
Akizungumza katika mahojiano maalum na Nipashe juzi, Hamad ambaye aliwahi kushika nafasi za uwaziri alipokuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na pia kuwahi kuwa Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni kwa tiketi ya CUF kabla ya kuhamia ADC, alisema nchi wahisani, zinampendelea Maalim Seif.
Alisema nchi hizo zinampendelea na ndiyo maana waangalizi wa Uchaguzi Mkuu uliofutwa wa Oktoba 25, mwaka jana walidai ulikuwa huru na wa haki huku wakishindwa kukemea kitendo cha Maalim Seif cha kujitangazia ushindi wa zaidi ya asilimia 52 badala ya kusubiri kazi hiyo kufanywa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).
Akieleza zaidi, Hamad alisema Uchaguzi Mkuu uliofutwa ulijaa kasoro nyingi na hivyo ZEC iko sahihi kuitisha uchaguzi wa marudio utakaofanyika Machi 20.
Alisema ADC itashiriki kwa ukamilifu licha ya baadhi ya vyama, ikiwamo cha CUF, kuususia na kutaka majumuisho ya kura kwa uchaguzi wa awali yaendelee na mshindi kutangazwa.
Hata hivyo, CUF kupitia Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar), Nassor Ahmed Mazrui, imekanusha mara kadhaa madai kuwa Maalim Seif alijitangazia ushindi.
Maalim Seif aliwaambia waandishi kuwa matokeo waliyopata kutoka kwa mawakala wao karibu katika vituo vyote yalionyesha anaongoza kwa asilimia 52.47 na hivyo akaitaka ZEC ifanye uadilifu kwa kumtangaza mshindi halali wa uchaguzi huo.
Hata hivyo, Oktoba 28 Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, alitangaza kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi huo.
Tangu wakati huo, mgogoro mzito wa kisiasa umeibuka visiwani humo na kupelekea uamuzi wa CUF kususia uchaguzi huo wa marudio kwa kusisitiza kuwa ZEC iendelee na majumuisho ya kura na kumtangaza mshindi huku, CCM ikiunga mkono uamuzi wa ZEC na kujiandaa kwa marudio ya uchaguzi huo.
Jitihada za mazungumzo yaliyowahusisha CCM chini mgombea wake, Rais Ali Mohamed Shein na CUF iliyowakilishwa na katibu mkuu, Maalim Seif, yaligonga mwamba licha ya kufanyika kwa vikao nane kujadili hali hiyo, vikiwahusisha pia marais wastaafu wa Zanzibar Dk. Salmin Amour Juma, Ali Hassan Mwinyi na Abeid Amaan Karume.
Kufuatia hali hiyo, nchi za Umoja wa Ulaya (EU) na Marekani ambazo husaidia miradi mingi ya maendeleo, zimekuwa zikitoa matamko ya kutaka uamuzi wa wananchi kupitia sanduku la kura uheshimiwe kwa kuendelea na majumuisho ya kura ya uchaguzi wa Oktoba 25, kwa sababu ripoti za waangalizi wote wa ndani na wa kimataifa zilionyesha kuwa uchaguzi huo ulikuwa huru na wa haki.
Taasisi nyingine zilizotuma waangalizi katika uchaguzi wa Zanzibar na kutoa ripoti zilizoonyesha kwamba ulikuwa "huru na wa haki" ni Jumuiya ya Madola, Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Afrika Mashariki na pia taasisi ya uangalizi wa uchaguzi nchini (TEMCO).
Akielezea ripoti za waangalizi wa kimataifa, Hamad alisema hazina ukweli kwa sababu kulikuwa na kasoro nyingi kama ZEC walivyoeleza na kwamba, inashangaza kuona kuwa waangalizi hao hawazungumzii kujitangazia ushindi kwa Malim Seif na badala yake kudai kuwa uchaguzi ulikuwa “huru na wa haki”.
“Mimi naomba ma-donnor (wahisani) wasitutishie… naomba sana waendeleze ushirikiano. Kutengeneza miundombinu mizuri ya kupata demokrasia ya kweli wasishikilie (kwamba) lazima CCM iondoke madarakani, sio sahihi,” alisema.
Hamad aliongeza kuwa siyo sahihi pia kwa wahisani kukipendelea chama chochote bali ni kusaidia kuona kuwa chama kinachoshinda kinapewa haki hiyo kihalali.
“Mbona hawataki kuona kitendo cha Maalim Seif kujitangazia matokeo (ya ushindi) ni kosa kisheria na kikatiba? Kwanini wanakuwa na upendeleo?”. Alihoji Hamad.
Akieleza zaidi, Hamad alisema hata ZEC haiko huru kwa sababu miongoni mwa makamishna wake ni makada kutoka CCM, CUF na chama cha SAU.
“Hii tume imeundwa kwa mfumo wa kivyama. Ndani yake kuna wajumbe wa CCM, CUF na SAU, kwa hiyo tayari kuna tatizo. Hivyo sisi kusema kuwa uchaguzi ulikua huru na haki wakati tume yenyewe haikuwa huru na haki siyo sahihi hata kidogo.
"Waangalizi wa uchaguzi hawakutenda haki na walikuwa na upendeleo.”
Aidha, Hamad alieleza kuwa miongoni mwa kasoro zilizojitokeza Oktoba 25, na ambazo anaamini ni sababu mojawapo kubwa ya kurudiwa kwa uchaguzi huo, ni takwimu za matokeo ya uchaguzi zilizojaa utata katika baadhi ya vituo, na hasa Pemba.
Akitolea mfano, alisema kuna kituo kimoja kulikuwa na karatasi ya matokeo iliyoonyesha kuwa yeye alikuwa akigombea uwakilishi wakati siyo kweli.
“Kuna karatasi nyingine za matokeo zinaonyesha Hamad (yeye) amepata kura moja, Dk. Shein amepata kura moja, na wagombea wengine wamepata kura moja moja wakati Maalim Seif amepata kura 150," alisema Hamad.
"Kwenye matokeo ya jumla katika karatasi hiyo kwa chini kuna kura mia mbili na zaidi. Tunajiuliza, hizi nyingine zinatokea wapi? Kwa hivyo mapungufu yalikuwapo makubwa sana katika uchaguzi.
“Hao waangalizi niliwauliza, mbona nyinyi waangalizi sikuwaona Pemba? Nimewaona waangalizi wa ndani pekee, lakini wale waangalizi wa nje sikuwaona… mimi ni mgombea urais. Hakuna hata mmoja (waangalizi wa kimataifa) aliyekuja akasema Hamad tukae, na tuzungumze na wewe juu ya uchaguzi.”
MAGUFULI, HATMA UKAWA
Akizungumzia utendaji wa Serikali ya awamu ya tano chini ya John Magufuli, Hamad alisema inastahili pongezi kwa sababu Rais ameonyesha ujasiri mkubwa wa kupambana na ufisadi.
“Alipoanza, kuna watu walidhani ni nguvu za soda… lakini kila anachokisema amekuwa akikifanyia utafiti na kukitekeleza. Kinachotakiwa ni kwa mawaziri kuwa makini na kufanya utafiti wa kila jambo na kutoa nafasi kwa upande wa pili kabla ya kuchukua hatua,” alisema.
Ni muhimu Serikali ikasimamia vizuri manunuzi ya umma kwa sababu ndilo eneo lenye mianya mingi ya kuhujumu fedha za nchi, alisema Hamad, na kupendekeza njia mojawapo kuwa ni kujielekeza katika matumizi ya elektroniki katika masuala ya uuzaji na ununuzi.
Hamad aliitaka pia Serikali ya Magufuli iangalie kwa umakini eneo la uingiaji wa mikataba kwa kuwa mingi hufanyika kwa siri na kuliumiza taifa.
“Uwazi ni muhimu. Kwa mfano, ukienda Ghana, serikali ikitaka kukopa fedha lazima bunge liidhinishe. Sheria ya bajeti ikisimamiwa vizuri tunaweza kupunguza kasoro zilizopo.”
Kuhusiana na kishindo cha muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na NLD, Hamad alisema aliupinga umoja huo kitambo kwa sababu haupo kisheria na hadhani kama utadumu.
“Maisha ya Ukawa siyaoni kwa sababu haupo kisheria. Uhai wao nauona upo tete kwa sababu haupo katika misingi ya kisheria, labda sheria ikija kubadilika itakaporuhusu vyama kuungana inawezekana ukawa ukawa na manufaa mbele ya safari,” alisema.
SEHEMU YA MAHOJIANO NA HAMAD
SWALI: Je, huoni kwamba ushiriki wako katika uchaguzi wa marudio unaweza kukujengea tafsiri mbaya mbele ya umma, hasa wapinzani, kuwa labda unatumiwa kudhoofisha kambi hiyo?
