Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ameuagiza uongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo kuzuia matumizi ya jengo la Makumbusho kuu ya Zanzibar baada ya kupata athari za kubomoka jana usiku…
Maalim Seif ametoa agizo hilo baada ya kutembelea na kuangalia maharibiko yaliyotokea baada ya jengo hilo kubomoka sehemu ya upande wa Ngome Kongwe na kusababisha hasara kubwa.
Hata hivyo Makamu wa Kwanza wa Rais ameelezea haja ya kulifanyia matengenezo jengo hilo ili kutunza historia ya Zanzibar na hifadhi ya Mji Mkongwe ambao ni urithi wa Kimataifa.
Akizungumzia hali hiyo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar Mhe. Said Ali Mbarouk amesema jengo hilo limepata athari hiyo wakati likiendelea kufanyiwa ukarabati. Amesema baada ya kuona athari zilizojitokeza hapo kabla, waliamua kulifanyia ukarabati kwa kuanza na hatua ya uezekaji, lakini mvua zinazoendelea kunyesha zimekuwa zikipelekea jengo hilo liendee kuvuja na kupelekea kubomoka sehemu hiyo.
Amesema kutokana na athari hiyo, wameamua kuitisha kikao ili kutathmini hasara iliyopatikana na kutokana na uharibifu huo. Mhe. Mbarouk amefahamisha kuwa baada ya kikao hicho watashauriana na washirika wa maendeleo wakiwemo mradi wa MACEMP uliokuwa ukisaidia kulifanyia ukarabati jengo hilo pamoja na majengo mengine ya kihistoria, ili waweze kuendeleza ukarabati huo.
Jengo la Makumbusho kuu la Zanzibar ni miongoni mwa majengo muhimu sana ya kihistoria ambapo inasemekana hata umeme ulianza kuwaka katika kituo hicho katika eneo zima la Afrika Mashariki.
Chanzo: ZanzibariYetu
No comments :
Post a Comment