Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Tuesday, February 16, 2016

Wanafunzi wasoma chini ya mti Mtwara

Wanafunzi wa shule ya msingi Nanyati iliyopo katika halmashauri ya wilaya ya Mtwara wakiwa darasani wanaelimika.
Wanafunzi wa shule ya msingi Nanyati katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, wanasomea chini ya miti, wakikabiliwa na mvua na jua hata wakati mwingine kulazimika kufungwa kwa siku kadhaa mvua zinaponyesha mfululizo. 
Shule hiyo ipo umbali wa kilomita zipatazo 10 kutoka Mtwara mjini, changamoto zinazoikabili ni upungufu mkubwa wa madarasa na hasa katika kipindi hiki cha masika kinachoweza kuwafanya wanafunzi wakose masomo kwa kipindi kirefu. 
“Tupate viwanja vya mpira… madarasa… madawati…wanafunzi wengi wanakaa chini. Tunasomea chini ya mkorosho, uandikaji wetu ni wa matatizo. Mvua inapotunyeshea tunarudi nyumbani tunakosa masomo. Mwalimu akiugua tunafunga shule tunakosa kusoma. Hii inaniuma sana...” anasema Asha Selemani, mwanafunzi wa darasa la tatu, shule ya msingi Nanyati katika Halmashauri ya wilaya ya Mtwara.
Wanafunzi wa Nanyati, wanaiomba serikali iwatatulie changamoto hizo ambazo zinakwamisha safari yao ya kujipatia elimu kwa kupoteza muda mwingi hasa mvua inaponyesha.
 