HAMAD: Tupo katika mfumo wa vyama vingi. Na maana yake vyama vyote vimeandikishwa kwa mujibu wa sheria namba tano, na kila chama kina haki sawasawa na chama chengine, ama kiwe kikubwa ama kidogo mbele ya sheria kina haki sawa sawa na kila chama katika kujiandikisha kwake, kimesema shughuli kubwa kitakachofanya kisiasa ni pamoja na kushiriki katika kupata dola.
Na njia ya kushika dola ni moja tu, nayo ni kuingia katika uchaguzi. Hayo ndiyo madhumuni makubwa ya vyama vya siasa.
Anaetulaumu sisi, kwanza atulaumu je, tumekwenda kinyume cha matakwa ya sheria na katiba? Na kuacha kushiriki katika uchaguzi je, sheria yetu ndivyo inavyotuelekeza?
Sisi katika chama chetu, toka tulipoanzisha chama tuliamua kabisa hakuna kipindi tutasusia kujiunga au kushiriki katika chaguzi. Hayo ndiyo maamuzi yetu ya chama tuliyojiwekea toka mapema. Kwa hiyo siyo kweli kwamba ushiriki wetu wa uchaguzi unategemea ridhaa ya chama kingine.
Kama tushiriki au tusishiriki, hapa ni uamuzi wa chama chetu. Ni wa kisheria na kikatiba na ndiyo dhumuni la kuanzishwa kwa chama chetu. Kwa hiyo anayesema tunatumiwa inategemea anajitazama kwa njia gani.
Kama wewe umegomea; je, tukikufuata wewe, mwengine anayeingia asiseme kuwa tunatumiwa kuwa tugomee kwa sababu kuna vyama vimekataa na vinatumiwa kuwa vimenunuliwa na chama ambacho kimegomea?
SWALI: Kwa mtazamo wako kama miongoni mwa wagombea urais, unauzungumziaje uchaguzi wa Zanzibar wa Oktoba 25, 2015?
HAMAD: Kwanza sisi wenyewe binafsi tuliandika barua Oktoba 27 mwaka jana tukilalamika juu ya mapungufu makubwa yaliyopo ndani ya tume ya uchaguzi Zanzibar na hatua nzima ya kuendesha uchaguzi.
Hata hao waangalizi niliwauliza mbona nyinyi sikuwaona Pemba, nimewaona TEMCO, waangalizi wa ndani pekee lakini wale waangalizi wa nje sikuwaona na mimi mgombea urais.Hakuna hata mmoja aliyekuja akasema Hamad tukae na tuzungumze na wewe juu ya uchaguzi.
La pili, katika uchaguzi huo huo unaosemwa huru na haki, mimi nimegombea urais, katika karatasi za kura zimeandikwa Hamad anagombea urais lakini katika karatasi za matokeo zimeandikwa Hamad Rashid Mohamed ni mgombea uwakilishi kituo fulani na nimepata kura moja.
Mimi nagombea urais na siyo uwakilishi. Kuna karatasi nyingine za matokeo zinaonyesha Hamad amepata kura moja, Shein amepata kura moja, na wagombea wengine kura moja wakati Maalim Seif amepata kura 150.
Kwenye matokeo ya jumla katika karatasi hiyo chini kuna kura mia mbili na zaidi. Tunajiuliza, hizi nyingine zinatokea wapi? Kwa hiyo, mapungufu yalikuwapo makubwa sana katika uchaguzi na hasa kisiwani Pemba.
Tumeandika katika malalamiko yetu hata wale wawakilishi wetu (mawakala) waliwekwa nje, hawakuwa na haki yoyote na tukalalamikia yote na tukasema.
Baya zaidi, inakuaje mgombea mmoja anapata taarifa ya matokeo ya uchaguzi na akatangaza matokeo hayo kwa asilimia mia juu ya mia ya kuwa yeye amepata asilimia 52.47 huku mwenzake amepata asilimia 47.13? Je, sisi vyama vingine tuliogombea hatukuwapo na hakuna kura zilizoharibika?
Hayo ni masuala ambayo tuliyawasilisha katika tume na tukasema hii tume ina upendeleo kwa sababu imeundwa kwa mfumo wa kivyama.
Ndani yake kuna wajumbe wa CCM, CUF na SAU kwa hiyo tayari kuna tatizo katika muundo wa tume. Tulilalamikia hilo, kwa hivyo sisi kusema kuwa uchaguzi ulikuwa huru na haki wakati tume yenyewe haikuwa huru na haki hilo siyo sahihi hata kidogo.
