Viongozi wa Jumuiya ya Uamsho kesho watapandishwa mahakamani kujibu mashtaka mbali mbali yanayowakabili kuhusiana na tukio la kutekwa kwa Sheikh Farid na kusababisha kutoweka hali ya amani nchini baada ya kutokea vurugu zilizosababisha watu wawili kuuawa,miundombinu na mali ya serikali na watu binafsi kuharibiwa
Sunday, October 21, 2012.
VIGOGO watano wa Uamsho wanashikiliwa na polisi na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani leo huku Jumuiya hiyo ikitoa waraka wa kuwataka Waislamu wadumishe amani.
Viongozi hao wako mikononi mwa polisi tangu juzi wakihojiwa mambo kadhaa likiwemo la kutoweka mmoja wao, Farid Hadi Ahmed ambaye ilidaiwa kuwa alikamatwa na polisi kwa siku nne.
Mbali na Farid vigogo wengine wa uamsho ambao wanahojiwa na polisi ni Amiri wa Uamsho, Sheikh Mselem Ali Mselem, Naibu wake, Azzan Khalid Hamdan, Mussa Juma na Hassan Bakari.
Mbali na Farid vigogo wengine wa uamsho ambao wanahojiwa na polisi ni Amiri wa Uamsho, Sheikh Mselem Ali Mselem, Naibu wake, Azzan Khalid Hamdan, Mussa Juma na Hassan Bakari.
Kamishna wa Polisi wa Zanzibar, Mussa Ali Mussa alisema jana kwamba wanawahoji msheikh hao na watawafikisha mahakamani leo iwapo wataona kuna mashitaka ya kujibu.
Katika hatua nyingine, Uamsho imetoa waraka kwenye misikiti ya Zanzibar wakiwataka Waislamu wawe watulivu na kuhudhuria kwa wingi mahakamani leo wakiwa na vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi.
Waraka huo uliosambazwa unasema hivi: “Kama hali ilivyo na mnavyosikia mnaombwa muwe watulivu na mufanye subra na leo (jana) hapo Msikiti wa Mbuyuni hapatakuwa na muhadhara si Adhuhuri wala Alasiri. Mnachoombwa na viongozi wenu muwe wavumilivu na watulivu hadi kesho (leo) mufike mahakamani bila ya fujo na muchukue kopi za vitabulisho vyenu vya Mzanzibari.
“Jingine ni kuwa msikae vikundi na mkawapa askari sababu, tunasisitiza amani na utulivu na Waislamu ni wenye kutii amri za viongozi wao. Tunasisitiza mani na utulivu pia subra na dua kwa wingi . Ukipata taarifa hii mjulishe na mwenzio toa kopi na uwape wengine. Wabillah taufq.”
Waraka huo ambao ulikuwa unasambazwa katika misikiti jana haukutiwa saini na mtu yeyote wala haukutaja umetolewa na nani.
Wakili wa Uamsho, Salim Tawfik alisema jana kuwa wateja wake watafikishwa mahakamani leo lakini akalaumu kwamba Polisi wamewahoji bila ya yeye kuwepo.
“Mimi nilikwenda polisi nikakuta Mselem anahojiwa nikataka kuingia wakanizuia, wakasema wataniita lakini hawakufanya hivyo,” alidai wakili huyo.
Hali ya Zanzibar imetulia lakini ulinzi wa polisi na askari wa vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wameimarisha ulinzi katika maeneo mbalimbali ya mji huu wakiwa wanazunguka na silaha mikononi.
Kwa siku tatu mji wa Zanzibar ulikumbwa na ghasia kubwa kwa askari kupambana na wananchi ambao walikuwa wakiandamana wakitaka Sheikh Farid aachiwe.
Chanzo: ZanzibariYetu
No comments :
Post a Comment