Shule ya msngi Nanyati iko umbali wa kilomita zipatazo 10 kutoka Mtwara mjini, yahitaji kutatuliwa changamoto zinazoikabili hasa katika kipindi hiki cha masika kinachoweza kuwafanya wanafunzi wakose masomo kwa kipindi kirefu. 
Shule hiyo ilianzishwa mwaka 2013 ina wanafunzi 210 kuanzia darasa la awali hadi darasa la tatu na mwaka huu watakuwa na  darasa la nne, wanakabiliwa na changamoto lukuki ikiwamo vyumba vya madarasa. Ina chumba kimoja kinachotumiwa na wanafunzi wa darasa la pili huku wale wa awali na darasa la tatu wanasomea chini ya mti.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Shaibu Hoja, anasema changamoto nyingine zilizopo ni uhaba wa walimu. Shule hiyo ina walimu wawili wa serikali na mmoja wa kujitolea, hali inayochangia wanafunzi kukosa masomo inapotokea mwalimu mmojawapo amepatwa na dharura ya kutohudhuria kazini kwa muda fulani.
Changamoto nyingine, ni ukosefu wa vyoo, nyumba za walimu, ofisi za walimu na upungufu mkubwa wa madawati yaliyopo ni 26 huku shule inahitaji madawati 88.
Kwa kukosa madarasa, anasema wanafunzi wanakuwa katika mazingira magumu ya kupata masomo hasa kipindi cha mvua kwa sababu wanalazimika kukimbia na kwenda nyumbani kwao ili kujihifadhi.
“Shule ina madarasa matatu pamoja na la awali na kusababisha idadi ya madarasa manne. Kwa sasa shule ina chumba kimoja tu kilichokamilika. Ina maana wanafunzi wa madarasa manne watakuwa nje hawana mahala pa kusomea...” anasema na kuongeza:
 “Changamoto ya kukosa madarasa imechukua nafasi ya kwanza, kwa sababu wanafunzi wanasomea chini ya miti, wanasumbuliwa na mvua, jua kali, wanamulikwa na jua, wanaloa maji mvua inaponyesha na shule inafungwa siku hiyo hata siku tatu kama mvua inaendelea,” anaongeza.
Anaziomba serikali za kijiji na halmashauri ya wilaya kushughulikia kero hizo kwa haraka ili kuwaokoa wanafunzi hao kuondokana na vikwazo hivyo ili wajitafutie elimu katika mazingira rafiki.
Wananchi wa kijiji hicho, ambao nguvu zao kwa pamoja zimefanikisha ujenzi wa shule hiyo, wanaitaka serikali kuwasaidia kuboresha miundombinu ya shule na kupanua eneo lao kwa kuwahamisha wananchi wanaoishi kuizunguka shule hiyo.
“Serikali tunaiomba itujengee choo cha kudumu kwa ajili ya wanafunzi. Tulichonacho ni cha muda mfupi…pia itupatie walimu wa kutosha kwa sababu hatukuanzisha kwa ajili ya wanakijiji pekee,” anasema Issa Chonga.
Mwenyekiti wa Kamati ya Shule, Fidea Chiponde,  anasema shule ina mahitaji mengi ikiwamo walimu wanaohitajika wanne, madarasa matano, matundu manane ya vyoo na nyumba saba za walimu na changamoto nyingine ya ukosefu wa vitendea kazi.
Kimsingi bado hawajapata msaada kutoka serikalini ukiachilia mbali fedha Sh.milioni tatu kutoka halmashauri zilizotumika katika ujenzi wa darasa moja, ambalo hata hivyo halijakamilika, ukiwamo msaada uliotolewa na mbunge wa jimbo la Mtwara vijijini, Hawa Ghasia, aliyechangia mabati 100.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Tamimu Kambona, ambaye pia ni Ofisa Elimu msingi, akizungumzia changamoto za shule, anasema kwamba tatizo lililokwamisha ujenzi wa madarasa linatokana na kuwekeza nguvu nyingi katika ujenzi wa maabara, uliotiliwa mkazo na mkuu wa mkoa ili kutekeleza agizo la Rais mstaafu wa awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete.
Anasema juhudi zinafanyika katika kutekeleza ujenzi wa shule hiyo, kwa bajeti ya mwaka 2015/2016 pamoja na ujenzi wa vyoo unaotegemewa kutekelezwa kupitia wafadhili mbalimbali.
“Makusanyo ya mwaka jana mengi yalielekezwa katika ujenzi wa maabara, lakini nafikiri kwa mwaka huu nguvu yetu tutaielekeza huko baada ya kukamilisha maabara...” anasema Kambona na kuongeza:
“Kuhusu suala la walimu ni kweli kuna walimu wawili. Na ikitokea mmoja ni mgonjwa ni tatizo.Tumeliona hilo kwa bahati mbaya mwaka 2015 Tamisemi haikutupatia mwalimu hata mmoja, lakini tunafanya juhudi mambo yaboreke,” anaongeza. 
Anasema kuwa, walishindwa kufanya uhamisho kwa wakati kutokana na kukumbwa na madeni ya fedha za uhamisho zilizofikia zaidi ya Sh.milioni 70, lakini kwa sasa madeni hayo yamelipwa na serikali, na uwezekano wa kufanya uhamisho upo.
Halmashauri ya wilaya ya Mtwara inasifika kwa kufaulisha wanafunzi hasa wa darasa la saba kwa kuongoza kimkoa katika matokeo ya mtihani wa mwaka 2015 kutokana na kufaulisha kwa asilimia 86.84 na kitaifa kushika nafasi ya 16.
Hali inachangia kuifanya ipande nafasi za juu ukilinganisha na takwimu za matokeo ya mwaka 2014 ilifaulisha kwa asilimia 71 na kuwa ya pili kimkoa na kitaifa kuwa katika nafasi ya 31.
Licha ya mafanikio hayo, serikali kupitia halmashauri hiyo zinatakiwa kufanya jitihada za ziada kuboresha miundombinu ya elimu vijijini ambako kwa kiasi kikubwa ni kikwazo kwa wanafunzi na shule kwa ujumla kupiga hatua za uhakika za maendeleo kitaaluma.
 Mwaka huu serikali ya awamu ya tano inayoongozwa ya Rais John Pombe Magufuli, imekuja na mpango wa kutoa elimu bure kwa shule za msingi na sekondari, kwa kutuma fedha moja kwa moja katika akaunti za shule ili kutatua matatizo ya shule hata kuwawezesha wanafunzi kusoma bila ya vikwazo.
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment