioni 10. Kiasi hicho ni mbali ya gharama nyingine kama Sh. 50,000 za ufunguaji wa jalada.
Kadhalika, Nipashe imebaini pia aina nyingine nyingi za upasuaji huwa si chini ya Sh. 500,000, na vipimo kama CT-Scan na MRI vikihitaji fedha nyingi pia, cha juu kikiwa ni Sh. 400,000 (MRI). Wenye kupata nafuu ni wagonjwa wenye kadi za Bima za Afya.
Kwa kawaida, wagonjwa wote katika taasisi hiyo hutozwa gharama kulingana na hadhi yao miongoni mwa makundi makuu matatu: wagonjwa wa kawaida (maarufu kama ‘general’), wagonjwa wenye kadi za bima za afya na wagonjwa binafsi (maarufu kama ‘private’).
Wakizungumza na Nipashe mwishoni mwa wiki, baadhi ya wagonjwa walisema kutokana na gharama za huduma za matibabu MOI kuwa kubwa, ni wazi kwamba wapo watu huishia kuwa walemavu kwa matatizo ya mifupa yanayoweza kutibika kwa kuwa Watanzania walio wengi ni wa kipato cha chini.
Kwa mujibu Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), pato la Mtanzania katika robo ya pili ya mwaka 2015 lilikuwa Sh. 1,828,022, sawa na wastani wa Sh. 5,008 kwa siku.
“Uliza utaambiwa… hapa kuna upasuaji unaogharimu hadi Sh. milioni 10. Hii maana yake ni kwamba mgonjwa, ili ajihakikishie matibabu ya aina hiyo, lazima awe na fedha hizo na kiasi kingine cha ziada kwa ajili ya usafiri kutoka huko anakoishi na pia kwa ajili ya matunzo mengine pale anapolazwa kama chakula,” alisema mmoja wa wagonjwa waliokutwa hospitalini hapo mwishoni mwa wiki na kuuliza:
"Je, ni wangapi wanaoweza kumudu gharama za aina hiyo?
"Ni vyema Serikali ikaliangalia jambo hili."
Jesca Joe, mmoja kati ya mamia ya watu waliokutwa kwenye eneo la mapokezi kwenye taasisi hiyo, alimueleza mwandishi kuwa kadri aonavyo, hivi sasa MOI haina tatizo kubwa la utoaji wa huduma kwa sababu yeye ameshuhudia namna watumishi wake kama madaktari na wauguzi wanavyojituma na pia jinsi wagonjwa wanavyolazwa wodini.
Lakini Jesca alisema changamoto kubwa anazoziona sasa ni mrundikano wa wagonjwa na pia gharama kubwa za matibabu.
“Kwakweli watumishi wao wanajitahidi sana. Na wagonjwa hivi sasa hulala mahala pazuri… ila kuna matatizo mawili makubwa ambayo Serikali hii ya (Rais John) Magufuli inapaswa kuyatafutia ufumbuzi," alisema Jesca.
"Kwanza (ni) wingi wa wagonjwa na pili ni gharama kubwa za matibabu.”
Akieleza zaidi, Jesca alisema ni vyema Serikali ikaanzisha taasisi nyingine kama MOI kwenye hospitali nyingine kubwa nchini ili kupunguza idadi ya wagonjwa wanaofika MOI.
“Hili la gharama ndiyo muhimu zaidi. Hivi sasa hali inatisha. Wenye nafuu ni watu wenye hali nzuri kifedha kwa sababu gharama zinazotozwa kwa huduma nyingi huanzia laki mbili (Sh. 200,000)," alisema Jesca.
"Kwa mfano, kufungua faili peke yake Sh. 50,000, vipimo kama CT-Scan au MRI ndiyo balaa… na upasuaji huhitaji mamilioni ili kufanikisha.
"Serikali ya Rais Magufuli iangalie namna ya kutupunguzia mzigo huu, vinginevyo watu wa kawaida wataendelea kutaabika.”
Wakizungumza wakiwa ndani ya wodi ya Sewahaji namba 17, baadhi ya wagonjwa walisema wanaridhishwa na huduma zinazotolewa, huku baadhi yao wakiamini kuwa hatua ya Rais Magufuli kutembelea MOI baada ya kuingia madarakani na kusisitiza juu ya uwajibikaji huenda imechangia kuimarishwa kwa utoaji huduma.
Hata hivyo, walisema gharama zinachotozwa kwa wagonjwa kwa ajili ya mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na vipimo, upasuaji na dawa ni changamoto kubwa inayopaswa kushughulikiwa na serikali.
“Nilifikishwa hapa tangu Novemba 2015 baada ya kupata ajali ya gari. Kwakweli sijapata tatizo hapa wodini… ukitaka daktari anakuja mara moja.
Hata unapopangiwa kupata vipimo, unapelekwa kwa siku inayotakiwa," alisema Hashim Juma, aliyelazwa katika wodi hiyo ya Sewahaji.
"Changamoto kubwa ni gharama za matibabu. Ukiugua kama mimi ni lazima ndugu zangu wajipange vizuri ili kuhakikisha kwamba kila kitu kinakwenda vizuri."
Juma alisema alipofikishwa, ndugu zake walilipia Sh. 50,000 za kufungulia jalada na kiasi kingine cha Sh. 250,000 kwa ajili ya matibabu.
“Sifahamu ni kiasi gani kingine kimetumika kwa ajili ya matibabu yangu tangu nikiwa hapa. Kwa kweli ni gharama za juu kidogo, lakini huwezi kulinganisha thamani yake na huduma bora ninazopata.
"Binafsi nimeridhishwa sana.”
MKURUGENZI AFAFANUA M10/-
Akizungumzia malalamiko ya baadhi ya wananchi kuhusiana na gharama kubwa za matibabu katika taasisi yake, Mkurugenzi wa MOI, Dk. Othman Kiloloma, alisema inawezekana gharama zikaonekana kuwa za juu kwa badhi ya watu, lakini ukweli ni kwamba kwao ni huduma za kipekee kwa wananchi, na tena kwa gharama nafuu zaidi.
Alisema MOI ni taasisi ya umma inayotegemewa na taifa zima kuhusiana na masuala ya mifupa na hutoa huduma nyingi za kipekee na kwa gharama nafuu maradufu kulinganisha na hospitali nyingine.
Akieleza zaidi, Dk. Kiloloma alisema vifaa tiba wanavyotumia hununuliwa kwa gharama kubwa kuliko gharama wanayowatoza wananchi na ushahidi kuhusiana na hilo uko wazi kwa sababu gharama za baadhi ya huduma wanazotoa huwa ni za juu maradufu katika hospitali nyingine nchini.
Akitoa mfano, Dk. Kiloloma alisema kifaa kimoja cha kuunganisha paja hukinunua kwa dola za Marekani 500 (zaidi ya Sh. milioni moja), lakini wao hutoa huduma hiyo kwa kuwatoza wagonjwa Sh. 350,000 na kati ya
fedha hizo, Sh. 250,000 huwa ni kwa ajili ya upasuaji na Sh. 100,000 kwa ajili ya kifaa hicho walichokinunua kwa dola 500.
Dk. Kiloloma alisema kuwa kwa wagonjwa wa kundi la ‘private’, gharama ya upasuaji wa paja huwa ni Sh. 800,000 hata hivyo.
“Gharama hii ni ya chini sana ukilinganisha na gharama za huduma hii katika hospitali nyingine binafsi ambazo hutoza kuanzia Sh. milioni mbili,” alisema Dk. Kiloloma.
Mkuu huyo wa MOI alisema mara zote, nia yao ni kusaidia wananchi wa hali ya chini ambao huwa tayari hata kuwatibu bure, lakini changamoto iliyopo ni gharama halisi za vifaa tiba ambavyo huvinunua nje ya nchi kwa bei ghali.
“Hata hivi viwango tunavyotoza ni vya chini sana ukilinganisha na huduma halisi. Tunawaomba wananchi watuelewe,” alisema Dk. Kiloloma.
