Wizara yashindwa kutoa milioni 500/- kwa ZMA
Na Mwinyi Sadallah
18th August 2012
18th August 2012
Wizara ya Fedha ya Zanzibar imeshindwa kuipatia Mamlaka ya Usafiri Baharini ya Zanzibar (ZMA) Sh. milioni 500 kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya kusimamia taratibu za usalama katika sekta hiyo.
Wizara hiyo iliyoko chini ya Waziri Omar Yussuf Mzee haijajibu maombi ya fedha ya mamlaka hiyo yaliyowasilishwa tangu mwezi Februari mwaka huu.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa ZMA, Abdalla Hussein Kombo, alimwandikia katibu mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, kuomba bajeti hiyo ili kurekebisha kasoro mbalimbali.
Katika barua yake, Kaimu mkurugenzi mkuu wa ZMA amebainisha mahitaji ya Sh 570.53 ili kukamilisha mahitaji yaliyoelekezwa na serikali kama hatua mahsusi za kuimarisha usimamizi wa usafiri na usafirishaji baharini.
Barua ya mamlaka ambayo gazeti hili limeiona, inaelezea kwamba imewasilisha maombi hayo baada ya kupokea agizo la Ofisi ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Kaimu mkurugenzi mkuu wa mamlaka hiyo ananukuu barua yenye Kumb. Na. BLM/15/MM/C.1/13 ya Januari 25, mwaka huu iliyotoka kwa katibu mkuu kiongozi, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee.
Katibu mkuu wa Wizara ya Fedha, uchumi na mipango, Khamis Mussa Khamis, ameiambia NIPASHE kuwa inawezekana wizara yao ilishindwa kutoa haraka fedha hizo kwa kuwa ziliombwa kipindi ambacho walikuwa kwenye matayarisho ya bajeti ya serikali.
Nyaraka zilizoonekana na gazeti hili zinaonyesha kuwa maagizo yaliyobainishwa na ofisi ya baraza la mapinduzi kwa utekelezaji wa mamlaka ya usafiri baharini ni pamoja na kutafuta jengo lenye nafasi na vitendea kazi vya kutosha, vikiwemo vifaa vya ukaguzi vinavyokwenda na wakati.
Maagizo mengine yaliyomo kwenye barua ya ofisi ya BLM, ni kupatikana wataalamu wa kutosha, wenye ujuzi, uzoefu na sifa stahiki katika fani za ukaguzi wa meli, ubaharia, usimamizi na udhibiti wa usalama wa abiria wanaopanda kwenye vyombo na kusomesha wachache waliopo.
Mengine ni kuwapatia wafanyakazi hasa wakaguzi na maafisa usalama wa meli mafunzo ya mara kwa mara ili kwenda na kasi ya mabadiliko ya teknolojia.
Maagizo mengine ni uongozi wa mamlaka kuanzisha muundo rasmi wa mamlaka, na mfumo wa utumishi utakaowezesha kuwalipa vizuri watendaji wake.
Kuandaa utaratibu mzuri wa kuelimisha wenye meli kufahamu majukumu yao katika biashara ya kusafirisha abiria na mizigo baharini; kununua meli zilizo nzima na zenye viwango vinavyokubalika na kuendesha usafiri unaozingatia sheria na kanuni.
Vyanzo vya habari vimeeleza kuwa mamlaka imeshaunda kamati ya wataalamu kwa ajili ya kuandaa kanuni ikiongozwa na Kapteni Msilimiwa Iddi Juma ambaye ni kaimu mkaguzi wa meli katika mamlaka hiyo.
Wajumbe ni Kapteni Saada Shafi, Kapteni King Chiragi (Msajili wa Meli SUMATRA), Skeikha A. Mohamed (Msajili Msaidizi wa Meli ZMA), Khalfan S. Omar (Idara ya Mipango katika wizara ya Miundombinu), Kassim Juma Othman (Mwanasheria wa Bandari Zanzibar), Hassan Ali Haji (Mwanasheria kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali) na Salma S. Omar atakayekuwa katibu wa kamati hiyo.
Taarifa zinasema kuwa kamati hiyo imeshindwa kufanya kazi kutokana na ukosefu wa fedha ambapo kazi yao ilihitaji Sh. milioni 70.
Miongoni mwa vifaa ambavyo mamlaka imeorodhesha kuvihitaji kwa bajeti waliyoiomba serikalini, ni boti kwa ajili ya shughuli za ukaguzi (Sh 194.4 milioni); kituo cha mawasiliano ya redio na vifaa vyake (Sh milioni 13), kifaa cha kupimia uzito wa chuma (Sh milioni 56.7), redio ya mawasiliano (Sh milioni 48.6), majarida ya masuala ya usafiri wa baharini (Sh milioni 24.3), jenereta moja (Sh milioni 10) na magari matatu (Sh milioni 153.9).
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment