Written by zamko // 19/08/2012 // Habari //
JK awaumbua Lowassa, Membe,
na Mwandishi wetu
RAIS wa Tanzania Ndugu Jakaya Kikwete
RAIS Jakaya Kikwete amesema hajaliagiza Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kupigana vita na Malawi kwa sababu za mpaka wa Ziwa Nyasa kati ya nchi hizo mbili.
Kauli hiyo ya Rais Kikwete ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama imekuja siku chache baada ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe kuitaka Serikali ya Malawi kusitisha utafiti wa gesi na mafuta unaofanywa kwa ndege juu ya ziwa hilo.
Baada ya Membe kutoa onyo hilo, aliyekuwa Waziri Mkuu wa kwanza katika serikali ya awamu ya nne inayoongozwa na Rais Kikwete, Edward Lowassa alisema wakati Bunge la Bajeti lilipokuwa likiendelea na vikao vyake mjini Dodoma kwamba, jeshi lipo tayari kuingia vitani na Malawi, endapo nchi hiyo itakaidi agizo la kuziondoa ndege zinazofanya utafiti kwenye anga la Ziwa Nyasa.
Kikwete awakata maini
Katika kile kinachotafsiriwa na wachambuzi wa musuala ya siasa kuzikana kauli za Membe na Lowassa, Rais Kikwete alimhakikisha Rais Joyce Banda wa Malawi, kwamba Tanzania haina mpango wa kuingia vitani dhidi yao, na kusisitiza kuwa hizo ni chokochoko za wanasiasa na waandishi wa habari.
Rais Kikwete aliyekuwa kwenye mazungumzo na Rais Banda wakati wa kikao cha viongozi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliomalizika jana jioni nchini Msumbiji, aliwataka Wamalawi kuondokana na hofu ya vita.
“Nanakuhakikishia dada yangu na watu wote wa Malawi, kwamba hatuna nia wala mpango wa kuingia vitani… hatuna matayarisho ya jeshi wala jeshi halijasogea popote kwani hakuna sababu.
“Mimi ndiye kamanda mkuu wa majeshi, na sijapanga wala kutoa maelekezo ya vita, tuviachie vyombo vyetu vifanye kazi. Hebu tuvipe nafasi. Wanasiasa na waandishi wa habari wajiepushe na maneno yanayosababisha taharuki na chokochoko, hayana maana… waachie diplomasia ifanye kazi yake,” alisisitiza.
Rais Kikwete alisema kumekuwa na sintofahamu ya muda mrefu kuhusu mpaka huo, huku akibainisha kwamba maofisa wa Malawi na Tanzania wameanza kulizungumzia suala hilo kwa nia ya kulitatua kwa amani.
Naye Rais Banda alisema amefarijika baada ya kusikia kauli ya Rais Kikwete iliyomhakikishia kwamba hakuna vita, huku akieleza kuwa tishio la vita liliwasumbua wananchi wake na kuwaongezea mshikamano.
“Nimefarijika sana, suala hili limetusumbua mpaka Wamalawi wote wakaungana bila kujali tofauti zao… navishukuru vyombo vya habari vya Malawi kwa kuonesha uzalendo na ukomavu katika suala hili,” alisema Rais Banda.
Rais Kikwete na Banda walikutana jijini Maputo nchini Msumbiji kwenye kikao cha viongozi SADC ambapo Tanzania ilichukua Uenyekiti wa Kamati ya Siasa, Ulinzi na Usalama.
Awali nafasi iliyochukuliwa na Tanzania ilikuwa inashikwa na Afrika Kusini huku Uenyekiti wa SADC ukichukuliwa na Msumbiji kutoka kwa Angola nafasi watakazokuwa nazo kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Kwa mujibu wa Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi, Premi Kibanga, Rais Kikwete alirejea nyumbani jana akitokea Msumbiji.
