Written by Stonetown (Kiongozi) // 23/12/2012
Katika harakati zangu za hapa na pale nimefikia pahala nikaona ipo haja ya kuanzisha jamvi la hoja tete hapa Mzalendoni lijulikanalo kama ‘Goya la mzalendo’. Katika jamvi hili nitakuwa nikizungumza mada tete na zenye mushkla katika jamii ili kuweza kupata taswira halisi ya fikira za wasomaji juu ya mada hizo nitazoziabiri kwa upana katika kijamvi hiki. Naishukuru mzalendo kwa kunipa kijikataa cha kuchapishia makala hizi. Shukran.
Wiki hii ‘Goya la mzalendo’ litaabiri na kutathmini kwa mapana faida za Muungano kwa Zanzibar na hasara za kuukata kwake iwapo wazanzibari wataamua kufanya hivyo. Mada hii inakuja mahali muafaka ambapo siku za hivi makaribuni tu tutaweza kuupata msimamo wa jumla wa maoni ya watu wa Zanzibar juu ya Muungano upi wanaoutaka.
Wakati kijungu hiki kikikaribia kuepuliwa baada ya kupwaga kwa muda sasa, kuna kila dalili kuwa Wazanzibari walio wengi hawaridhishwi na muundo wa Muungano uliopo, na wengine wengi wanasema kuwa hawautaki kabisa kabisa, yaani kwa jina maarufu watu hawa huitwa ‘Tuachiwe tupumuwe’.
Mungu ndie kadiri, tujaalie ije iwe hivyo. Yaani wenzetu wa bara waseme ‘haya tunawaachia Mupumuwe’, nyie kwenu, na sie kwetu’. Hali hii bila shaka kwa sasa itaonekana ya faraja sana lakini tukiangalia kwa upana kuna athari kubwa kuliko faida ya kuachwa ‘tukapumuwa’. Nasema kwa kiasi kikubwa, Muungano una faida nyingi kwa Zanzibar. Na kila lenye faida nyingi na hasara haiwi ndogo kimaumbile. Kama hujui waulize wafanya biashara juu ya hili.
Moja ya faida kubwa ya Muungano kwa Zanzibar ni vile kuachiwa tukajenga magorofa kule bara na kuumiliki uchumi wa kule ambao kwa asilimia kubwa umo mikononi mwa Wazanzibari. Hii ni faida kubwa ya Muungano kwani Wazanzibari wamenufaika sana kibiashara kule kuliko hata walivyokuwa kwao visiwani. Sasa kabla ya ‘kupumuwa’ wanapaswa hili walitazame upya kwanza.
Faida nyengine ni ile hali ya kuchanganya damu na wenzetu wa bara na kuunga udugu. Leo hii kwa sababu ya Muungano Mzanzibar kaowa Tabora, Shinyanga na kila pahala. Na kawaida unapofunga ndoa unajenga udugu wa kudumu baina ya kaya hizo. Hii nayo tusiipuuze hata kidogo ni moja kati ya faida kubwa kwa sasa.
Kwa upande mwengine Muungano, umechangia kwa kiasi kikubwa kuiweka salama Zanzibar. Tukumbuke kuwa Mapinduzi ya mwaka 1964, yaliyomuondoa Sultani, ysingeiacha Zanzibar salama. Zanzibar baada ya Mapinduzi ilikuwa na maadui wengi, kiasi kama si Muungano ingepinduliwa mara kwa mara na kukabiliwa na matatizo makubwa ya uvunjifu wa amani. Kwa sasa Zanzibar haiwezi kupinduliwa kwani si nchi yenye mamlaka kamili. Rejea kesi ya 1997 ya viongozi wa juu wa CUF walioshtakiwa kwa uhaini.
Zanzibar ina nafasi kubwa ya ushiriki katika vyombo vya kutunga sheria. Kama utaangalia kwa utulivu zaidi utaona kuwa ni Wazanzibari tu wanaopata kuingia baraza la Wawaikilishi na Bungeni, wakati bara wanapata haki moja tu ya hayo. Muungano umeijengea mazingira mazuri Zanzibar ya kujiamulia mambo yake na kujiletea maendelea kwni wana uwakilishi mkubwa katika vyombo vya sheria kuliko hata bara. Dogo hili?
Tugeukie Michezo na burudani. Ushiriki wa Zanzibar katika michezo kama mpira wa miguu umeipatia faid kubwa Zanzibar kuliko bara. Kwani hakuna mcheazji yoyote duniani anaechezea timu mbili za Taifa ukitoa Mzanzibari. Mfano mzuri ni akina Nadir, Agrrey, Mcha nwachezaji wetu wengi wa Timu ya Taifa, yaani heroes. Wote wanachezea timu mbili za Taifa na kuimba nyimbo mbili tafauti za Taifa. Hii ni historia katika dunia, haijapata kutokea isipokuwa kwetu chini ya Muungano huu.
Isitoshe, kutokana na Muungano Mzanzibari na Mbara kwa pamoja wanauwezo wa kuingia nchi zote mbili bila vikwazo wala pingamizi. Ingekuwa si Muungano suali hili lingehitaji ghrama na vitambulisho kadhaa kwa Raia wa nchi moja kuweza kusafiri kwenda sehemu nyengine ya nchi.
Kwa hivyo pamoja na kuwepo kwa kasoro ndogo ndogo katika Muungano kama vile kuchaguliwa Rais Dodoma (ni kasoro ndogo tu), kutozwa ushuru mara mbili bandarini bara, kupata mgao mdogo wa fedha, kutokuwa na dhamana ya wizara nyeti na Muhimu kwa Zanzibar ni mambo madogo tu hayo. Lakini hasara ya utokuwepo kwa Muungano ni kubwa zaidi.
Zanzibar nje ya Muungano, haiwezi kusimama bila Ubaguzi kama alivyosema Baba wa Taifa, Nyerere. Nje ya Muungano wazanzibari wangebaguana tu, kukawa na huyu ‘Mpemba, na huyu ni Muunguja, kwani dhambi ya Ubaguzi ni sawa na kula nyama ya mtu’. Tungebaguana tu. Pia Sultani angerudi tena visiwani kama si Muungano. Kwa hivyo haya ni mambo ambayo mzanzibari lazima ayafikirie kabla ya kutaka aachwe apumuwe ‘Majuto ni mjukuu’.
Nakunja jamvi, na goya langu!
Zanzibar nje ya Muungano, haiwezi kusimama bila Ubaguzi kama alivyosema Baba wa Taifa, Nyerere. Nje ya Muungano wazanzibari wangebaguana tu, kukawa na huyu ‘Mpemba, na huyu ni Muunguja, kwani dhambi ya Ubaguzi ni sawa na kula nyama ya mtu’. Tungebaguana tu. Pia Sultani angerudi tena visiwani kama si Muungano. Kwa hivyo haya ni mambo ambayo mzanzibari lazima ayafikirie kabla ya kutaka aachwe apumuwe ‘Majuto ni mjukuu’.
Nakunja jamvi, na goya langu!
Chanzo: Mzalendo
No comments :
Post a Comment