Na hilo napingana kabisa na waangalizi wa uchaguzi, hawakutenda haki na walikuwa na upendeleo. Lakini baya zaidi, hata matokeo aliyoyatoa Maalim Seif hayakuwa sahihi kwa sababu ukichukua mahesabu aliyochukua yeye, maana yake ukishasema majibu ni asilimia 100, je, majimbo ambayo hayajahesabiwa, hiyo asilimia 100 inatokea wapi?
Sasa angesema asilimia 100 kwa kura ambazo zimeshahesabiwa ningemfahamu lakini anaposema asilimia 100 atangazwe kuwa mshindi wakati majimbo hayajamaliza kuhesabiwa, unajuaje kama umeshindwa?
Na cha ajabu zaidi, Maalim Seif alisema kuwa ameshinda kwa kura 17,000 wakati katika historia ya uchaguzi wa Zanzibar, tokea ukoloni hadi leo, hakuna chama kilichoshinda zaidi ya kura 5,000. Kwa hiyo hizo namba hazipo. Lazima zimetengenezwa na tunasema kuwa uchaguzi haukuwa wa haki.
SWALI: Je, kwa uzoefu wako katika siasa nchini, unaamini kwamba ipo siku chama cha upinzani kikishinda uchaguzi Zanzibar kinaweza kuachiwa kitawale?
HAMAD: Kwanza kuna kosa moja ambalo linafanyika sana. Vyama vyote ni vyama vya siasa. Kuna chama ambacho kipo madarakani na kuna chama ambacho hakipo madarakani.
Tulipoanza uchaguzi, tokea ukoloni tulipoanza, vyama ni hivi hivi vikishindana kwa uchaguzi unapata asilimia hii, unapata asilimia hii, Waziri Mkuu wa kwanza Mwalimu Shamte, alikuwa katika chama cha upinzani na alipata viti vitatu tu, akashirikiana na ZNP, akapata serikali. Kwa hiyo, kwanza tofauti hizi kura chache ni za kawaida.
Lakini la pili, tunapofanya uchaguzi siyo suala kuwa chama cha upinzani kinashinda au hakishindi.
Mimi nasema ridhaa ikipatikana safi, tukawa na tume huru ya uchaguzi, chama kitakachoshinda kitapata madaraka yake. Mimi ndivyo ninavyoamini. Lakini kuna dhana lazima kishinde chama cha upinzani.
Hakuna hiyo, duniani kuna chama kinachoingia katika uchaguzi, aidha kiwe cha upinzani au siyo cha upinzani, alimradi kiwe kimeshinda, (basi) kinapata haki yake. Nitoe mfano Malawi alishinda Dk. Muluzi (Bakili), alikuwa mpinzani na alipoingia madarakani akabadilika, akaonekana tatizo kuliko chama tawala.
Au Zambia ilivyokuwa chini ya Chiluba. Kwa hiyo, dhana hii mimi nataka tuiondoe kabisa. Upande wa upinzani hakuna malaika, sote tunaingia katika uchaguzi, inategemea na kujiamini kwa wananchi nani watampa kura. Mbona majimbo mara hii ya uchaguzi wapinzani wameshinda na mbona wameachiwa?
Maana katika uchaguzi siyo lazima kushinda urais. Sisi tunasema hakukuwa na usawa. CUF na CCM walipata ulinzi mkubwa zaidi, walipata fedha nyingi, lakini sisi hadi leo tunaingia katika uchaguzi hatuna fedha.
Tumeshamalizikiwa kabisa, lakini tumekubali kuingia kwa hicho hicho kidogo tulicho nacho na kupita nyumba kwa nyumba.
Tunakwenda katika hali ngumu sana, sasa hiyo peke yake ndio uhalisia kuwa je, kama chama cha upinzani kitashinda na usawa utapatikana?
Na ndiyo maana nikasema ili kuhakikisha chama cha upinzani kinashinda au kitashindwa, ni lazima kuwe na tume huru ya uchaguzi, kwanza wajumbe wake wasiwe wanasiasa.
Wawe ni wataalamu ambao wanaweza kusimamia uchaguzi. Tume iwe na rasilimali ambayo haitegemei serikali. Wawe na mfuko wao katika mfuko wa hazina.
Wawe na watumishi wao maalum wa kusimamia uchaguzi ili wawe na heshima na tume isiwe na mamlaka ya mwisho, mamlaka ya mwisho iwe ni mahakama. Yakipatikana hayo ndiyo mimi utaniuliza mbona chama cha upinzani kimeshinda lakini hakijapewa madaraka.