Tamko la Membe na Lowassa
Wiki mbili zilizopita, Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama, ilisema majeshi ya Tanzania yapo tayari kiakili na kivifaa ikibidi kuingia vitani kutokana na mzozo wa mpaka wa Ziwa Nyasa kati ya Tanzania na Malawi.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Edward Lowassa alitoa kauli hiyo mkoani Dodoma, alipokuwa akizungumza na waandishi na habari na kusisitiza kuwa Tanzania inaomba isifike katika hatua hiyo, lakini ikibidi wanajeshi wetu wapo imara kutetea mipaka ya nchi hadi tone lao la mwisho la damu.
“Jeshi letu lipo tayari, na tumeridhika na utayari wao na ‘commitment’ yao. Sisi ni moja ya jeshi lililojiandaa vizuri sana na miongoni mwa majeshi mazuri duniani. Tunajivunia vijana wa Tanzania waliopo kwenye jeshi letu. Tupo imara kiakili, vifaa vya kisasa,” alisema.
Alisema kamati hiyo inaunga mkono kauli ya serikali iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, kwani ni sahihi inayoelezea msimamo wa Tanzania kuhusu jambo hilo.
Lowassa alisema kuwa wanategemea jambo hilo litamalizika kidiplomasia ndani kwa ndani ama ikibidi kuomba msaada wa watu wengine kusuluhisha kwa kuwa Tanzania na Malawi ni marafiki na ndugu.
“Watu waliopo mipakani ni ndugu, tusingependa kufika mahali kutokuelewana mpaka kuhusisha vyombo vya ulinzi na usalama, lakini kwa faida ya Watanzania tumepewa maelezo ya jeshi letu, tumeridhika kwamba ikibidi jeshi letu limejipanga vizuri sana.
“Watanzania wasiwe na shaka yoyote, wanajeshi wamejipanga vizuri na kwa uhakika na kama ilivyo ahadi yao, wapo tayari kulinda nchi yetu mpaka tone la mwisho la damu yao,” alisema na kuongeza kuwa kama wabunge, nao wameridhika na maandalizi ya jeshi, kwani wapo imara na timamu.
Alisema serikali haitaki kufika huko, kwani wakati wa vita ya Uganda mwaka 1978, wananchi waliumia na kwamba kama nchi, inafahamu athari za vita kiuchumi na kwa maisha ya binadamu.
“Hatutaki kufika huko kwani si jambo jema, ndiyo maana tunasema tumalize kwa njia ya mashirikiano na kwa mazungumzo ya kidiplomasia ya mawaziri wanaohusika ikishindikana tutafute msuluhishi,” alisema.
Mwaka 1978, Tanzania iliwahi kuingia katika vita na Uganda, baada ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Iddi Amin Dada, kuvamia sehemu ya Tanzania na kudai kuwa ni yao.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe naye alitoa tamko la serikali na kuzitaka kampuni zote zinazoendelea kufanya utafiti wa mafuta katika ziwa hilo kuondoka mara moja pamoja na Serikali ya Malawi kuheshimu mazungumzo yaliyofikiwa. Alisisitiza eneo linalobishaniwa katika ziwa hilo lipo Tanzania.
Alisema pamoja na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuzipiga marufuku ndege za utafiti za kampuni hizo, bado zilikaidi na ndege tano zilitua katika eneo la Ziwa Nyasa.
“Serikali ya Tanzania inapenda kuzionya na kuzitaka kampuni zote zinazoendelea na shughuli za utafiti katika eneo hilo zisitishe mara moja…,” alisema Membe na kuongeza kuwa, Serikali ya Tanzania iko tayari kulinda mipaka yake kwa gharama yoyote.
Alisema kwa kuzingatia nyaraka zilizotengenezwa na wakoloni wa Kiingereza mwaka 1928 na 1938, zinaonesha kuwa mpaka wa ziwa hilo upo katikati.
Alisema hoja ya Tanzania ina nguvu kulingana na sheria za kimataifa kwa vile tatizo kama hilo linafanana na mgogoro uliokuwepo kati ya Cameroon na Nigeria.
Source: Mzalendo.net
No comments :
Post a Comment