Aidha, mkurugenzi huyo alisema ni kweli kuna upasuaji unaomhitaji mgonjwa kulipa Sh. milioni 10, ambao ni ule unaohusisha kubadilisha nyonga kwani matibabu hayo huhitaji vifaa ambavyo huuzwa ghali zaidi.
Alisema matibabu hayo ya nyonga ndiyo hutozwa kwa gharama kubwa zaidi na kwamba, kiasi cha Sh. milioni 10 ni cha chini mno kulinganisha na gharama halisi ambazo MOI huzibeba.
Akifafanua, Dk. Kiloloma alisema vifaa peke yake kwa ajili ya kufanikisha matibabu ya nyonga huuzwa kwa dola za Marekani 15,000 (sawa na Sh. milioni 32).
“Kwa bahati mbaya sana, matibabu hayo hayapatikani katika hospitali binafsi yoyote hapa nchini… kama siyo MOI, maana yake mgonjwa hulazimika kwenda nje ya nchi ambako gharama za matibabu huwa kubwa zaidi,” alisema Dk. Kiloloma.
Aidha, Mkurugenzi huyo alitoa mifano ya gharama nyingine nafuu wanazotoza kuwa ni pamoja na tiba ya upasuaji na kuunganisha goti ambayo mgonjwa hutakiwa kulipia Sh. milioni sita wakati katika hospitali nyingine binafsi, huduma hiyo hutozwa Sh. milioni 18.
Alisema gharama nyingine kwa wagonjwa huwa ni ufunguaji wa jalada ambayo ni Sh. 50,000 huku matibabu yote kwa ujumla yakiwa ni Sh. 250,000, bila kujali uzito wa tatizo au muda atakaotumia mgonjwa kwenye taasisi hiyo kupata matibabu.
HOSPITALI BINAFSI DAR
Uchunguzi zaidi uliofanywa na Nipashe katika baadhi ya hospitali kubwa binafsi jijini Dar es Salaam umebaini gharama za baadhi ya matibabu ni kubwa maradufu kulinganisha na MOI.
Katika hospitali moja (jina tunalihifadhi), mwandishi alielezwa kuwa gharama za matibabu yoyote yale yanayohusiana na mifupa huanzia Sh. 500,000, achilia mbali gharama za kumuona daktari na za kufungua jalada.
Katika hospitali nyingine (jina tunalo), gharama za kumuona daktari kwa mara ya kwanza ni Sh. 40,000 na baada ya hapo, mgonjwa hulazimika kulipa gharama za vipimo, dawa na kitanda, achilia mbali upasuaji wenyewe ambao huhitaji fedha nyingi zaidi.
“Hizo ni gharama zetu za awali baada ya daktari kumuona na kufanyiwa vipimo. Malipo zaidi yatategemea ukubwa wa tatizo na matibabu atakayopata mgonjwa,” alisema mfanyakazi wa hospitali moja kubwa jijini Dar es Salaam aliyezungumza na mwandishi wa Nipashe ambaye aliulizia wastani wa gharama za mtu anayetaka kufanyiwa upasuaji wa goti.
Aidha, uchunguzi zaidi wa Nipashe umebaini kuwa gharama katika hospitali nyingi binafsi huwa kubwa maradufu kulinganisha na MOI kutokana na ukweli kuwa wengi wao huwa hawana madaktari bingwa wenye ajira za kudumu.
Hospitali hizo hukodi wataalamu kutoka katika hospitali za umma kama taasisi ya MOI, baada ya kuingia nao mikataba maalum.
“Kuingia mkataba na mtaalamu kutoka MOI, Muhimbili na taasisi nyingine za umma huwa ni ghali sana kwa hizo hospitali, siyo jambo jepesi hata kidogo,” daktari mmoja wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili aliiambia Nipashe.
"Na hili huchangia kuongeza gharama za matibabu kwa wagonjwa wanaofika hospitali hizo kupata matibabu."
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments :
Post a Comment