SWALI: Je, unadhani ni kitu gani kifanyike ili kuondoa mgawanyiko wa Wazanzibari kiitikadi unaodaiwa kukwaza mambo mengi ya maendeleo visiwani humo?
HAMAD: Kwanza Zanzibar tuna kasoro moja kubwa sana. Kila kitu tumekifanya ni siasa. Hata mtu ukitaka kufanya jambo la maendeleo itaingizwa siasa.
Tupunguze hilo jambo. Tuangalie suala zima la kiuchumi. Jambo la pili la ni kuacha kuombaomba na kutegemea misaada kutoka kwa wafadhili.
Kubadilisha mfumo wa kufanya kazi kwa kuacha kufanya kazi kwa mazoea. Lazima utendaji kazi ubadilike na siyo kukaa ofisini kula urojo na chauro.
Kuzitumia rasilimali za Zanzibar, sisi hatuzitumii rasilimali hizo. Samaki tulionao sisi ni wengi, tukizitumia rasilimali vizuri, tabia ya kufanya kazi kwa uvivu itaondoka na kila mtu atakuwa na hamu ya kufanya kazi.
SWALI: Je, unadhani kwamba chama chako cha ADC kinaweza kuwa mbadala wa kweli wa CCM na CUF katika kuongoza visiwani Zanzibar… na hasa baada ya mgongano wa wazi uliojitokeza hivi karibuni baina yako na viongozi wengine wa ADC kuhusiana na suala la Zanzibar?
HAMAD: Lazima bila ya kuwapo na utatuzi huwezi kutatua matatizo. Na lazima kuwe na utatuzi na ndiyo maana sisi hatuna uadui na CCM wala CUF. Hatuna ubaguzi na mtu yoyote na nimeanzisha vikundi vingi vya Vicoba bila ya kubagua chama au dini au ukabila. Sisi siasa zetu zaidi zipo kiuchumi.
Na ukitaka kuingia katika uchumi, mvutano wa kisiasa utabadilika. ADC tutajitahidi kufuatilia mgawanyo wa kodi katika serikali ya muungano ili mpangilio ujulikane.
Je, Zanzibar wanapata kiasi gani na bara wanapata kiasi gani? Fedha ikipatikana na ikapangiwa mipangilio mizuri ya matumizi, nakuhakikishia kabisa mvutano huu wa kisiasa utaondoka.
Lazima wananchi uwafanye wawe na shughuli za kiuchumi. Uhalifu utaondoka, tofauti za kisiasa itaondoka na madawa ya kulevya yataondoka.
SWALI: Je, leo hii ukikutana na Dk. Shein utamshauri mambo gani matatu muhimu kwa ustawi wa Zanzibar kisiasa, kiuchumi na kijamii?
HAMAD: Dk. Shein asimamie amani na utulivu na asiwe analisimamia jambo hilo kisiasa. Alisimamie kikatiba na kisheria. Siyo mwingine anafanya kosa, yule anaachiwa na mwingine anakamatwa.
Asiwe na ubaguzi katika hilo. Asimamie vyombo vya sheria na vyombo vya kutoa haki vizuri ili haki iweze kutendeka. Ijapokuwa anafanya hivyo, lakini ufanyaji wake ulikuwa unatiwa dosari na baadhi ya watu wake.
SWALI: Na je, ukikutana na Maalim Seif, utamshauri mambo gani matatu yaliyo muhimu kwa nia ya kuikwamua Zanzibar kutoka kwenye tishio la kutengwa na jumuiya ya kimataifa?
HAMAD: Maalim Seif atangulize matatizo ya wananchi na siyo matatizo yake binafsi. Akubali ukweli, ashukuru kwa yale ambayo Mungu amempangia na mimi namshukuru sana, baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana aliweza kuwatuliza watu watulie. Hivyo hivyo, anatakiwa afanye pia kwa wahisani ili nchi ibaki salama.
Wajenge mfumo mzuri wa demokrasia ili haya yaliyotokea yasitokee tena. Lazima awaambie wafuasi wake wabadilike katika mitazamo yao ya kisiasa, waingie katika mawazo ya kujenga uchumi.
Waingie katika mfumo wa kutoka hapa kuingia hatua nyingine ya kuweza kujenga nchi na kuondokana na umasikini, maradhi na ujinga. Kufanya hivyo atakuwa ameiepusha nchi na chuki.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments :
Post a Comment